Umbali wa takribani kilomita 196 kutoka jijini Dar es Salaam hadi Morogoro. Ndiko Mwanaspoti lilisafiri kwenda kuisaka historia ya mmoja wa mabeki hodari hapa nchini, Dickson Job.
Safari ya Mwanaspoti inafikia kwa mama mzazi wa Job, Faraja Mwakabeta, ambaye anasema haikuwa kazi rahisi kwa mwanaye huyu kutimiza ndoto yake kwani amemsumbua sana hasa katika masuala ya masomo.
Kitasa huyu anayetambulika kwa jina la utani la 'Big Brain Defender' (beki mwenye akili kubwa), alianza kujulikana alipochaguliwa kuichezea Serengeti Boys (Timu ya Taifa ya vijana ya U-17 ambayo ilishiriki fainali za Mataifa ya Afrika (U-17) 2017 nchini Gabon) akiwa na klabu ya Mtibwa Sugar kabla ya kutua Yanga SC.
Akiwa Yanga, Job ameiwezesha klabu hiyo kushinda mataji yote sita katika misimu miwili iliyopita (mawili ya Ligi Kuu Bara, mawili ya ASFC na mawili ya Ngao ya Jamii). Pia aliifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo huku msimu huu akiifikisha hatua ya makundi la Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 25 ya kuikosa hatua hiyo na ameifikisha robo fainali ya CAF-CL akiwa moja ya nguzo muhimu katika kikosi cha timu ya Wananchi.
Mwanaspoti linaamini kuna mengi umeyasikia na mengine hujayasikia kuhusu Job. Hapa, mama Job anafunguka mengi kuhusu mwanaye tangu utotoni hadi sasa akiwa ni mmoja wa nyota muhimu kwenye kikosi cha Wanajangwani hao na nahodha msaidizi baada ya Bakari Mwamnyeto.
MAMA ANAFUNGUKA
Baada ya Mwanaspoti kupata nafasi hiyo ya kufanya mahojiano na mama Job, anaanza kwa kujitambulisha.
"Majina yangu halisi naitwa Faraja Mwakabeta, ni mama mzazi wa Dickson Job ambaye ni mtoto wangu wa kwanza. Nimejaaliwa kupata watoto wawili na wa pili ni dada yake, Diana, ambaye muda mwingi anamsisitiza dada yake huyo kusoma kwa bidii na anampenda sana mdogo wake na kila likizo lazima aende kwa kaka yake."
Kuhusu kipaji cha Job anasema, "Dickson alianza kuonyesha kupenda soka tangu akiwa mdogo sana, miaka mitatu. Kila alipokuwa anacheza, alipenda zaidi michezo inayohusu mipira."
"Baada ya kuanza kuonyesha hilo, baba yake naye akawa anamfuatilia kwa karibu na akaanza kumnunulia mipira ili afurahi, nguo zake nyingi alipokuwa mdogo zilikuwa ni jezi mbalimbali."
ALIANZAJE SOKA
Mama Job anasema baba yake alianza kumtabiria ipo siku atacheza soka. Hata hivyo, hakujua hilo (kipaji chake) litakuja kutokea na kabla hata ya kufikisha mwaka, alikuwa akienda uwanjani na baba yake huku akiwa na nepi kwenye mfuko kwa ajili ya kumbadilisha.
"Tulikuwa tunamnunulia sana jezi namba tano bila kujua tunamtabiria na alipoanza kukua akawa hashikiki kuhusu mpira jambo ambalo mimi sikulitaka kabisa kwani niliona hatasoma.
"Alipokuwa darasa la tatu, alianza kusifika kwa kucheza vizuri lakini sikufurahia kwa kweli na alipofika la nne alikuwa akiokota mipira (ball boy) katika mechi kubwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro," anasema mama Job na kuongeza alikuwa mtoto mtundu na mgomvi mgomvi.
"Dickson alikuwa mtoto mtundu kidogo na ugomvi ugomvi wa hapa na pale kama ambavyo baadhi ya watoto wengine walivyo wakiwa wadogo. Hata hivyo, kadiri anavyokua, alibadilika, niseme kwa mara ya mwisho kumwona anagombana na wenzake labda alipokuwa darasa la tatu kushuka chini, baada ya hapo alipokuwa anakua akawa mpole, kifupi hakuwa mtundu wa kupitiliza.
"Alipofika darasa la nne ndipo alianza kuonyesha ana kipaji cha mpira, nakumbuka kuna kipindi Simba ilikuja Morogoro na Dickson alikuwa miongoni wa watoto wanaookota mipira uwanjani, hili lilikuwa tukio kubwa kwake la kwanza kupata hiyo nafasi, baada ya hapo basi akawa anaendelea kupambania mchezo anaoupenda."
KARITHI KWA BABA
Mama Job anasema kipaji cha soka alichonacho mwanaye amerithi kwa baba yake na hata alipokuwa akimkataza kucheza, alikimbilia kwa baba ambaye alipenda acheze.
"Alikuwa ananiambia mwache mtoto acheze. Hujui kesho yake itakuwaje kwenye soka kwani ndiyo mchezo anaoupenda," anasema na kuongeza, baba yake ndiye alikuwa anamwombea ruhusa ya kucheza kwani naye alikuwa anapenda kile mwanaye anachofanya na alikuwa akimnunulia vifaa vya michezo.
Kuhusu baba Job kucheza soka, anasema; "Baba yake alikuwa anacheza namba nane, ingawa hakucheza kwa ukubwa, ila enzi zake akiwa shule alifahamika kwa uwezo wake na alipomaliza alikuwa akicheza timu za mtaani tu."
MAMA ALITAKA ASOME
Anasimulia wakati Job anasoma, alikomalia zaidi masomo kwa mwanaye huyo na hakufurahishwa na kucheza kwake soka. Hata alipomaliza kidato cha nne, alitaka aendelee kusomea kitu kingine wakati anasubiri matokeo ya mtihani wa mwisho.
"Mimi nilikomalia elimu, alipomaliza shule nikawa nataka aendelee kusomea kitu kingine huku akisubiri majibu ya kidato cha nne. Hata hivyo, hakufanya hivyo, kila siku alinidanganya atafanya hivyo, alisema ataenda kesho, mara nikimuuliza anasema wamefunga ofisi, wakati mwingine anadai ameshatoa hela hivyo asubiri ataambiwa siku ya kujiunga. Nilichoka kumuuliza kwani niliona hataki."
"Kwenye mambo ambayo sikupenda kabisa ayafanye (Job) ilikuwa kucheza soka. Ilinipa tabu sana. Niliona kabisa akiegemea huko ataacha kusoma. Nilitaka asome ingawa ilikuwa ni mambo mawili yamegongana, yeye anapenda soka na mimi nataka asome."
MZEE JOB AINGILIA KATI
Anasema wakati akipambana kuhakikisha mwanaye anasoma na kuachana na soka, baba yake (pichani juu akiwa na Dickson Job mbele ya nyumba yao) aliingilia kati na kutaka mwanaye acheze.
"Wakati mimi nikipambana kumzuia, baba yake alikuwa nyuma yake, akawa anampa nguvu ya kutaka acheze, ikawa ikitokea nimemsema sana kuhusu mambo ya mpira, anakwenda kusema kwa baba yake, anamfuata anamwambia baba mama hataki nicheze mpira, au ikitokea ana mechi na mimi nimemzuia anakwenda kumwambia baba yake na huko akawa anapata ile ruhusa anayotaka."
"Baba yake akawa ananifuata anazungumza nami kwa utaratibu akinitaka nimwache acheze akisema huwezi kujua, mwache afanye kitu anachokipenda. Basi ikawa hivyo hadi sasa," anasema na kukumbuka moja ya mechi baada ya Job kuanza kuichezea Yanga na baba yake alienda uwanjani na aliporudi alimwambia kuhusu kwenda na mwanaye uwanjani akiwa mdogo.
"Mechi kati ya KMC na Yanga, hii ilimkumbusha historia ya zamani baba yake kwani alienda uwanjani kumwangalia na aliporudi akasema; "Job nilikuwa nambeba nampeleka uwanjani leo nimeenda kumwangalia yeye.
"Basi tukamshukuru Mungu, tukamkumbuka sana mtoto wetu alikotoka."
Anasema hata bibi yake alikuwa anapatana naye sana kwani alipenda acheze soka na walielewana sana na alikuwa akisisitiza sana nimwache acheze.
"Tangu alipokuwa mdogo alikuwa anapatana sana na bibi yake ingawa yeye ni shabiki wa Simba mimi Yanga, hivyo namtaniaga sana na tulipomfunga mabao 5-1 alizima simu na kila wakicheza lazima nimpigie," anasema kwa furaha.
AANZA KUMWAMINI
Anasema hakumuamini katika harakati zake zote za mpira kuanzia yuko Moro Kids, ingawa hata yeye alikuwa mpenzi wa soka tangu akiwa shule ya msingi lakini hakuamini kama mwanaye atafika mbali, lakini kuna jambo moja tu ndilo lililomfanya aamini kweli mwanaye ana kipaji na anapenda soka.
"Siku aliyochaguliwa kujiunga na timu ya vijana ya Serengeti Boys, ndipo nilipomuamini ana uwezo mkubwa na mpira na atafika mbali. Hivyo, nilianza kumpa sapoti taratibu nikiamini katika safari yake ya soka.
"Kama mzazi niliwaza Tanzania kuna watoto wangapi hadi mwanangu apate hiyo nafasi ya kwenda timu ya Taifa, hapo ndipo nilipoanza kuwa upande wa Dickson," anasema na kuongeza yeye na mwanaye ni marafiki na huwa wanaongea kila baada ya mechi iwe wameshinda au wamepoteza mchezo na humpa moyo na kumkumbusha kusali na kumshukuru Mungu kwa lolote.
MJENGO ALIOWAJENGEA
Anasema timu ya kwanza kumwajiri mwanaye ni Mtibwa Sugar na hapo ndipo alipoanza kuona mabadiliko yake binafasi na familia kwa jumla baada ya kuanza kupata mafanikio na tulimwambia ni muda wa kubadili maisha.
"Dickson alianza kutujengea nyumba tunayoishi akiwa Mtibwa, maana alipoanza soka la kulipwa aliniambia mama sasa ni muda wa kuhama hapa tunapoishi. Nilifurahi kuona soka linaweza kubadilisha mambo kwa haraka. Hata yeye kukumbuka nyumbani tu na kujali familia yake kwa kile anachopata, kwangu niliona kama mafanikio makubwa," anasema na kuwashauri wazazi kuwaacha watoto wafanye kile wanachopenda kwani huleta faida na hapendi kusikia kipaji cha mtoto kinakufa kwa sababu ya wazazi kuwazuia watoto wao kuonyesha kile walicho nacho.
MTIBWA, YANGA ZAMPA WAKATI MGUMU
Anasema yeye na mumewe, baba Job ni mashabiki wa Yanga tangu hawajampata Dickson na wengi wanajua hivyo. Hata hivyo, mwanaye alipojiunga na Mtibwa walikuwa wanapata wakati mgumu sana kama familia wao wakishabikia Yanga, huku mtoto wao akiichezea Mtibwa.
"Ilikuwa kazi sana kushabikia Mtibwa na wakati huo tunaipenda Yanga ila mechi zote tulikuwa tunazitazama kwa sababu yake, ila kuishabikia Mtibwa ilikuwa haiwezekani. Nilikuwa nakosa amani zikicheza kwani sitaki Yanga ishindwe na Mtibwa, pia Mtibwa ikifungwa najua malalamiko yote yataenda katika safu ya beki ambayo mwanangu yupo, basi ilikuwa ngumu.
"Kuna mechi moja Mtibwa iliifunga Yanga, sikufurahi wala sikuhuzunika, ila nilikuwa namwambia Dickson napata shida sana mnapocheza na timu ninayoishabikia," anasema na kuongeza mechi iliyompa furaha ni ya kufuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na hatokaa haisahau;
"Msimu uliopita mechi ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho walipowafunga mabao 2-0 Marumo Galants, nilifurahi sana kuona wamefika hatua kubwa na hata walipokuwa washindi wa pili bado nilishukuru."
YANGA, MJUKUU VYAMSHTUA
Anasema alipata taarifa za mwanaye huyo kutakiwa na Yanga. Hata hivyo, zilikuwa ni tetesi tu alizoziona kwenye mitandao ya kijamii na ili kujiridhisha alimuuliza Job mwenyewe.
Hata hivyo, anasema alipokuwa akimuuliza alikuwa akimtuliza tu bila jibu la kueleweka na kutokana na uvumi kuwa mkubwa alikuwa akiombea iwe hivyo, ingawa Job mwenyewe alikuwa kimya.
"Hakuwa ananipa jibu la kueleweka, hapo awali alisema tu nitulie ataniambia, lakini ilikuwa tofauti sana kwani uvumi ulikuwa mkubwa sana wakati huo yeye akiwa kimya.
"Siku moja alinipigia na kuniambia tayari ameshasajili Yanga. Ilikuwa ni furaha kubwa kwangu kwani sikuamini kile nilichokisikia, ilikuwa ni furaha kama familia kwani ameenda tulipopataka," anasema na kuongeza alishtuka zaidi aliposikia kuwa mwanaye ana mtoto na hilo aliona limezidisha furaha yake.
"Akanishtua tena kuniambia ana mtoto, wakati mimi nilikuwa namwona ni mdogo. Hata hivyo, nilifurahi sana lakini sikutegemea, kwa sasa huniambii kitu kuhusu mjukuu wangu."
ISHU AFCON
Anazungumzia michuano ya Afcon ambayo mtoto wake alichaguliwa lakini hakucheza mechi hata moja kati ya tatu walizocheza Taifa Stars ikiwa kundi F na timu za Morocco, Zambia na DR Congo.
"Hakuniambia sababu ya kutokucheza ingawa tulikuwa tunaongea sana muda mwingi na ninachompendea mwanangu sio mtu wa kutikiswa, aliona ni kawaida na yuko imara muda wote wala hakuwa na huzuni.
"Nilikuwa namwambia amshukuru Mungu hata kwa kwenda tu huko kwani wapo waliotamani hata kuchaguliwa tu kwenda na haikuwezekana, hivyo kwa kuwa bado ni mdogo atacheza sana na alinielewa."
HUYU NDIYE JOB SASA
Anasema mwanaye ni mtoaji sana na hata akirudi mapumziko hutembelea timu alizocheza za mtaani na kuwapa chochote.
"Ni mtoaji sana tangu alipokuwa mtoto hadi sasa. Aliwahi kusafiri na shule kwenda Bagamoyo. Alikuwa darasa la pili. Aliporudi akaleta zawadi na kugawia majirani ingawa hazikuwa kubwa.
"Hata akija kusalimia muda mwingi anaenda kwenye timu za mtaani anaongea nao sana na kuwachia mipira au chochote na wanamkumbuka sana kila anapoondoka," anasema na kuongeza Job ni mpenzi wa ugali, dagaa na tembele na mara nyingi akirudi nyumbani anapenda apikiwe hivyo ingawa sio mkaaji, siku mbili au tatu anaondoka.
KIBWANA, KIBABAGE, MSHERY TANGU WATOTO
Anasema nyota hao ambao wote wapo Yanga kwa sasa wamekuwa marafiki tangu wakiwa darasa la tatu.
"Dickson amekua na marafiki zake tangu utotoni ambao ni Kibwana Shomari, Nickson Kibabage na Abdutwalib Mshery na walikuwa wanakuja nyumbani tangu akiwa darasa la tatu.
Ni watoto ambao nawaombea na Mungu amekuwa akiwasaidia, nilifurahi sana kuwaona wote wako timu moja kwani hiyo ndio ilikuwa ndoto yangu kubwa, hata nikimkosa Job huwa nampigia Kibwana sana ndio nampata, lakini huwa nawasisitiza sana upendo ili waweze kudumu.
"Siku zote huwa namshauri Dicki kuweka pesa na kufanya maendeleo kama kijana ili aweze kuwa na maisha mazuri na yasiyo na majuto huko mbele, pia ana familia.
Kuhusu kazi naongea naye kuhusu heshima kwa kila mtu na asichukulie poa kile ambacho anaelekezwa kila siku na viongozi au kocha bila kumdharau yeyote."