Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama Kibabage adokeza ishu ya Simba

Job X Mama Yake Mama Kibabage adokeza ishu ya Simba

Wed, 13 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

“Sijui kama aliwahi kutakiwa na Simba ila mimi nataka abaki hapo hapo alipo. Marafiki zetu ambao ni mashabiki wa Simba, huwa wananiambia timu yao itambeba siku moja katika utani, lakini natamani akitoka hapo aende mbali zaidi ya pale.”

Hayo ni maneno ya mama mzazi wa nyota wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, Nickson Kibabage anayejitambulisha kwa jina la Flora Ngwido.

Kibabage ni beki wa kushoto wa Wanajangwani na kwenye familia yao ni wa kwanza kuzaliwa katika watoto watatu, akiwa na dada zake wawili kwa mama yao, Flora.

Nyota huyo ambaye amepita timu kadhaa za dani na nje ya nchi kama Mtibwa Sugar, KMC, Singida Big Stars, Difaa El Jadida na Yanga aliyo kwa sasa, pia alicheza timu ya vijana ya Serengeti Boys, ana historia tamu kama mama yake anavyosimulia mama yake wakati wa mahojiano na Mwanaspoti lililofunga safari hadi nyumbani kwake, Mkundini Morogoro.

KUHUSU SIMBA

Bila kumung’unya maneno, mama Kibabage ambaye ni mnazi mkubwa wa Yanga anasema hataki wala hategemei kuyasikia ni mwanaye kumwambia anakwenda Simba na anataka akiondoka Yanga arudi nje ya nchi.

“Mimi ni shabiki mkubwa wa Yanga, natamani sana mwanangu aendelee kucheza soka lakini sio Simba. Natamani akitoka Yanga arudi nje akacheze soka la kimataifa.”

YANGA YABADILI MAISHA YAO

Flora ambaye anakiri Yanga imebadilisha maisha yao kiuchumi, anasema walikuwa wakiishi Morogoro mjini wakati huo wakiwa hawana mipango ya kuhamia waliko sasa nje ya mji, lakini soka limewaweka sehemu nzuri zaidi ya hapo awali.

Pia anasema Kibabage amejenga nyumba wanayoishi na anasomesha wadogo zake na sasa ameanza ufugaji wa Kuku na Bata.

KWA KIBABAGE HUMWAMBII KITU

Anasema Kibabage ni kama, pacha kwake na tangu anakua wengi walikuwa wanasema anafanana naye na wanalingana urefu mbali na ukaribu waliokuwa nao.

“Watu hawajui tabia tatu za Kibabage. Wanasema ni mkali au ana hasira mambo ambayo sijawahi kabisa kuyaona kwake ila ni mtoto wa kipekee sana kati ya wote.

“Ni mpole sana na hiyo inamfanya asiwe mwongeaji sana, pia ana heshima na kama mzazi kuwa na mtoto wa kiume mwenye nidhamu inanipa furaha. Pia wengi hawajui kama ni mpishi mzuri,” anasema.

“Wakati yuko Morocco kaka yake Msuva (Saimon) alikuwa ananiambia jinsi alivyo mpishi mzuri ingawa hakuwahi kupika hadi anaondoka na aliporudi nikataka kuonja mapishi yake ndipo nilipoamini,” anasema Flora na kuongeza anaumia sana akimwona Kibabage anaanguka au kupata majeraha uwanjani na wakati mwingine kama mama anashindwa kabisa kuendelea na kuangalia mpira.

“Nilikuwa sifurahi sana kwenda kwake kucheza lakini baada ya kuona matokeo ya ndoto zake nilivutiwa na mpira na kuwa shabiki yake wa kwanza, kwani wanawake sio wapenzi sana wa soka kama wanaume.”

MUME AMVUTA YANGA

Flora anafichua mapenzi yake na timu hiyo yanatokana na mumewe na ni shabiki wa Yanga kabla hata hawajafunga ndoa.

“Niliolewa nikamkuta mume wangu anashabikia Yanga na alikuwa anamsapoti sana Nickson katika mambo ya soka jambo ambalo kwangu lilikuwa ni la kawaida.

“Mtoto wetu alivyoanza kucheza ndipo nilipoanza kuuelewa mpira nikaamua kuchagua timu moja wapo kati ya hizi kubwa, lakini chaguo langu likawa katika timu ya mzee ili tuwe tunashangilia wote ushindi.”

MAISHA YA MOROCCO

Anasema maisha ya Kibabage akicheza Morocco, Al Jadida yalikuwa magumu kwani hakuwa anapata nafasi licha ya uwezo aliokuwa nao.

“Kila alipokuwa ananiambia majaribu magumu aliyokuwa akipitia kama mzazi nilikuwa naumia ila sikuacha kumpa matumaini na kumwambia bado mdogo hivyo anaweza kufanikiwa.

“Aliporudi kwa ajili ya mapumziko wakati anaondoka aliitwa timu ya Taifa na haikuchukua muda akaniambia harudi tena Morocco bila sababu na kwa kuwa najua anaelewa anachokifanya basi nilikubaliana na maamuzi yake,” anasema

TAARIFA ZA KUSHTUA

Anasema moja ya taarifa zilizomshutua na kufurahi ni kwenda Yanga na mtoto.

“Alinipigia simu akasema mama nimesaini Yanga ila hawajanitangaza bado ila muda sio mrefu watafanya hivyo, kama mzazi nilifurahi na kuona nyota ya mafanikio kwa mbali imeanza kuchomoza.”

Anasema hakuwahi kufikiria kupewa taarifa ya familia kwa Kibabage kwani hakuwahi kumwona na hekaheka zozote na mabinti tangu utotoni zaidi ya dada zake.

“Siku mbili kabla ya kutangazwa Yanga aliniambia mama nina mtoto, nikajua kama kawaida ananitania lakini nikaomba anitumie picha kwani nilijua hapo ndipo ningejua ukweli.

“Basi alinitumia picha nikaamini kwa sababu hakuna mtu atakubali mwanae apigwe picha akiwa mdogo, nikamwambia sasa anatakiwa kupambana kwani tayari ana familia na bado ni mdogo,” anasema.

JESHINI AU PADRI

Flora anasema alitamani mtoto wake afanye kitu tofauti na zaidi mambo ya dini ikiwamo kuwa padri.

“Nilitaka aende Jeshi au awe padri lakini yeye hakuwa anataka chochote akili yake yote ilikuwa kwenye soka hivyo ilikuwa ngumu kumbadilisha kwani alikuwa na nia ya soka.

“Siku zote alikuwa ananiambia mama subiri mimi bado mdogo nitaamua tu na nitakupa majibu kama nitaenda jeshini au kanisani ila kwa sasa niache kidogo.”

KIBWANA NA JOB

Anasema wakati wapo wadogo marafiki zake wakubwa ni Dickson Job na Kibwana Shomari lakini baadae akamwona Mshery ameongezeka hilo lilimfanya kuona kuwa ana watoto zaidi ya Nickson.

“Urafiki wao ni wa kweli kabisa na nimeushuhudia tangu utotoni licha ya kuwa sikufahamu familia za marafiki zake hao ila watoto wetu wamekuwa ndugu na baadae tutaonana.”

“Kibwana anakuja sana kwani amejenga karibu na Kibabage ila wengine sasa tunawasiliana sana kuliko kuonana na ninawaelewa, lakini bado ukaribu wao naupenda sana una manufaa,” anasema na kuongeza Msuva amekuwa kama kaka yake Kibabage kwani alikuwa nae Morocco na ndiye aliyeondoka nae lakini muda mwingi huwa anafika nyumbani kusalimia na huwa anamshauri vitu vingi mdogo wake.”

USHAURI

Mpira ni kazi ya muda mfupi kwani inaenda sawa na umri hivyo kama mama huwa anongea naye mambo mengi hasa upande wa uwekezaji;

“Muda mwingi namshauri kutunza heshima yake ili acheze bila shida. Afanye uwekezaji hasa wa mali kama kujenga na mengine ili atakapostaafu basi awe mfano kwa vijana wengine ambao leo au kesho wanataka kuwa kama yeye,” anasema na kuongeza Kibabage ni msafi tangu utotoni na anapenda kufua na ni mpenzi wa mbwa, pia anapenda chakula kimoja tu na kama ukipika tofauti na hicho mtagombana. Anapenda wali na njegere au mboga yoyote.”

USHAURI KWA WANAWAKE

Flora anaongea na wanawake ambao ni walezi wa watoto; “Mama yeyote asimzuie mtoto kufanya kile anachokipenda na atakifanya kwa moyo na kufanikiwa. Sikuupenda mpira ila mwanangu alicheza ila nilimpa ratiba ambayo haitamfanya asisome hiyo ilimfanya afanye majukumu yake kwa wakati na kucheza soka bila shida.”

Chanzo: Mwanaspoti