Miamba ya soka Zanzibar, Malindi SC na Mlandege FC, inatarajiwa kushuka dimbani leo kwenye mchezo wa 'Dabi' ya Zanzibar Ligi Kuu mzunguko wa 21 wa ligi hiyo inayoelekea ukingoni.
Timu hizo kongwe katika medali za soka Visiwani Zanzibar, zitapepetana leo katika Uwanja wa Mau A majira ya saa kumi alasiri huku zote zikiwa bado zinasaka alama za kujihakikisha zinabaki Ligi Kuu mwishoni mwa msimu, Mlandege FC wakiwa nafasi ya 10, wakati Malindi SC wakiwa nafasi ya tisa timu na kila moja ikiwa na pointi 25.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Malindi SC, Suleiman Mohmed, alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwa kuwa timu zote bado zinahitaji alama za kujihakikishia kubaki Ligi Kuu.
Alisema hawakuwa na mwanzo mzuri wa kwenye ligi kwa upande wao na hata kwa wapinzani wao, hivyo lazima kila mmoja atakuja na mbinu mbadala za kusaka ushindi.
Alisema katika mchezo huo wanahitaji alama tatu na zitapatikana iwapo wachezaji watacheza kwa utulivu na kutokuwa na hofu ya mchezo.
“Mchezo huu unahitaji uzoefu kwa wachezaji na hata makocha hasa katika kufanya maamuzi ya haraka uwanjani, hatuhitaji kutumia nguvu nyingi bali wachezaji wawe na uwezo wa kuwasoma wapinzani wetu," alisema.
Naye Kocha Mkuu wa Mlandege FC, Hassan Ramadhani, alisema amewaandaa wachezaji wake vizuri kuhakikisha wanacheza kwa ushindani katika mchezo huo muhimu.
Alisema bado kikosi chake kipo imara na kina hamasa kubwa kuona wanashinda mchezo huo dhidi ya wakongwe wa soka na dabi ya miaka mingi.
Ramadhani alisema mchezo wa dabi siku zote huwa mgumu na wenye ushindani mkubwa, hivyo wao Mlandege FC wamejipanga kuwakabili wapinzani wao.
“Tunaenda uwanjani kupambana kuhakikisha tunapata alama ambazo zitatufanya tupate matokeo mazuri katika michezo yetu hii iliyobaki,” alisema.