Malkia Letizia wa Hispania anatarajia kwenda nchini Australia kuhudhuria mechi ya fainali za kombe la Dunia la Wanawake (soka) jijini Sydney. Katika mechi hiyo timu ya Taifa ya England itachuana na timu ya Taifa ya Hispania.
Shirikisho la soka la nchini Hispania limethibitisha kuwa Malkia Letizia atahudhuria mechi hiyo na binti yake Infanta Sofia (16). Kutokana na kutingwa na shughuli zingine Mfalme Felipe wa Hispania hatoweza kuhudhuria.
Malkia Letizia aliitembelea timu ya taifa ya Hispania ya wanawake wakati ikifanya mazoezi mwezi Juni na kuzungumza na wachezaji pamoja na makocha.
Hadi sasa taarifa zinaeleza kuwa hakuna mwakilishi kutokea familia ya kifalme ya nchini Uingereza atakayehudhuria mechi hiyo.
Mwana mfalme William atatizama mechi hiyo kupitia televisheni akiwa katika kasri ya Kesington nchini Uingereza.
Sababu mojawapo ya mwana Mfalme huyo kutohudhuria mechi hiyo imetajwa kuwa ni kujaribu kupunguza safari ndefu sana za ndege (hasa za kwenda kukaa kwa muda mfupi) kwani husababisha uzalishwaji wa kaboni hivyo si rafiki kwa mazingira.
Mwanamfalme William amefanya suala la kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kuwa moja ya mambo yenye kipaumbele zaidi kwake.
Mwanamfalme huyo aliitembelea timu ya taifa ya England (wanawake) wakati ikifanya mazoezi yake mwezi Juni.
Mfalme Charles III ameipongeza timu hiyo na kuwatakia kila la kheri kwenye mechi ya Jumapili.
Mara ya mwisho kwa timu ya taifa ya soka ya England kuingia katika fainali za kombe la dunia ilikuwa mwaka 1966, mechi hiyo iliyochezwa Wembley ilihudhuriwa na Malkia Elizabeth II, timu hiyo iliifunga West Germany magoli 4 kwa 2.