Kikosi cha JKT Tanzania kinaendelea na mazoezi kujiwinda na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Malale Hamsini akiwataka mastaa kutorudia makosa waliyofanya awali ambapo walikumbana na aibu kwenye mechi ya pili dhidi ya Yanga.
JKT iliyorejea katika ligi hiyo ilianza msimu huu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo kabla ya kufumuliwa 5-0 na Yanga, na kocha Malale alisema amekaa na wachezaji ili kuwajenga kisaikolojia huku akiwataka wasifadhaike kwa kile kilichotokea.
“Yalikuwa matokeo ya kuumiza sana, ila nashukuru baada ya kukaa chini na wachezaji waliyapokea na kuniahidi kutorudia tena makosa. Binafsi nilifarijika kuona wamerejea kwenye hali za kawaida,” alisema.
Aliongeza kuwa kufungwa mabao mengi kama ilivyowatokea njia rahisi ya kuwapima wachezaji kama wako tayari kiakili na kimwili ni kupata mchezo mwingine wa kiushindani japo bahati mbaya haikutokea.
“Wakati tunapoteza tulihitaji mchezo mwingine lakini bahati mbaya tukaingia kwenye kalenda ya Fifa, japo tumeendelea kucheza michezo mingi ya kirafiki kwa ajili tu ya kurejesha ile hali ya kujiamini kwao.”