Azam FC kwa sasa ipo moto, lakini hilo halijamshtua Kocha wa JKT Tanzania, Malale Hamsini ambaye kesho Jumatatu timu yake itavaana na vinara hao wa Ligi Kuu Bara, akisema licha ya ubora iliyonayo, lakini hahofii chochote na watajuana uwanjani wakati wakiumana kwa dakika 90 za pambano hilo.
Azam itakuwa wenyeji wa JKT kwenye Uwanja wa Azam Complex, ikiwa ni kati ya mechi mbili za Ligi Kuu zinazopigwa kesho ikiwamo ile ya Singida Fountain Gate dhidi ya KMC jijini Arusha kwenye Uwanja wa Black Rhino.
Akizungumza nasi, Malale alisema licha ya kutambua ugumu wa mchezo huo, wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri huku akiweka wazi kila mchezaji ana morali kubwa na anatambua umuhimu uliopo wa kuzipigania pointi tatu.
“Ni mchezo wa mtego kwa sababu siku zote unapokuwa ugenini ni lazima ujiandae kwa maana ya kiakili na kimwili na hii ni kutokana na kila timu inapigania kupata ushindi hivyo sio rahisi kwetu lakini tutaonyesha ubora tuliokuwa nao,” alisema.
Malale aliongeza mchezo huo kuchezwa Azam Complex kwao pia ni faida maana ndio uwanja wanaoutumia katika michezo yao ya nyumbani baada ya ule wa Kambarage mkoani Sinyanga kuendelea na maboresho hivyo watacheza kwa nidhamu na sio kuwaogopa.
Kikosi hicho kitakuwa na kibarua kigumu cha kupambana na Azam iliyotoka kuifunga KMC mabao 5-0, katika mchezo uliopita huku ikimkosa pia nyota wake muhimu, Hassan Nassor ‘Machezo’ aliyepata kadi nyekundu mechi na Singida Big Stars, Desemba Mosi.