Wakati kiungo mshambuliaji wa JKT Tanzania, Hassan Dilunga akionesha matumaini ya kurejea upya uwanjani, kocha mkuu wa timu hiyo Malale Hamsini amesema nyota huyo atarudi kwa kiwango bora.
Pia amesema kwa nidhamu aliyonayo kikosini anaamini baada ya misimu miwili ijayo hatabaki JKT Tanzania na kwamba kiwango chake kitarejea zaidi na wengi watamshangaa.
Hamsin ametoa kauli hiyo leo jijini Mbeya wakati akizungumza na Mwanaspoti baada ya mchezo wao dhidi ya Prisons iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, huku Dilunga akiingia dakika ya 80.
Dilunga aliyewahi kuzichezea timu kadhaa, mara ya mwisho alikiwasha Simba kabla ya kupatwa majeruhi na kuwa nje ya uwanja kwa takribani mwaka mmoja na sasa anakipiga kwa Maafande hao kujiweka fiti.
"Huyu (Dilunga) naongea naye kama mwanangu nafurahishwa na mwenendo wake haswa nidhamu, naamini atarudi upya na baada ya msimu mmoja au miwili nchi na dunia watamshangaa na sidhani kama atabaki hapa" amesema kocha huyo.
Kwa upande wake Dilunga ameiambia Mwanaspoti kuwa kwa sasa anaendelea vyema na kwamba muda anaopewa kucheza anautumia vyema ili kurejesha ubora wake.
"Nimetoka kwenye majeruhi makubwa kwa muda mrefu, hivyo kwa sasa napewa dakika chache ila naamini kadri navyocheza nitaimarika zaidi na kurudi kwa ubora uleule" amesema Dilunga.