Kuna makocha wana kibarua kigumu cha kuhakikisha wanazinusuru ajira zao, kutokana na kile walichokivuna kwenye mechi tano ambazo timu zao zimecheza Ligi Kuu Bara.
Katika raundi tano hizo Simba ndio inayoongoza Ligi Kuu ikiwa haijapoteza mchezo ikiwa na pointi pointi 15, ikifuatiwa na Azam FC pointi 13 na Yanga pointi 12, timu hizo zikiwa zinatamba nafasi za juu, zipo zile zilizo nafasi ya chini ambazo makocha wao wanatakiwa kupambana ili kujiondoa kwenye nafasi mbaya.
Timu ambazo zipo nafasi tano za mwisho ni Coastal Union nafasi ya 16 pointi 2, katika mechi tano haijashinda, sare mbili na imefungwa mitatu inamiliki mabao mawili na imefungwa mara saba.
Mtibwa Sugar iliyopo nafasi ya 15, ina sare mbili, imefungwa mechi tatu (pointi mbili), Namungo ipo nafasi ya 14 ina sare tatu, imefungwa mechi mbili (pointi tatu), Prisons ipo nafasi 13 ina pointi nne, imeshinda mchezo mmoja, sare tatu, imepoteza mchezo mmoja na Geita Gold iliyopo nafasi ya 12 ina pointi nne, imeshinda mechi moja, sare tatu na imefungwa mchezo mmoja.
Makocha wa timu hizo ni wapya ambao ni Fred Felix Minziro (Prisons), Habib Kondo (Mtibwa), Cedrick Kaze (Namungo), Mwinyi Zahera (Coastal) na Hamed Morocco (Geita Gold), kwani msimu uliopita hizo timu zilikuwa na makocha wengine ambao waliachana nazo.
Msimu uliopita Coastal Union, Mtibwa Sugar, Prisons na Coastal Union hazikuwa kwenye nafasi nzuri, hivyo msimu huu zina kazi ya kuhakikisha zinajikwamua mapema ili kuondoka na adha ya kupambana kushuka daraja.
Pamoja na matokeo hayo, kocha Minziro alisema "Tuna nafasi ya kupambana kuhakikisha michezo inayofuata tunafanya vizuri, hivyo hatuwezi kukata tamaa."
Hoja yake inaendana na ya kocha Morocco wa Geita Gold aliyesema "Ligi imeanza kwa ugumu, lakini bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi zinazofuata, ili kuondoka na matokeo mabaya."