Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha wazungu waigombea Simba

BARBARA?fit=720%2C461&ssl=1 Makocha wazungu waigombea Simba

Sat, 30 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

UONGOZI wa Simba umesema mafanikio waliyopata katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita yamekuwa ni 'chachu' kwa makocha mbalimbali kutoka Ulaya kutuma maombi ya kutaka kurithi mikoba iliyoachwa na Mfaransa Didier Gomez, imefahamika.

Hata hivyo, Simba imesema idadi ndogo ya makocha kutoka barani Afrika ndio wametuma maombi ya kuajiriwa na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, aliliambia gazeti hili jana wamepokea maombi 73 na idadi kubwa ya makocha waliotuma maombi yao wanatoka Ulaya.

Barbara alisema umefika wakati makocha kutoka hapa Afrika kujiamini na kujiweka tayari kukabiliana na changamoto ya kazi hiyo wanayoifanya.

Kiongozi huyo alisema hadi kufikia jana mchana asilimia 95 ya maombi waliyopokea yanatoka kwa makocha walioko nje ya Afrika.

"Inaonekana ama makocha wetu wanaogopa kukutana na changamoto ya ushindani au hawana sifa za kutosha kutuma maombi," alisema Barbara.

Aliongeza hii ni dalili kwamba umefika wakati wa kila klabu kuweka vigezo vya aina ya kocha inayemhitaji kwa ajili ya kuwa tayari kukabiliana na ushindani lakini pia kufikia malengo ya kufanya vyema kwenye michuano ya kimataifa.

Kwa sasa Simba iko chini ya Thierry Hitimana na katika mchezo wake wa kwanza baada ya kukabidhiwa mikoba alifanikiwa kuifunga Polisi Tanzania bao 1-0 na kesho atakiongoza kikosi hicho kuwakaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Chanzo: ippmedia.com