Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania limetaja makocha 14 ambao hadi sasa hawana vigezo vya kuwa sehemu ya maofisa wa mabechi ya ufundi kwa timu mbalimbali zitakazoshiriki Ligi ya Championship iliyopangwa kuanza mwezi ujao.
Makocha hao wamekosa sifa ama kwa kutokuwa na daraja la leseni inayoruhusiwa kikanuni kuwa miongoni mwa maofisa wa benchi la ufundi ama hawajafanya kozi za kupigwa msasa (refresher) ambazo ni lazima kwa kila mmoja ili wakidhi vigezo.
Orodha hiyo ya makocha 14 wasioruhusiwa inawajumushia makocha wakuu Mohamed Kijuso (Cosmopolitan), Iddi Cheche (Pan African), Venance Kazungu (Copco), Leonard Budeba (Mbuni), Amani Josiah (Biashara United) na Zulfikir Mahad wa Stand United.
Makocha wasaidizi ni Riziki Shawa (Pan African), Mohamed Abbas (Polisi Tanzania), Omary Madenge (Biashara United), Michael Mnyali (Mbeya Kwanza), Mathias Wandiba (Mbeya City) na Simbaliana Rashid (Fountain Gate).
Kuna makocha wawili wa mazoezi ya viungo ambao wametajwa kutoruhusiwa na TFF ambao ni Stanley Nkomola wa Green Warriors na Hamis Kulogwa wa Mbeya Kwanza.