Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha watano bora wenye umri mdogo

Xabi Alonso Makocha watano bora wenye umri mdogo

Thu, 30 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Miaka ya hivi karibuni imekuwa jambo la kawaida kwa makocha vijana kupata mashavu ya kufundisha kwenye klabu mbalimbali kubwa kuanzia Afrika hadi Ulaya kutokana na soka kubadilika kadiri siku zinavyosogea.

Yapo majina mengi makubwa Ulaya ambayo yanatikisa sokoni kutokana na uzoefu wao kama vile Carlo Ancelotti (64) yuko katika kibarua chake cha pili Real Madrid, huku Maxi Allegri (56, Juventus), Stefano Pioli (57, AC Milan) na Jose Mourinho (60, Roma). Kwingineko, yupo Mauricio Pochettino (51, Chelsea), Diego Simeone (53, Atletico Madrid) na Erik ten Hag (53, Man United), hao ni makocha wakongwe kwenye tasnia.

Lakini pia makocha hao wanakumbana na changamoto ya ushindani wa kimbinu kutoka kwa makocha vijana ambao wameibuka na kuanza kufanya vizuri mfano mzuri ni Xabi Alonso, 41, ambaye ameifanya Bayer Leverkusen kuwa moto wa kuotea mbali kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani ambayo ni maarufu kama Bundesliga.

Hii ni orodha ya makocha watano vijana huko Ulaya na pengine kwa miaka michache ijayo wanaweza kuwazidi kete makocha wakongwe ambao CV zao zinaonekana kutisha kutokana na kufanya kwao vizuri kwa miaka mingi.

Xabi Alonso, 41, Bayer Leverkusen

Mwaka mmoja tu baada ya uongozi wake wa kwanza kama kocha mkuu katika klabu ya Bayer Leverkusen, kiungo huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Hispania na klabu za Real Madrid na Liverpool, tayari ameanza kujizolea umaarufu. Labda ni mapema kwa kiasi fulani, lakini hata hivyo anatajwa kuwa huenda kwa miaka michache ijayo akapata ulaji mkubwa zaidi.

Bila kujali sifa za kupendeza, Alonso bila shaka ameifufua timu inayoyumba ya Leverkusen. Baada ya kuchukua usukani Oktoba mwaka jana, Mhispania huyo aliiongoza klabu hiyo ya Ujerumani kutoka nafasi ya pili chini kabisa ya Bundesliga hadi kumaliza katika nafasi ya sita, na kufika nusu fainali ya Europa Ligi.

Mwaka mmoja baadaye, kikosi cha Alonso kimekaa kileleni mwa ligi, baada ya kushinda michezo 11 huku ikitoka sare moja tena ya mabao 2-2 wakiwa ugenini dhidi ya Bayern Munich.

Kocha huyo anayependa kutumia mfumo wa 3-4-3 ameifanya Leverkusen kuwa moto wa kuotea mbali na ni wazi kwa mwenendo wao wanaweza kutoa changamoto kwenye mbio za ubingwa wa Bundesliga mbele ya Bayern Munich, Dortmund na RB Leipzig ambao wamekuwa wakipewa nafasi kwenye kinyang’anyiro hicho.

Will Still, 31, Reims

Mzaliwa wa Ubelgiji na wazazi wake Waingereza, alibamba vichwa vya habari kote duniani alipopandishwa cheo na kuwa kocha mkuu katika klabu ya Reims baada ya kuondoka kwa Oscar Garci­a Oktoba mwaka jana akiwa na umri wa miaka 30 tu.

Alikuwa amefanya kazi kubwa katika soka kama mchambuzi wa video, akisimamia mechi nane pekee akiwa kama kocha mkuu wa mpito katika Ligi ya Daraja la Pili Ubelgiji akiwa na umri wa miaka 24. Hata hivyo, Reims alifanya vizuri mno chini yake kwa kucheza michezo 17 bila kupoteza.

Hata hivyo, klabu hiyo iliingia kwenye majanga kwa kulazimika kulipa faini ya Euro 25,000 kwa kila mchezo kutokana na kocha huyo kukosa diploma inayohitajika ya ukocha. Mwaka mmoja baadaye, kila kitu kikawa sawa na timu yake inafanikiwa kumaliza katika nafasi ya sita.

Sebastian Hoeness, 41, Stuttgart

Licha ya jina lake la ukoo, Hoeness ni mtoto wa mshambuliaji wa kati wa zamani wa Bayern Munich, Dieter na mpwa wa Uli, kocha huyo amekuwa akifanya makubwa akiwa na Stuttgart.

Hoeness aliingia katika ukocha akiwa na umri wa miaka 29 na kujifunza kazi yake katika akademi za Bayern na RB Leipzig. Katika majira ya kiangazi ya 2020 alipewa nafasi ya kuchukua jukumu la kukinoa kikosi cha kwanza cha Hoffenheim, ingawa misimu yake miwili aliiongoza timu na kumaliza katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.

Mafanikio yake makubwa hadi sasa, hata hivyo, ni kuinusuru Stuttgart kushuka daraja kutoka Bundesliga mwishoni mwa msimu uliopita huku kukiwa na mechi nane pekee aliiongoza timu hiyo na kuwa mbali na hatari ya kushuka daraja.

Msimu huu, Stuttgart ikisaidiwa na mfungaji wa mabao 13, Serhou Guirassy ni kati ya timu ambazo zinawashangaza wengi kwenye ligi, ipo nafasi ya tatu juu ya Dortmund yenye pointi 24 kwa tofauti ya pointi tatu.

Francesco Farioli, 34, Nice

Kijana huyo wa Kiitaliano hakuchagua njia ya kuwa kocha mkuu katika moja ya timu zenye malengo makubwa katika ligi ya “Top Five” Ulaya. Kutoka kuwa kocha msaidizi na sehemu ya kocha wa makipa wa Roberto De Zerbi huko Frosinone na Sassuolo, Farioli aliamua kuchukua jukumu la kuinoa timu ya Uturuki ya Karagumruk miaka mitatu iliyopita.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Farioli alifanya vyema kiasi cha kutosha kupata nafasi ya kuinoa Alanyaspor kabla ya kuteuliwa kuwa kocha mpya wa Nice msimu huu wa joto. Matokeo yake ya heshima akiwa na timu za Kituruki yaliwavutia mabosi wa Nice na kuamua kumpa nafasi.

Licha ya mzunguko mgumu wa mechi za ufunguzi, Nice iliwahi kutushangaza kwa kuzitandika PSG na Monaco ugenini. Fagioli amekiri waziwazi shukrani zake ni kwa De Zerbi kwa kumpa ujuzi na mwishowe kuwa mmoja wa makocha vijana ambao kwa sasa wanatolewa macho kwenye soka la Ulaya.

Thiago Motta, 41, Bologna

Kiungo huyo wa kati mzaliwa wa Brazil bado anakumbukwa zaidi kwa enzi zake za uchezaji bora ambapo alicheza mechi 30 za wakubwa akiwa na timu ya taifa ya Italia, lakini kwa sasa anafanya kazi ya kufundisha.

Motta anafuatiliwa kwa karibu na klabu kubwa barani Ulaya, kwa kiasi kikubwa kutokana na sifa zake binafsi kama mzungumzaji mnyoofu na mchapakazi.

Chanzo: Mwanaspoti