Siku moja baada ya dirisha la usajili kufungwa, huku Simba ikisajili washambuliaji wawili usiku, imewaibua makocha na kusema timu hiyo imecheza kamari.
Simba imesajili washambuliaji wawili, Mgambia, Pa Omar Jobe akitokea FC Zhenis ambaye ilimtangaza jana mchana na Freddy Michael kutoka Green Eagles.
Usajili wa Simba umefanyika baada ya kuondolewa kwa washambuliaji wawili Moses Phiri ambaye amefunga mabao matatu na Jean Baleke mwenye nane msimu huu.
Hata hivyo, usajili wa mastaa hao wawili , Jobe na Fredy umeonekana kuwagawa mashabiki, baadhi wakiamini ni mastaa wa kazi na wengine wakiona haukuwa usajili sahihi kwa sasa.
Simba ilikuwa na uhitaji mkubwa wa mshambuliaji kwa ajili ya michezo ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoendelea kuanzia Februari.
Freddy ambaye anakuja na jina kubwa, ametua Simba akitokea Zambia alikokuwa kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya nchi humo akiwa nayo mabao 14 katika michezo 18 na anatajwa ni mmoja wa mastaa wakubwa kwenye ligi hiyo. Baada ya staa huyo kutua, Simba iliwaachia Phiri na Baleke ambao walikuwa wakicheza kwenye nafasi hiyo kwa kupokezana.
Baada ya usajili huo, makocha wazoefu wa Ligi Kuu Bara wamesema ni jambo la kusubiri lakini ni kama kamari kwani kuna wachezaji waliotua nchini na majina makubwa lakini wakashindwa kufanya vizuri.
Kocha wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Charles Mkwasa amesema uamuzi uliofanywa na Simba kwa kuacha wachezaji wote wawili kwa wakati mmoja ni kujitoa mhanga kwani wamevunja muunganiko ambao tayari ulitengenezwa na sasa wanaanza upya.
“Siwezi kuzungumzia zaidi ishu yao kwani ni makubaliano ya pande mbili kuvunja mkataba na klabu ndio inayoajiri, lakini kiufundi wamevuruga ushirikiano uliokuwepo awali ambao ulionekana kuanza kuzaa matunda.
“Timu haijengwi kwa siku au saa, inahitaji muda ili kuwa na ushirikiano, lakini suala la kuondoa na kuleta wengine ni kutoa kazi nyingine ya kuhakikisha wanatengeneza kikosi cha muunganiko mpya, sina shaka lakini hofu ni kama watashindwa kuwika kwa wakati husika,” amesema.
Kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ amesema Simba ina kocha bora na mwenye rekodi nzuri ya kutwaa mataji Afrika, kama uamuzi wa kuachana na washambuliaji hao kaufanya yeye, anaungana naye kwa asilimia 100, lakini kama ni viongozi wamekosea.
“Abdelhak Benchikha ndiye anayekaa na wachezaji na kuwaandaa muda wote, hivyo kuchukua uamuzi kama huo ni sahihi kwake kwa sababu hawampi anachokitaka lakini kama kuna watu wengine nje na benchi la ufundi ndio wameamua hilo watakuwa wamekosea;
“Viongozi kuamua kuacha mchezaji ambaye yupo kwenye mahitaji ya kocha ni kosa kubwa kwani wanakuwa wanaingilia kazi ya benchi la ufundi lakini kama ni uamuzi wa kocha ambaye ana uwezo mkubwa kunizidi mimi sina budi kuungana naye,” amesema Julio kocha wa zamani wa Taifa Stars.
Kocha wa zamani wa Tanzania Prisons, Adolf Rishard, ambaye amekuwa kwenye ligi kwa muda mrefu alisema kwenye usajili kuna mambo mawili kubahatisha au kukosea kutokana na kuwa na matarajio makubwa na mchezaji na baadaye akashindwa kukupa kile unachokihitaji.
“Kazi ya mshambuliaji ni kufunga wawili hao miezi miwili ya hivi karibuni wameshindwa kutoa kile walichokuwa wanatarajiwa na wengi hivyo uamuzi uliofanywa unaweza kuwa sahihi au sio sahihi;
“Kulikuwa na taarifa Phiri alikuwa anataka kuvunja mkataba wake mwenyewe baada ya kuona hafanyi kile anachotakiwa kufanya, Baleke licha ya kuwa bora pia alipoteza umakini akiwa ndani ya boksi hivyo kulikuwa na umuhimu wa kukaa na wachezaji hao kujua kilichokuwa nyuma ya pazia kabla ya uamuzi walioufanya,” alisema.
Rishard amesema kwa upande wake, Baleke bado alikuwa ni muhimu kwenye kikosi cha Simba hasa dirisha hili la usajili ambalo kupata mchezaji wa kiwango kikubwa ni mtihani kwani hadi sasa alikuwa ana mabao nane kwenye ligi mawili nyuma ya kinara.
“Dirisha hili ni bahati kupata mchezaji atakayekupa kile unachotamani. Usajili wa washambuliaji wawili unaweza ukawa bora kwao au ukawaangusha kutokana na wawili hao kutokuwa na muda wa kukaa pamoja hivyo watahitaji muda;
“Ni kweli eneo lao la ushambuliaji lilikuwa na uhitaji kutokana na wawili walioachwa kupoteza ubora wao lakini walipaswa kumwacha mmoja ili kumjenga mchezaji mpya na kumfahamisha mfumo na aina ya uchezaji wa timu hiyo,” alisema
Pia akizungumzia ubora wa mmoja mmoja alisema kila mmoja ana aina yake ya uchezaji lakini itategemea ndani ya Simba ni kina nani watawazunguka na kuwapa kile kitakachowapa nafasi ya kufunga.