Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha wanavyoiona Dabi ya Kariakoo

Makocha Ligi Kuu Makocha wanavyoiona Dabi ya Kariakoo

Sat, 4 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hata kama ukiwa nje ya klabu za Simba na Yanga, siku ya mchezo baina ya timu hizo utajikuta unahusika kwa namna moja au nyingine.

Wakati presha ikizidi kupanda kuelekea mechi hiyo ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu kati ya klabu hizo kongwe zaidi hapa nchini itakayopigwa kesho, Novemba 5, makocha wa timu pinzani katika mashindano hayo wametia neno juu ya mchezo huo wakiuangalia mtanange huo utakavyokuwa.

Hawa hapa ni makocha wa baadhi ya timu nchini namna wanavyoutazama mchezo huo kiufundi.

Mwinyi Zahera (kocha timu ya vijana Coastal Union)

Aliyekuwa kocha wa Coastal Union, Mwinyi Zahera anasema timu zote zinacheza soka la tofauti kulingana na mbinu za makocha wanavyotaka zicheze.

Zahera anasema Simba licha ya kucheza soka la taratibu, imekuwa inacheza mpira wa pasi na hutulia kupanga mashambulizi, na kwamba mbinu zao hizo hatashangaa kama zitaipa ushindi.

Akiizungumzia Yanga, Zahera anasema inacheza soka tofauti na Simba ikiwa inacheza la kasi ikikaba kwa nguvu na kufanya mashambulizi ya haraka.

“Timu zote zinacheza kwa utofauti mkubwa. Unawaona Simba wao wanacheza soka la taratibu. Wanacheza mpira wa pasi na wanashinda na inaonekana wanaitendea haki falsafa ya kocha wao,” anasema kocha huyo.

“Simba hawaonekani kupata shida, ndio maana unaona walicheza hivyo walipokutana na Al Ahly na walicheza mpira mkubwa kwa mbinu hizohizo na kama wakirudia kiwango kile Jumapili itakuwa mechi ngumu.

“Yanga wako tofauti na Simba wao wanakaba sana na wana kasi ya kumalizia mashambulizi yao. Ile kasi yao inawafanya wapinzani kushindwa kujipanga haraka. Wachezaji wa Yanga wana akili, ubora na mbio ndio maana unaona wanafika kwa idadi kubwa eneo la wapinzani na wanafunga.

“Hii mechi itakuwa ngumu sana na mimi naona itaamuliwa kwa makosa madogo ya kibinadamu kwa wachezaji. Ambaye atashindwa kumdhibiti mwenzake vizuri atajikuta anapoteza. Pia sioni kama itakuwa mechi ya mabao mengi sana.”

Goran Kopunovic (Tabora United)

Kocha wa Tabora United, Goran Kopunovic anasema ingawa hajapata muda wa kuzifuatilia kwa muda mrefu timu hizo mbili, kwake anaamini itakuwa mechi ngumu lakini itaamuliwa na ubora wa mbinu za makocha na ubora wa wachezaji.

“Nimekuwa natumia muda mwingi kuangalia wapinzani ninaokutana nao kwenye ligi, ni mara chache sana kuziona hizo klabu mbili, lakini haitakuwa mechi rahisi. Kwa timu yoyote nadhani kocha ambaye atafaulu kwa mbinu dhidi ya mwenzake atashinda au upande ambao wachezaji wake watacheza kwa ubora,” anasema Goran ambaye amewahi kuifundisha Simba akiifunga Yanga mara moja.

Zuberi Katwila (Mtibwa Sugar)

Naye kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila anasema licha ya mchezo huo kuwa mgumu, lakini anafurahi mechi hiyo itachezwa na kuamuliwa kwa mbinu za kisayansi za soka.

Katwila anasema ubora wa wachezaji wa timu hizo ndio utatengeneza matokeo ya mechi hiyo kutokana na falsafa za makocha kuwa sawa kwa kucheza mpira wa kushambulia.

“Mpira umebadilika sana kwa sasa. Zamani mechi kama hizi zilikuwa zinategemea nguvu kubwa ya nje ya uwanja, lakini sasa ni tofauti. Mtazamo wangu ni kwamba itakuwa ni mechi ambayo itaamuliwa na mbinu za kisayansi ya mpira kwa manaa ufundi wa uwanjani,” anasema Katwila.

“Timu zote zinacheza soka la kushambulia, ingawa zinatofautiana utekelezaji wa majukumu. Zote zitacheza mpira wa wazi wa kushambulia hapa, wanaokwenda kutengeneza matokeo ni ubora wachezaji ambao watacheza kwa akili kubwa, watashinda.”

Mecky Maxime (Kagera Sugar)

Maxime anasema dabi ni moja kati ya michezo migumu kuliko watu wanavyodhani kwani kila upande hupambana kuweka historia na sio kukusanya pointi kama ilivyozoeleka kwenye mechi zingine za ligi.

Kocha huyo anasema kuwa katika mtanange huo Simba ikishinda itakuwa juu na Yanga ikishindwa itashuka chini, hivyo mtihani utakuwa mzito kwani rekodi ya kusalia kileleni ni jambo la heshima kwa watani

“Naona ugumu mkubwa na hakutamalizika kwa sare kama mchezo uliopita, lazima kuna mmoja atapoteza kwani timu zote zimetoka kushiriki mashindano ya kimataifa ambapo kote huko wamefanya vyema,” anasema.

Kutakuwa na upinzani ukizingatia hakuna aliye chini ya mwenzake kwa ubora na uwezo wamelingana vingi hali inayoongeza ushindani ambao unazua kitendawili cha nani atafaulu mtihani huo mzito ila atakayetumia nafasi vizuri atashinda.”

Kessy Mziray (Alliance)

Kocha wa zamani wa Alliance, Kessy Mziray anasema Simba na Yanga zina makocha wenye utaalamu, na Yanga itaingia ikilenga kisasi kutokana na kupoteza mechi mbili - moja ya ligi (msimu uliopita) na Ngao ya Jamii (msimu huu).

Anasema Simba itaingia mchezoni kwa kujiamini kwani ilikuwa na rekodi nzuri msimu uliopita japokuwa ina udhaifu kadhaa ambao wapinzani wao wakiweza kuutumia wataweka rekodi nyingine mpya.

“Safu ya ulinzi ya Simba haiko vizuri sana, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuadhibiwa na Yanga kwani wako vizuri katika maeneo mengi hasa viungo wa kati na kila anayeingia ana uwezo wa kufunga.”

Edna Lema (Biashara United)

Edna anasema mchezo huo anaupa asilimia 50 kwa kila timu, lakini Simba inatakiwa kuwa makini zaidi ili kuhakikisha hairuhusu mabao kama rekodi zake zinavyoonyesha.

“Wamekuwa wakifungwa katika mechi japokuwa wanafunga, lakini wameruhusu (mabao) hali inayopunguza uhakika mkubwa wa kupata matokeo mbele ya wapinzani wao ambao hawana rekodi ya kuruhusu mabao mengi,” anasema kocha huyo aliyewahi pia kufundisha timu ya Yanga Princess inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

Chanzo: Mwanaspoti