Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha wanaolipwa mkwanja mrefu AFCON 2023

Djamel Belmadi Djamel Belmadi.

Mon, 8 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni Januari 13 nchini Ivory Coast ambapo mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) yanatarajiwa kuanza. Kuna mengi yanayosubiriwa na miongoni mwa hayo ni uwapo wa makocha tajiri msimu huu.

Hapa tunakuletea orodha ya makocha 10 wanaolipwa mishahara mikubwa zaidi ambao watakuwepo kwenye mashindano mwaka huu.

10.  Avram Grant (Zambia) Kocha huyu wa zamani wa Chelsea na West Ham United, kabla ya kuajiriwa kuifundisha Zambia aliwahi kuifundisha timu ya taifa ya Ghana kuanzia 2014 hadi 2017. Kwa mezianalipwa mshahara wa Euro 25,000.

9. Rigobert Song (Cameroon) Baada ya kuhudumu kwenye timu mbalimbali za vijana, Song alilamba dili la kuifundisha Cameroon 2022. Akaenda nayo kwenye mashindano ya  Kombe la Dunia Qatar mwaka jana.

Beki huyu wa zamani anapokea Euro 29,000 kwa mwezi. Hajawahi kushinda taji lolote akiwa na timu hiyo ya taifa.

Tangu achukue mikoba ya kuifundisha Cameroon ameisimamia kwenye mechi tisa, akishinda tano, sare moja na kufungwa tatu.

8. Chris Hughton (Ghana) Ni mmoja kati ya makocha wapya na hii itakuwa ni mara yake ya kwanza kuiongoza timu kwenye Afcon. Alichukua mikoba ya kuinoa Ghana mwaka jana ikiwa  ni baada ya kuhudumu kama mkurugenzi wa ufundi kwa mwaka mmoja. Hadi sasa ameiongoza kwenye mechi tisa, akishinda nne, sare mbili na kufungwa tatu. Kwa mwezi anapata Euro 46,000.

7. Aliou Cisse (Senegal) Ndiye bingwa mtetezi wa mashindano haya akirejea na vijana wake wa Senegal. Cisse ambaye wakati wa uchezaji wake aliwahi kuitumikia PSG na amekuwepo kwenye kikosi cha Senegal tangu 2015 akiwa mmoja kati ya makocha waliohudumu kwenye timu moja kwa muda mrefu watakaokuwepo kwenye mashindano ya mwaka huu. Kocha huyu analipwa Euro 46,000 kwa mwezi. Mkataba wake unamalizika mwaka huu.

6. Jose Peseiro (Nigeria) Peseiro ambaye pia ni raia wa Ureno alikuwa akipata mshahara wa Euro 70,000 kwa mwezi, lakini Septemba, mwaka jana mkataba wake ulirefushwa na kupunguziwa hadi kufikia Euro 50,000 kwa mwezi.

Anatajwa kukalia kuti kavu kutokana na kiwango cha timu ya taifa ya Nigeria kutoridhisha katika siku za hivi karibuni.

5. Hugo Broos (Africa Kusini) Kocha huyu kutoka Ubelgiji amekuwa akihudumu kwenye kikosi cha Afrika Kusini tangu 2021. Mkataba wake unamalizika 2026, lakini hajawahi kuipatia timu hiyo taji lolote ingawa historia yake kwenye mashindano haya aliwahi kushinda kombe akiwa na Cameroon 2017. Kwa mwezi anakunja Euro 50,000.

4. Walid Regragui (Morocco) Akiwa mmoja kati ya makocha waliofanya vizuri kwenye Kombe la Dunia mwaka juzi akiifikisha nusu fainali Morocco, Walid anakunja Euro 60,000 kwa mwezi.

Kocha huyu ana mkataba wa kuifundisha Morocc hadi 2025 na kwa nyakati zote amekuwa akifurahia mafanikio aliyoyapata akiwa na kikosi hicho. Mbali ya fedha pia ni mmoja kati ya makocha tishio wanaotarajiwa kuwepo kwenye mashindano ya mwaka huu.

3. Rui Vitoria (Misri) Kocha huyu ana mkataba wa kuitumikia Misri hadi  2026, na aliajiriwa 2022. Huyu ni mmoja kati ya makocha bora kutoka Ureno ambaye mfukoni mwake ana medali za ubingwa wa ligi nchini humo mara mbili.

Ilihitaji nguvu ya ziada kuweza kumpata ndio maana taifa hilo linamlipa Euro 200, 000 kwa mwezi. Tangu achukue mikoba ya kuinoa nchi hiyo ameisimamia kwenye mechi 13, ikashinda 11, sare moja na kufungwa moja.

2. Jean-Louis Gasset (Ivory Coast) Kocha wa wenyeji wa mashindano hayo naye ameingia kwenye orodha hii. Anakunja Euro 108,000 kwa mwezi.  Tangu aanze kuifundisha Ivory Coast 2022 amepoteza mechi mbili kati ya 14, huku tisa akishinda na tatu sare.

1. Djamel Belmadi  (Algeria) Kocha huyu ambaye ni raia wa Algeria ndiye anaongoza kwa kuwa na mshahara mkubwa zaidi kwenye mashindano hayo. Mshahara wake wa Euro 208,000 kwa mwezi ameanza kuupokea tangu 2018 alipochukua mikoba ya kuifundisha timu hiyo.

Belmadi ameisaidia nchi hiyo kushinda taji moja la Afcon mwaka 2019 na pia aliwahi kuifundisha timu ya taifa ya Qatar. Pia, aliwahi kuchukua tuzo ya kocha bora wa mwaka wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) 2019.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live