Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha wanafukuzwa kisomi sana

Cedrick Kazeeee Cedrick Kaze

Sat, 4 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Klabu za Tanzania zimeonekana kustaarabika sana siku hizi pindi zinapoamua kuwatimua makocha tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Zamani ilikuwa zikiachana na makocha zinaibuka hadharani na kusema kuwa tumemfukuza au kumtimua kocha kwa sababu hii na ile.

Lakini hivi sasa mambo yanakwenda kistaarabu sana na wana lugha zao zisizoumiza pindi wanapofikia uamuzi wa kumfukuza kocha ambayo mojawapo ni kusema tumefikia makubaliano binafsi ya kuvunja mkataba na kocha.

Hii ya makubaliano binafsi mara nyingi huwa kwa wale makocha ambao mikataba yao haina vipengele vigumu sana kulipwa pindi inapovunjwa, hivyo klabu inakuwa haitumii gharama kubwa ya fedha katika kulipa stahiki zao.

Sasa kwa wale ambao mikataba yao ni migumu kuvunjwa na klabu zinatakiwa kulazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha ili kuivunja, kumekuwa na ujanja wa kubadilisha majukumu kwa makocha na kuwapa yale ambayo yatawafanya washindwe wenyewe na kuamua kutupa taulo.

Na wadhifa ambao wamekuwa wakiutumia sana kutengeneza mazingira ya kumfanya kocha ashindwe mwenyewe ni ule wa ukurugenzi wa ufundi au ukuu wa soka la vijana.

Kwa soka letu, hizo nyadhifa huwa hazina kazi yoyote maana timu zenyewe za vijana huwa zinakusanywa tu kipindi fulani halafu baada ya hapo kocha anakuwa hana kazi yoyote ya kufanya jambo ambalo kwa taaluma yake linakuwa linamshusha.

Kwenye nafasi ya ukurugenzi wa ufundi nako kunakuwa hakuna kazi yoyote ya kufanya maana mwishowe anakuwa hana mamlaka yoyote kwenye timu na kocha mkuu ndio anakuwa bosi.

Nimeona tayari kwenye Ligi Kuu msimu huu kuna kocha ambaye amebadilishiwa majukumu na kupewa yale ya ukurugenzi wa ufundi wa klabu yake baada ya kuwa na mwenendo usioridhisha kwenye ligi.

Kifupi huyo amefukuzwa kwa lugha isiyoumiza na kama hamuamini subirini muda utatoa majibu.

Chanzo: Mwanaspoti