Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha waliowahi kuionea PSG

Carlo Ancelotti.jpeg Carlo Ancelotti

Sun, 11 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Carlo Ancelotti. Thomas Tuchel. Unai Emery. Mauricio Pochettino. Laurent Blanc. Gerard Houllier na Christophe Galtier. Kwa kuwataja kwa uchache, ndio makocha waliowahi kuinoa Paris Saint-Germain.

Makocha wa hadhi kubwa kabisa. Wapo wenye medali za ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, tena wengine zaidi ya moja, lakini hawakufanya hivyo walipokuwa Parc des Princes. PSG inahitaji taji hilo la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kutimiza hilo imekuwa ikifanya usajili wa maana kwelikweli kwenye kikosi chao, ikiwamo kunasa wakali kama Lionel Messi, Neymar, Kylian Mbappe, Sergio Ramos, Zlatan Ibrahimovic, Achraf Hakimi, Gianluigi Donnarumma, Ander Herrera na Georginio Wijnaldum – kwa kuwataja kwa uchache, lakini wapi. Hakuna taji.

Na siku chache zilizopita, wamemfuta kazi kocha Galtier kwa kushindwa kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya licha ya kwamba aliwapa ubingwa wa Ligue 1.

Na kinachoelezwa ni kwamba mabosi wa Paris Saint-Germain wamemgongea simu Zinedine Zidane , AKA Zizzou wakimtaka aende akachukue mikoba ya kuinoa miamba hiyo ya Parc des Princes.

Lakini, kocha huyo wa zamani wa Real Madrid, Zidane amekataa ofa hiyo ya kwenda kuwa bosi mpya wa miamba hiyo ya Ufaransa.

Zidane, 50, amekuwa hana kazi kwa muda mrefu, akiwa hajakubali kibarua chochote tangu alipoachana na Real Madrid mwishoni mwa msimu wa 2020-21 baada ya kurejea Bernabeu kwa mara ya pili.

Kutokana na yale mafanikio aliyopata Bernabeu, Zidane hakuwa na usumbufu wa kupata ofa za kutoka katika klabu mbalimbali katika kipinsi cha miaka miwili iliopita, lakini Mfaransa huyo bado hajapata dili tamu lililomshawishi kukubali kwenda kufanya kazi.

Staa huyo wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa awali ilidhaniwa kwamba alikuwa anasubiri kazi ya kuinoa timu ya Les Bleus kwamba kibarua kingekuwa wazi baada ya kukamilika kwa fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar, lakini kocha wa sasa Didier Deschamps alisaini mkataba mpya wa kuendelea kuinoa timu hiyo hadi 2026, wakati wa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Amerika Kaskazini.

Kutokana na kibarua cha kuinoa Ufaransa kufutika, Zidane alitarajia atarejea mzigoni kwenye kazi yake ya ukocha na kujiunga na moja ya klabu kubwa za Ulaya, lakini kinachoripotiwa kwamba amegomea kwenda kukalia kiti cha moja cha benchi la ufundi la PSG.

Kocha Christophe Galtier alifutwa kazi huk PSG baada ya kuinoa timu hiyo kwa msimu mmoja tu na kwa mujibu wa Le Parisien, mabosi wa miamba hiyo ya Paris, waliwasiliana na Zidane na kujadili uwezekano wa kwenda kufanya kazi kwenye timu hiyo kuanzia msimu ujao wa 2023-24.

Hata hivyo, Zidane aliwajibu PSG “hapana”, akipuuzia nafasi hiyo ambayo ingempatia pia mkwanja wa kutosha – ikiwa sasa anakuna kichwa ni wapi pa kwenda kufanyakazi akijipanga kurudi kwenye benchi.

Katika nyakati zake mbili alizoinoa Real Madrid, Zidane alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo, La Liga mara mbili, Klabu Bingwa Dunia mara mbili, UEFA Super Cups mara mbili na Spanish Super mara mbili.

Zidane alitajwa kuwa Kocha Bora Dunia wa timu za Klabu mwaka 2017 na 2018 baada ya kutamba kwenye soka la Ulaya na kwenye majira ya kiangazi ya mwaka jana, mshauri wake alikanusha kwamba alikuwa amejiweka tayari kwenda kurithi mikoba ya Pochettino huko PSG.

Kwa kukataliwa na Zidane, PSG waliamua kwenda kumwaajiri Galtier na kumpa mkataba wa miaka miwili, lakini badala yake akadumu na timu hiyo kwa mwaka mmoja tu na imemtimua mwishoni mwa msimu huu wa 2022-23. Hilo limekuja baada ya PSG kumaliza pointi moja tu juu ya Lens kwenye msimamo wa Ligue 1, huku kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya walikomea nafasi ya 16 bora baada ya kuchapwa jumla ya mabao 3-0 na Bayern Munich.

Makocha wengine wanaohusishwa na miamba hiyo ya Ufaransa ni Luis Enrique na Jose Mourinho. Lakini, habari mpya za hivi karibuni, matajiri hao wameanza kumfukuzia kocha wa zamani wa Bayern Munich, Julian Nagelsmann – ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuchukua mikoba hiyo ya kwenda kumnoa Mbappe.

Nagelsmann, 35, alijiondoa kwenye mbio za kuwa kocha Chelsea na Tottenham Hotspur na kinachoelezwa ni kwamba yupo kwenye mazungumzo mazuri na mabosi wa PSG, lakini mabingwa hao wa ufaransa watapaswa kuilipa Bayern fidia kama watamchukua Nagelsmann.

Thierry Henry alikuwa akipewa nafasi ya kwenda kuwa msaidizi wa Nagelsmann huko PSG, lakini nguli huyo wa zamani wa Arsenal hana mpango wa kwenda kufanya kazi ya ukocha kwenye kikosi hicho cha Parc des Princes.

Chanzo: Mwanaspoti