Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha waliomkanda mara nyingi mwamba Pep Guardiola

Legendary Managers Makocha waliomkanda mara nyingi mwamba Pep Guardiola

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kama unapenda soka, lazima utakuwa unamjua Pep Guardiola. Kiungo aliyekuwa na kipaji matata wakati wa enzi zake akiwa mchezaji, alipotamba Barcelona chini ya makocha imara, Johan Cruyff, Bobby Robson na Louis van Gaal.

Katika miaka yake 21 aliyokuwa uwanjani kama mchezaji, alipita pia kwenye nchi za Italia, Qatar na Mexico ukiweka kando kwao Hispania.

Ameitumikia pia mara 47 kwenye timu ya taifa ya Hispania, katika kipindi cha miaka tisa na kufunga mabao matano akiwa na La Roja.

Katika kipindi hicho cha miaka 21, ameshinda La Liga mara sita, Copa del Rey mara mbili, Supercopa mara nne, Kombe la Ulaya, Kombe la Washindi na European Super Cup ameshinda mara moja, yote akiwa Barca.

Alipohamia kwenye ukocha, Guardiola ameendeleza makali yake na kufanya kitu kikubwa kwenye soka. Kwa sasa anatajwa kama mmoja wa makocha mahiri kabisa duniani. Rekodi zake ukiweka kando Barcelona B, Guardiola alikinoa kikosi cha wakubwa cha Barcelona katika mechi 247, alishinda 179, sare 47 na vipigo 21. Amefunga mabao 638 na kufungwa 176 na timu hiyo aliinoa kuanzia Julai 1, 2008 hadi Juni 30, 2012.

Kisha alikwenda Bayern Munich, kuanzia Juni 26, 2013 hadi Juni 30, 2016 ambapo aliiongoza timu hiyo kwenye mechi 161, akishinda 121, sare 21 na vichapo 19. Amefunga mabao 396 na kufungwa 111.

Julai 1, 2016, alitua Manchester City, mahali ambako yupo hadi sasa, ambapo ameiongoza timu hiyo katika mechi 453, akishinda 328, sare 62 na vichapo 62. Amefunga mabao 1,115 na kufungwa 371. Amebeba mataji 37.

Licha ya umahiri huo wa kocha Guardiola, kuna makocha ambao wamempa wakati mgumu kwenye mechi alizokutana nao na kufanikiwa kupata matokeo dhidi yake. Hii hapa orodha ya makocha ambao wameshinda zaidi ya mara moja kwenye mechi zao walizokutana na Guardiola kwenye michuano tofauti.

1.Guardiola vs Klopp - mechi 29, vichapo 12

Ilipotangazwa kwamba kocha Jurgen Klopp ataachana na Liverpool mwishoni mwa msimu huu, jambo hilo limepokewa kwa masikitiko makubwa na Guardiola akisema anampoteza mpinzani wa kweli kwenye soka la England. Guardiola anafahamu namna Klopp anavyompa usumbufu wanapokutana na katika mechi 29 ambazo wameshakutana, Klopp ameshinda 12, sare sita na Guardiola amefanikiwa kushinda mara 11.

2.Guardiola vs Mourinho - mechi 25, vichapo 7

Jose Mourinho na Guardiola walianza kuonyeshana ubabe walipokutana huko Hispania kwenye mechi za El Clasico baina ya Real Madrid na Barcelona. Kisha vita yao ikahamia Ligi Kuu England kwenye Manchester derby na hakika makocha hao wawili wanapokutana tambo ni nyingi sana. Rekodi zinaonyesha wamekutana mara 25, Mourinho ameshinda saba na Guardiola mara 12, huku mechi sita baina yao zilimalizika kwa sare.

3.Guardiola vs Pochettino - mechi 24, vichapo 4

Mauricio Pochettino kwa sasa mambo yake si matamu huko Chelsea, lakini ni mmoja wa makocha wasiotetemeshwa kabisa na Guardiola kwa sababu alishawahi kumshinda zaidi ya mara moja.

Takwimu zinaonyesha Guardiola na Pochettino wamekutana mara 24 na katika mechi hizo, sare ni saba, huku Pochettino akishinda mechi 13 na Pochettino alishinda nne, kuonyesha kwamba kuna pointi za ushindi alizoweza kuokota dhidi yake.

4.Guardiola vs Solskjer - mechi 9, vichapo 4

Kama kuna kocha alimpa Guardiola wakati mgumu kwenye Ligi Kuu England basi ni Ole Gunnar Solskjaer, aliyekuwa akiinoa Manchester United na wawili hao kukutana kwenye mechi za Manchester derby. Makocha hao wawili, Guardiola na Solskjaer wamekutana mara tisa na katika mechi hizo, sare ni moja tu, huku kila mmoja akishinda mara nne na kuonyesha upinzani mkali uliopo baina yao.

5.Guardiola vs Conte - mechi 7, vichapo 4

Unaweza kusema Antonio Conte ndiye mwamba wake Guardiola kwenye zama zao za ukocha. Kwenye mechi ambazo makocha hao walikutana, Conte alishinda mara nne katika mechi saba, huku Guardiola ameibuka na ushindi kwenye mechi tatu na hakuna mchezo wowote ambao ulimalizika kwa sare baina ya miamba hiyo mara zote walizokutana. Ubora wake wote Guardiola, lakini hana kitu anachoweza kumtambia Conte.

6.Guardiola vs Wenger - mechi 11, vichapo 3

Guardiola katika timu zote alizowahi kuzinoa amekutana na kocha Arsene Wenger mara 14. Na kinachovutia ni kwamba Wenger ni miongoni mwa makocha ambao wamefanikiwa kuibuka na ushindi mbele ya mgumu Guardiola zaidi ya mara moja na katika mechi hizo, Wenger aliibuka na ushindi mara tatu, huku Guardiola akishinda nane na mechi tatu baina yao zilimalizika kwa sare.

7.Guardiola vs Arteta - mechi 11, vichapo 3

Kwenye mchezo wa raundi ya pili katika Ligi Kuu England msimu huu, Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta atajaribu kusaka ushindi wake wa nne dhidi ya Guardiola katika mechi walizokutana. Hadi sasa makocha hao wamekutana mara 11 na Guardiola ameshinda nane na Arteta mara tatu na hakuna mchezo wowote baina yao uliomalizika kwa sare. Kwenye mchezo wa raundi ya kwanza kwenye Ligi Kuu England msimu huu, Arteta alimtambua Guardiola uwanjani Emirates.

8.Guardiola vs Tuchel - mechi 12, vichapo 3

Kocha Mjerumani, Thomas Tuchel ni miongoni mwa walio wachache ambao walifanikiwa kushinda zaidi ya mara moja kwenye mechi zao walizokumbana na fundi Guardiola.

Mara 12 ambazo makocha hao walikutana, sare ni mbili tu, huku Guardiola alishinda saba na Tuchel, anayeinoa Bayern Munich kwa sasa, timu ya zamani ya Guardiola ameshinda mechi tatu.

9.Guardiola vs Ancelotti - mechi 10, vichapo 3

Mtaliano Carlo Ancelotti ni miongoni mwa makocha wenye heshima kubwa kwenye mchezo wa soka duniani. Ancelotti na Guardiola wamekutana mara 10 na katika mechi hizo sare ni moja tu, huku Guardiola akishinda sita na Ancelotti ameibuka na ushindi katika mechi tatu.

Jambo hilo limemfanya Ancelotti kuonyesha ubabe wake juu ya kocha huyo mwenye ufundi mwingi wa kuwasoma vyema wapinzani wake.

10.Guardiola vs Pellegrini - mechi 14, vichapo 2

Moja ya makocha waliopata nafasi ya kunoa timu kubwa za Ulaya ikiwamo Manchester City na Real Madrid amewahi kukutana na Guardiola katika mechi 14, ambapo kwenye mechi hizo sare ni moja tu, huku Mhispaniola, Guardiola ameshinda 11 na Pellegrini ameibuka na ushindi kwenye mechi mbili tu. Hata hivyo, jambo hilo walau linamweka kwenye orodha ya makocha waliowahi kupata ushindi dhidi ya Guardiola walau kwenye mechi mbili.

Chanzo: Mwanaspoti