Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha wakubali mfumo wa Amrouche

Stars Safarini Tunisia Makocha wakubali mfumo wa Amrouche

Mon, 4 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kikosi cha Taifa Stars kutangazwa hivi karibuni, wadau wa soka nchini wengi wamehoji juu ya kuachwa kwa wachezaji, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein 'Tshabalala' na kiungo mshambuliaji, Feisal Salum.

Taifa Stars inajiandaa na mchezo wa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) dhidi ya Algeria utakaochezwa Septemba 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa 19 Mei 1956, mjini Algers.

Algeria ndiyo vinara wa Kundi F wakiwa na pointi 15, huku tayari wakiwa wamefuzu, upande wa Tanzania ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi saba na inahitaji sare au ushindi kufuzu.

Wakati Taifa Stars ikiwa inapambana kufuzu, inatakiwa kuwaombea matokeo mabaya Uganda, ambayo inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi nne, huku mchezo wake wa mwisho ikimaliza na Niger inayoshika mkia kwa pointi mbili.

Kama Uganda itashinda mchezo wake na Niger, ambayo ishatoka kinachofanyika ni kuangaliwa mabao ya kufungwa na kufunga. Taifa Stars imefunga mabao matatu na kuruhusu mabao manne huku Uganda ikifungwa mabao sita na kufunga matatu. Makocha mbalimbali hapa nchini wameunga mkono uchaguzi wa mastaa wa kocha mkuu wa Stars, Adel Amrouche kwani katika mechi hiyo kinachohitajika ni pointi moja au tatu. Kocha wa Biashara United, Aman Josiah akizungumza kutokana na aina ya kikosi kilichoitwa ni wazi ni wale ambao wanaweza kuwa watumwa kwa mpira ndani ya dakika 90.

Josiah alisema mchezo huo ni wa kwenda kufuzu kwa timu ya Taifa, hivyo kocha anaangalia ni nini ambacho anatakiwa kukifanya kwa kikosi anachokiita. "Ameita wachezaji ambao watakuwa ni watumwa kwa dakika zote 90, wawe na mpira au wasiwe nao, yaani lazima wapambane ndani ya uwanja kuhakikisha matokeo yanapatikana. "Pia uzoefu na ndiyo maana hata Bocco (John) yupo kikosini, kukosekana kwa Feisal (Salum) ni lazima uangalie unahitaji viungo wa namna gani kulingana na mpango wa mechi husika," alisema kocha huyo.

Kocha wa zamani wa Eagle FC, Joseph Kanakamfumu alisema watu wengi wanashangaa kuachwa kwa Kapombe na Tshabalala kutokana na ubora wao wa kushambulia, lakini kocha wa Taifa Stars ameangalia aina ya mchezo.

"Wanasahau hata mechi ya mwisho hapa walicheza mfumo wa 3-5-2 (dhidi ya Niger) na Job (Dickson), Novatus (Dismas) walikuwa kwenye kiwango bora.

"Licha ya Algeria kufuzu, itataka kushambulia, kocha anahitaji pointi, kwahiyo naona ni sawa kwenda na kikosi hiki kwa sababu Job na Novatus ni wazuri kwenye kupiga mipira mirefu," alisema Kanakamfumu.

Kwa upande wake, kocha wa zamani wa KMC, Ahmad Ally alisema: "Naheshimu uamuzi wa kocha mkuu kwa sababu anaita kikosi kulingana na wapinzani wake alivyowaona, kuna muda kinaitwa kikosi kulingana na mashindano yanahitaji nini."

Taifa Stars kama itafuzu kwenda AFCON, ambayo itafanyika nchini Ivory Coast itakuwa ni mara ya tatu baada ya kufanya hivyo 1980 na 2019.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live