Wakati sababu kadhaa zikitajwa kuchangia kutimuliwa kwa kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' na wasaidizi wake wawili licha ya takwimu bora alizonazo tangu alipojiunga na timu hbiyo, Januari mwaka huu, nyota wa zamani wa soka na makocha wameonekana kushangazwa na uamuzi huo uliotangazwa jana.
Licha ya mtendaji mkuu wa Simba, Imani Kajula kutoeleza sababu za kufikia uamuzi kupitia taarifa yake kwa umma jana, gazeti hili linafahamu kuwa kichapo cha mabao 5-1 ambacho Simba ilikipata kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumapili mbele ya Yanga kilichangia kwa kiasi kikubwa kuhitimisha ajira ya Robertinho.
"Klabu ya Simba imefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba na kocha mkuu wa kikosi cha kwanza Roberto Oliveira Goncalves Do Carmo (Robertinho). Vilevile tumefikia makubaliano ya kusitisha mkataba wa kocha wa viungo Corneille Hategekimana.
"Katika kipindi cha mpito, kikosi chetu kitakuwa chini ya kocha Daniel Cadena akisaidiwa na Seleman Matola," ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo ya Simba.
Robertinho ametimuliwa na Simba akiwa amepoteza mechi moja tu ya Ligi Kuu tangu alipojiunga nayo, Januari mwaka huu ambapo ameiongoza katika mechi 17 za ligi, ikishinda 14, kutoka sare mbili na kupoteza hiyo moja huku ikifunga mabao 42 na kuruhusu mabao 15 tu.
Kocha huyo anaondoka akiiacha Simba na taji moja ambalo ni la Ngao ya Jamii msimu huu, akiiongoza kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita ambao pia aliifanya imalize katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Rekodi na takwimu hizo za Robertinho zimeonekana kuwafanya wadau wengi wa soka kuamini kwamba uongozi wa Simba umefanya uamuzi wa pupa kumuacha baada ya kupoteza mbele ya Yanga.
Lakini kana kwamba haitoshi, jambo lingine ambalo limewashangaza wadau hao ni kitendo cha uamuzi huo kuchukuliwa muda mfupi kabla ya Simba kuanza mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo mechi ya kwanza watacheza nyumbani dhidi ya Asec Mimosas, Novemba 25.
Kocha mkuu wa Biashara United ya Mara, Aman Josiah alisema Simba haijafanya sahihi kuachana na Robertinho katika kipindi hiki.
"Malengo waliyoingia nayo ndio kitu muhimu na kikubwa. Kwenye Ligi hakuna timu ambayo haijapoteza hata hao Yanga walifungwa na Ihefu. Ukiangalia kwenye msimamo hawapo pabaya na hata kimataifa wapo vizuri,"alisema Aman.
Nyota wa zamani wa Simba, Bakari Kigodeko alisema hakutegemea Simba ingemfukuza kocha baada ya mechi ya juzi.
"Wamekosea kumfukuza kisa tu kufungwa na Yanga. Ukiangalia wachezaji wenyewe tu walikuwa wanacheza bila kufuata mbinu za kocha. Yeye ameifunga Yanga mara ngapi? kiukweli Simba imekosea kuachana na kocha," alisema Kigodeko.
Licha ya Simba kutoanika sababu za kuachana na Robertinho, gazeti hili linafahamu kuwa mbali na kichapo kutoka kwa Yanga, sababu nyingine ambazo zimepelekea timu hiyo kuchukua uamuzi huo ambazo imezinasa kutoka kwa baadhi ya vigogo wa Simba ni mahusiano duni kati yake na baadhi ya wachezaji, kiwango kisichoridhisha katika michezo mingi hata ile ambayo timu ilipata ushindi lakini pia presha kutoka kwa kundi kubwa la mashabiki.
Inaripotiwa kuwa Robertinho alishindwa kumaliza mpasuko uliopo kikosini kwa baadhi ya wachezaji jambo ambalo lilisababisha kupoteza imani na utawala katika vyumba vya kubadilishia nguo pamoja na uwanja wa mazoezi.
Hata hivyo, nyota wa zamani wa Simba, Fikiri Magoso alisema Simba ina matatizo mengi zaidi ya kocha hivyo kumtimua sio suluhisho.
"Watu wa mpira tunajuana, kikubwa waangalie wapi kwenye makosa kisha wafanye marekebisho mapema kabisa. Simba kweli kuna shida nyingi hata ndani zipo, wakati huo huo kwenye uwanja timu ulikuwa inaruhusu mabao licha ya kufunga," alisema Magoso.
Kocha wa Ruvu Shooting, Khalid Adam alisema inawezekana kuna sababu nyingine ambayo ilikuwepo ndani ya timu na matokeo yametumika kama kigezo kingine tu.
"Muda mwingine ni kuna vitu vilikuwa vinaendelea na walikuwa wanasubiri tu kitu watokee wamtimue. Naumia kama kocha kuona mwenzangu kapoteza kazi lakini napongeza pia ujio wa Matola (Seleman),"alisema Adam.
Mshambuliaji wa zamani wa Moro United, Benedict Ngassa alisema kilichoiangusha Simba ni usajili ilioufanya na sio kocha Robertinho.
"Ukiangalia kikosi cha wachezaji waliocheza msimu uliopita na msimu huu ni wawili tu Ngoma na Malone ndio wanacheza kikosi cha kwanza. Wale wengine wamepewa nafasi lakini hawaonyeshi kama waliocheza msimu uliopita, hawa wa msimu uliopita nao wameshacheza mechi nyingi hivyo wamechoka," alisema Ngassa.
Mshambuliaji wa zamani Simba, Zamoyoni Mogela alisema ubora wa wachezaji Simba umepungua na hilo lilijionyesha dhidi ya Yanga.
"Mpira ni mchezo wa wazi kwa hiyo kila mmoja aliona ipi timu ambayo imekamilika. Viongozi wanatakiwa waangalie tiba ya haraka ili wamalize tatizo," alisema Mogella.