Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha makini wa kuinusuru Chelsea ni hawa jamaa

Makocha Chelsea.jpeg Makocha makini wa kuinusuru Chelsea ni hawa jamaa

Thu, 12 Jan 2023 Chanzo: Mwanaapoti

Graham Potter presha inapanda tu huko kwenye kiti chake cha ukocha Chelsea. Kocha huyo aliyetua Stamford Bridge akitokea kuinoa Brighton ameshuhudia matokeo mabovu zaidi akiwa kwenye kikosi cha The Blues katika wiki za karibuni.

Ndani ya muda mchache tu akiwa na timu hiyo, Chelsea imejikuta ikitupwa nje kwenye makombe yote ya ndani, Kombe la Ligi na Kombe la FA, ambapo juzi Jumapili, chama hilo lilikubali kichapo cha kudhalilisha cha mabao 4-0 kutoka kwa Manchester City.

Potter amekuwa na mwanzo wa hovyo zaidi kwa makocha waliowahi kuinoa Chelsea kwenye mechi zinazoanzia 11 katika kipindi cha miaka 30 ya karibuni. Kutokana na hilo, gwiji wa Chelsea, Frank Leboeuf amesema "inatosha" baada ya Man City kuifanyika manyanyaso makubwa Chelsea uwanjani na kusisitiza Potter aondoke.

Wakati mashabiki wa Chelsea wakiimba nyimbo za kutaja jina la kocha wao wa zamani, Thomas Tuchel - kocha wa Man City, Pep Guardiola ametaka bosi wa Chelsea endelee kumpa muda Potter wa kuendelea kubaki Stamford Bridge.

Tayari kuna makocha wanaoangaziwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuja kunusuru hali ya mambo huko Stamford Bridge.

MAURICIO POCHETTINO

Muargentina na kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino anapewa nafasi kubwa zaidi ya kwenda kumbadili Potter baada ya kuonekana kwamba mguu wake hautoshi kwenye viatu vya kuinoa Chelsea.

Pochettino ana uzoefu wa kufanya kazi kwenye timu zenye presha kubwa ikiwamo Paris Saint-Germain. Katika nyakati zake alizokuwa Spurs, Pochettino hakuwa na wakati mbaya dhidi ya mashabiki wa Stamford Bridge hivyo maisha yake hayawezi kuwa magumu.

BRENDAN RODGERS

Kocha wa Leicester City, Brendan Rodgers ana historia na Chelsea, akiwahi kukinoa kikosi chao cha akiba mwaka 2006 na 2008. Thamani yake imeshuka kidogo baada ya Leicester City kuwa na mwanzo wa hovyo kwenye Ligi Kuu England msimu huu, lakini hilo halifichi ukweli kwamba Rodgers bado ni kocha anayeheshimika. Kutokana na hilo, Chelsea inaweza kuhamia kwenye kocha huyo aliyewahi kukaribia kabisa kubeba taji la Ligi Kuu England akiwa na Liverpool.

DIEGO SIMEONE

Muargentina, Diego Simeone amekuwa kocha wa Atletico Madrid tangu mwaka 2011 na anatajwa kuwa ndiye kocha anayelipwa pesa nyingi zaidi duniani, akipokea Pauni 36.2 milioni kwa mwaka. Simeone, 52, ana CV inayovutia kwelikweli, lakini hatazamwi kama mtu anayefaa zaidi kwenye kikosi cha Chelsea kutokana na kusajili makinda wengi na yeye ni mtu wa kutaka wapiga kazi ambayo tayari wamekomaa kwa ajili ya kuleta matokeo ndani ya uwanja.

ZINEDINE ZIDANE

Zinedine Zidane alikuwa akisubiri kazi ya kuinoa timu ya taifa ya Ufaransa, ambayo imemponyoka baada ya Shirikisho la soka la Ufaransa kuamua kumwongezea mkataba Didier Deschamps hadi 2026. Jambo hilo linamfanya Zidane sasa kufikiria kurudi kwenye kazi ya ukocha baada ya kuwa nje ya uwanjani tangu alipoachana na Real Madrid mwishoni mwa msimu wa 2020-21. Zidane anaweza kuwa chaguo sahihi la kwenda kunusuru hali ya mambo kwenye kikosi cha Chelsea kurudisha furaha.

THOMAS TUCHEL

Wanasema usirudi nyuma, lakini kwa mashabiki wa Chelsea baada ya kuona timu yao ilichofanywa na Man City juzi Jumapili, walitaka Tuchel arudi haraka. Kipindi chama hilo lilipokuwa chini ya Mjerumani huyo, Man City iliteseka sana kupata ushindi mbele ya The Blues, lakini ilimfuta kazi Septemba mwaka jana na matamanio ya mashabiki wa Chelsea kwa sasa ni tajiri mmiliki wa timu hiyo, bilionea Todd Boehly akubali tu alikosea na kumrudisha Tuchel kwenye benchi la ufundi.

Mechi zijazo za Chelsea

-Januari 12 vs Fulham (ugenini)

-Januari 15 vs Crystal Palace (nyumbani)

-Januari 21 vs Liverpool (ugenini)

-Februari 3 vs Fulham (nyumbani)

-Februari 11 vs West Ham (ugenini)

-Februari 15 vs Dortmund (ugenini)

Chanzo: Mwanaapoti