Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha hawa watajwa kumrithi Benchikha Simba

Makocha  Dzv Makocha hawa watajwa kumrithi Benchikha Simba

Fri, 3 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kuondoka kwa Abdelhak Benchikha, timu ya Simba fasta imeanza mchakato wa kutafuta kocha mpya atakayerithi mikoba ya Mualgeria huyo ikipanga kukamilisha ishu hiyo kabla ya msimu huu kumalizika Mei 28, 2024.

Mabosi wa Simba walikaa kikao baada ya kuondoka kwa Benchikha aliyesepa na wasaidizi wake Farid Zemit na Kamal Bougnan, na kuamua kuanza mara moja mchakato wa kupata mrithi wake ambaye atainoa walau mechi tatu za mwisho msimu huu, ili ajue wapi pa kuanzia katika usajili dirisha kubwa likifunguliwa.

Licha ya Simba kufanya kuwa siri, lakini Mwanaspoti inajua Wekundu wa Msimbazi wanatafuta kocha haraka ili aweze kusimamia shoo nzima ya usajili ambao timu hiyo imepanga kufanya kufuru kwa kushusha majembe yatakayoipambania na kurejesha ufalme ilioupoteza misimu mitatu sasa.

"Kama tulivyoongea mwanzo wachezaji wengi wanamaliza mikataba na tulisitisha mazungumzo ya kuwapa mikataba mipya. Sasa hatuna kocha mkuu nani atasajili? Tunataka kupata kocha kabla ya ligi kuisha ili awaone wachezaji na kujua anaanzia wapi kwenye usajili. Pia kushauri nani atoke na nani abaki kati ya hawa ambao mikataba yao inafika ukomo msimu huu," amesema mmoja wa viongozi wa Simba na kuongeza:

"Hatutatangaza makocha waombe kazi kwetu, lakini tuna baadhi ya makocha Tuliwaona na tumeanza maongezi. Tunataka kufanya jambo hili kwa weledi zaidi na kupata kocha atakayeendana na falsafa zetu na kutupa kile tunachohitaji."

Licha ya kutoweka majina ya makocha wanaozungumza nao, lakini moja ya sifa za kocha ambaye Simba inamtaka kwa sasa ni yule atakayekuwa na ubora wa kutengeneza wachezaji na kuleta usawa kikosini.

Simba inataka kocha atakayewajengea uwezo wachezaji na kupata timu itakayocheza kwa muunganiko, umoja na mshikamano bila kuwa na matabaka.

Sifa nyingine ambayo Simba inaizingatia kupata kocha mpya ni lazima awe na uzoefu wa kutosha kwenye soka la Afrika, hususan katika michuano ya CAF ambayo timu hiyo kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa ikiishia robo fainali.

Mwanaspoti inajua katika makocha wanaofuatiliwa kwa karibu na vigogo wa Msimbazi wengi wao waliwahi kuzungumza nao hapo kabla, lakini dili kutua unyamani hazikukamilika kwa sababu mbalimbali.

Miongoni mwa makocha hao ni Msenegali Lamine N'Diaye ambaye kwa sasa ni kocha wa TP Mazembe, lakini kabla ya hapo aliwahi kuzinoa Horoya ya Guinea, Al Hilal ya Sudan, Maghreb de Fes ya Morocco, Coton Sports ya Cameroon na timu ya taifa ya Senegal.

Kocha huyo msimu huu ameifikisha TP Mazembe hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ukiwa ni msimu wake wa kwanza.

Mwingine ni Mreno Alexandre Santos, kocha mkuu wa Petro de Luanda ya Angola ambayo msimu huu imetolewa katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kocha huyo pia aliwahi kuwindwa na Simba 2022, lakini dili lake halikukamilika.

Yupo pia Omar Najhi, Mwingereza mwenye asili ya Morocco ambaye alizidiwa kete na Benchikha kwani alikuwa kwenye rada za Simba wakati alipofukuzwa Oliveira Roberto 'Robertinho'.

Kocha huyo aliyewahi kuzifundisha Wydad Casablanca na Mouloudia za Morocco kwa sasa yupo huru baada ya kuchana na Ittihad Tanger ya nchini humo.

Hao ni baadhi ya makocha ambao inaelezwa wapo kwenye listi ndefu iliyopo mezani kwa Simba huku Juma Mgunda naye akifikiriwa kubakizwa kikosini hapo kama kocha msaidizi endapo watapata kocha mkuu.

Kwa sasa Simba ipo chini ya Mgunda anayekaimu nafasi ya kocha mkuu akisaidiwa na Selemani Matola aliyewahi kuwa kiungo na nahodha wa zamani wa timu hiyo.

Simba iliyo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na alama 47 baada ya mechi 22, itashuka uwanjani tena Ijumaa, Mei 3 kucheza na Mtibwa Sugar inayobuluza mkia na alama 17 baada ya mechi 23.

Chanzo: Mwanaspoti