Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliwahi kunukuliwa kwenye hotuba zake, akiwaambia wasaidizi wake akisema; ‘Ukinizingua tunazinguana? Ikiwa ni njia ya kuwakumbusha kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Sasa unaambiwa, hata kwenye soka wapo makocha ambao hawana mchezo kwenye kazi zao na wachezaji wakizingua nao wanawazingua kinomanoma!
Hawa ni aina ya makocha ambao ni wakali kwelikweli na wasiopenda mizaha kazini na kwa wachezaji waliowahi kufanya kazi nao wanajua ukweli huo, kwani licha ya kuwa watu wenye ucheshi, utani na ushikaji mwingi na mastaa, lakini ikija ishu ya kazi wanawachenjia kama hawawajui.
Kitu cha kujivunia ni kwamba ukali wao umekuwa msaada mkubwa kwa vikosi walivyowahi au wanavyovifundisha kuwa na umakini uwanjani na utimamu wa mwili na hapa chini ni makocha hao ambao hawachelewi kuliamsha pale wachezaji wakimzingua!
MECKY MAXIME (KAGERA SUGAR)
Nahodha na nyota huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars ni kati ya makocha vijana wenye uwezo mkubwa aliyebahatika kuvinoa vikosi kadhaa ikiwamo timu aliyoitumikia kwa muda mrefu, Mtibwa, Kagera Sugar aliyonayo sasa na hata zile za taifa.
Kocha huyu ni miongoni mwa makocha bora na wazuri lakini wasio na masihara wakiwa katika majukumu ya kazi na hakuna mchezaji anayeleta mdhaha wanapokuwa mazoezi hakuna mchezaji ambaye anaweza kuzembea mbele ya kocha huyo.
Mwanaspoti limezungumza na baadhi ya wachezaji ambao amewafundisha na anaowafundisha kwa sasa.
“Kocha Mecky sio mchezo kwanza mazoezi yake anayendesha kisela sana ukizingua anakupiga dongo unacheka na maisha yanaenda lakini lazima utatekeleza tu kilichomkwaza,” anasema George Kavila mchezaji wa zamani wa Kagera Sugar.
Anasema Maxime ukizingua anakuzingua mara mbili baada ya kazi hana kinyongo na mtu lakini wakati wa kazi anahitaji utulivu na kujituma.
Kocha huyo amekiri huwa hataki na wala haitaji mchezo katika kazi na wachezaji wanalitambua hilo bila ya kufanya hivyo kutoboa ni vigumu.
“Wachezaji wetu bila ya kuwa mkali hawakuelewi ili mwende sawa ni lazima usicheke nao wakati wa kazi baada ya hapo tunacheka vizuri tu, mimi nikisema kimbia alafu anatembea hapo lazima nibadilike,” anasema.
Aidha Mecky anasema hata hivi karibuni kuna picha ilitembea mitandaoni ikimuonyesha akiwa juu ya kichuguu wakati wa mazoezi na alipigwa na wachezaji wake hao hao lakini kwa kuwa mazoezi yalikuwa yamemalizika ameiona na kucheka tu.
ZUBERY KATWILA (MTIBWA)
Katwila mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar na Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kwa kumtizama hauwezi kulijua balaa lake mpaka ukae nae kwa ukaribu.
Ukitizama kikosi anachokinoa mzawa huyu utaona utofauti kwa wachezaji wake kutokana na nidhamu kubwa waliyokuwa nayo ndani na hata nje ya uwanja.
Katwila amekinoa kikosi cha Mtibwa Sugar kwa muda mrefu kabla ya kuamua kubadilisha upepo na kwenda kuifundisha Ihefu.
Mmoja wa wachezaji wa Ihefu aliiambia Mwanaspoti kuwa Katwila awapo mazoezini na hata kwenye mechi ni mkali kama haujamzoea unaweza kushindwa kucheza.
“Ukimuona mkiwa mnaongea kawaida ni mpole sana tena mnyenyekevu lakini hataki ujinga kabisa, sisi wachezaji kuna wakati tunajisahau akiwepo karibu akili inakuwa inafanya kazi muda wote,” alisema mchezaji huyo.
JAMHURI KIHWELO ‘JULIO’
Kocha mwenye maneno mengi. Mzawa huyu amezinoa timu mbalimbali hapa nchini kwa mafanikio makubwa licha ya sasa kuwa huru tu na majukumu yake mengine.
Julio amekinoa kikosi cha Simba kwa muda mrefu akisaidiana na mkongwe Abdallah Seif ‘King Kibadeni’ ambaye naye kwa sasa ameamua kufanya mambo mengine katika kituo chake cha michezo kilichopo Chamazi Dar es Salaam.
Wachezaji wengi ambao wamepita mikononi mwake wanaujua na kuutambua ukali wake ambao una tija kwao kutokana na umuhimu wa kazi yao.
“Julio baba yangu yule yaani mkiwa mazoezini ukazingua unalo, siunajua sisi wachezaji kuna katabia ka kutegea katika baadhi ya mazoezi sasa akikubahatisha umefanya hivyo unapewa na adhabu kabisa, ikiwemo kuzunguka uwanja mpaka atakapoamua yeye kukurejesha kwa wenzako,”anabainisha mchezaji huyo.
Anasema, baada ya mazoezi ni mtu mmoja pisi sana ambaye anasikiliza na ana huruma kwa kila mtu bila ya kujali ulimkosea muda mchache uliopita.
“Sisi wachezaji tunakuwa na tabia fulan hivi za kuzingua tunajisahau kuwa mpira ndiyo kazi yetu inayotufanya tuendeshe familia zetu, kama mwalimu ni mchizi tu anakuangalia hapo lazima mambo yashindwe kwenda,”anaongeza.
Julio yeye anaamini bila ya kuwa mkali kwa wachezaji wa Kibongo ni ngumu kutoboa kutokana na namnba ambavyo wanaridhika mapema sana.
FRED FELIX ‘MINZIRO’ (TANZANIA PRISONS)
Katika makocha bora wazawa hapa nchini jina la mwamba huyu haliwezi kukosa kutokana na ubora wake na uwezo mkubwa aliokuwa nao katika ufundishaji.
Amekuwa kocha mwenye cv ya kipekee kuzipandisha timu mbalimbali kutoka Championship kwenda Ligi Kuu na baada ya kufanikiwa klabu hizo humuacha na kutafuta mbadala wake.
Minziro amezipandisha Geita Gold, KMC, Singida ambazo kwa sasa zina mafanikio makubwa katika ligi na zinatoa ushindani mkali.
Minziro anaonekana mpole na mkarimu sana nje ya uwanja lakini hana masihara awapo katika majukumu yake ya kazi na hakuna mchezaji ambaye analeta ndivyo sivyo wakati wa kazi.
“Utadhani tuko na mwalimu mwanajeshi kumbe raia tu, aisee hataki mchezo ni mkali hasa nje ya majukumu ya kazi ni mtu freshi sana, hata sisi mwanzoni tulipata shida kumuelewa lakini sasa hivi mambo freshi tu tunaenda naye sawa,” anasema mmoja wa wachezaji ndani ya kikosi chake cha Tanzania Prisons.
Mchezaji wake Geita Gold jina tunalihifadhi alisema, kocha huyo akikasirika utadhani anamwaga machozi kumbe hasira tu.
“Muda mwingine hata sisi tulikuwa tunaona aibu kumkwaza maana mtu mzima yule akiangusha chozi kwa ajili yako sio poa hata kidogo japokuwa tunazingua sana wachezaji na yeye hapendi kuzinguliwa ni mkali sana yule baba lakini mpaka umkwaze,” alisema mchezaji huyo.
Minziro hivi karibuni kwa hasira baada ya mchezo dhidi ya Simba waliokubali kichapo cha mabao 3-1 aliongea kwa hasira kuhusu viwango vya mastaa wake ndipo unapogundua ukweli wa wachezaji wanachokisema.
Baada ya mchezo alisema inahitaji kuvumilia sana kuwafundisha wachezaji wa hapa nchini kwa kuwa makosa ni yaleyale yanajirudia kila siku.
“Shida ya wachezaji wetu hawako smati vichwani hilo ni tatizo kubwa sana, unafanya mazoezi ya kuongea kila siku lakini mambo yanajirudia unakuwa mkali hawakuelewi hata kidogo ni kazi sana,”anasema Minziro ambaye amewahi kuwa kocha na mchezaji wa zamani wa Yanga.