Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha hawa Ligi Kuu Bara matumbo joto

Juma Mwambusi 1 Juma Mwambusi

Wed, 7 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Ligi Kuu ikimalizia mzunguko wa kwanza na kila timu ikivuna ilichopanda, baadhi ya makocha wapo katika presha kubwa katika kulinda vibarua vyao wakisubiri raundi ya pili kujua hatma zao.

Hadi sasa hakuna timu ambayo haijaonja kipigo tofauti na msimu uliopita baada ya Yanga kumaliza ligi bila kupoteza mchezo, huku ikitwaa ubingwa wa michuano hiyo na ile ya Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).

Hata hivyo, bingwa huyo mtetezi na watani zao, Simba, ndiyo timu pekee zilizopoteza mchezo mmoja na kuwa katika nafasi tatu za juu, huku Ihefu na Ruvu Shooting na Tanzania Prisons zikipoteza idadi kubwa ya mechi (10) na kukaa mkiani.

Makala haya yanakupa orodha ya baadhi ya makocha ambao ‘Moja haikai wala mbili haikai’, wakinywa maji hayashuki kutokana na presha walizonazo kufuatia matokeo yasiyoridhisha na kuwa katika hali ngumu ya kutemeshwa vibarua.

Mwinyi Zahera -Polisi Tanzania

Baada ya kumtema kocha mkuu wa timu hiyo, Josillin Bipfubusa raia wa Burundi, Polisi Tanzania imemtangaza Mwinyi Zahera kuchukua mikoba yake.

Pamoja na Zahera kuwa na uzoefu wa Ligi Kuu Tanzania akidumu kwa zaidi ya misimu miwili akiwa na Yanga, lakini kocha huyo raia wa Congo ana kazi ngumu kuhakikisha timu hiyo inabaki kwenye ligi.

Hadi sasa Maafande hao ndiyo wanaburuza mkia wakiwa na pointi nane na rasmi Zahera ataanza kazi katika mzunguko wa pili akipambana kuirejesha kwenye ramani timu hiyo.

Mtihani wa kocha huyo mwenye maneno mengi, huenda akajikuta akitema kibarua chake pale atakaposhindwa kuifikisha kwenye malengo wanayohitaji mabosi zake.

Boniface Mkwasa - Ruvu Shooting

Tayari kocha huyu mwenye sifa na rekodi za kutosha kwenye soka nchini ameshamwaga manyanga kuifundisha Ruvu Shooting tangu jana. Mkwasa mchezaji wa zamani wa Yanga alikuwa anapitia magumu sana akiwa na Ruvu Shooting kutokana na matokeo aliyomaliza nayo mzunguko wa kwanza. Ni wazi Mkwasa aliyewahi kuwa kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Yanga na Prisons hakuwa na furaha Ruvu Shooting sehemu ilipokuwepo ni dhahiri alipatwa na mchecheto katika kuiokoa ili isishuke daraja.

Laiti kocha huyo msomi kama asingesoma alama za nyakati angetimuliwa kwenye michezo ijayo. Ameiacha Ruvu ikishika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 11 baada ya kushinda michezo mitatu tu kati ya 15 iliyocheza hadi sasa.

Juma Mwambusi– Ihefu

Pamoja na uzoefu wake kwenye Ligi Kuu lakini moja haikai, mbili haishikiki kwa kocha huyo aliyewahi kuzinoa Mbeya City na Yanga kwa nyakati tofauti kutokana na hali ilivyo kwa chama lake la Ihefu kwa sasa.

Pamoja na rekodi nzuri aliyoweka Mwambusi kuwa kocha wa kwanza kuifunga Yanga mabao 2-1 na kuitibulia rekodi ya mechi 49 za bingwa huyo mtetezi lakini hana furaha kutokana na mwenendo wa timu hiyo kwenye ligi kuu.

Kocha huyo ambaye amekabidhiwa majukumu hivi karibuni kusaidiana na Kocha Zuberi Katwila, matokeo ya Ihefu hayajampa raha kutokana kuwa nafasi tatu za chini na lolote linaweza kumtokea dhidi ya mabosi wake.

Patrick Odhiambo – Tanzania Prisons

Usimuone mkimya, kocha huyo raia wa Kenya anapitia kipindi kigumu kutokana na matokeo ya timu yake yalivyo na tayari amewashiwa taa nyekundu kuhusu mwenendo wa Tanzania Prisons kutoridhisha.

Odhiambo aliyetamburishwa Ligi Kuu na Biashara United misimu miwili iliyopita, alikabidhiwa kikosi cha Wajelajela msimu uliopita na kufanikiwa kuinusuru kushuka daraja dakika za mwisho alipoishia ‘play off’.

Odhiambo kwa sasa anasubiri muda tu kwani msimamo wa mabosi wake ulikuwa ni kwenye mechi mbili za kumaliza raundi ya kwanza dhidi ya KMC iliyoisha kwa suluhu na Yanga.

Yusuph Chipo – Coastal Union

Pamoja na soka safi la vijana wake lakini bado ishu ya matokeo si nzuri sana na kocha huyo Mkenya anaweza kukumbana na kitu kizito kutoka kwa mabosi wake kama hatashtuka mapema.

Katika mechi takribani sita za nyuma Coastal Union haijapata ushindi, akipoteza tano na sare moja hali inayokiweka hatarini kibarua chake na amebakiza michezo miwili kumaliza raundi ya kwanza.

Katika mechi hizo sita imetoa sare na Mbeya City 2-2, ikapoteza kwa Mtibwa Sugar 2-1 sawa na kwa Ihefu, akala 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, 3-2 dhidi ya Azam, kisha 3-0 mbele ya Simba.

Wengine ambao matokeo yao ni ya kusuasua ni kocha mkuu wa Namungo, Hanoor Janza ambaye timu hiyo haijawa na mwendelezo mzuri ikiwa nafasi ya tisa na pointi 18.

Yumo pia kocha asiye na maneno mengi, Hitimana Thiery raia wa Rwanda anayekinoa kikosi cha KMC ambapo matokeo ya sare mfululizo anapaswa kubadili gia ili kulinda kibarua chake.

Melis Medo wa Dodoma Jiji naye hajawa salama sana kutokana na kuanza kwa kusuasua kabla ya kuamka kwenye mechi mbili za mwisho akishinda dhidi ya Coastal Union 1-0 kisha 2-1 na Ruvu Shooting na kuiondoka timu hiyo nafasi tatu za mkiani.

Katika mzunguko wa pili atapaswa kukaza kamba kuhakikisha ushindi huo unaendelea ili timu hiyo ibaki kwenye ligi msimu ujao vinginevyo hatavumiliwa.

Wenyewe hawa hapa:

Mwambusi anasema baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza kwa matokeo hayo, anaenda kusahihisha makosa akisaidiana na benchi lake la ufundi ili raundi ya pili timu ibadilike.

Anasema hatua ya kwanza ni kuangalia sehemu gani ya kuboresha wakati wakielekea kwenye dirisha dogo la usajili ambapo wapo watakaotemwa, na wengine kutolewa kwa mkopo.

“Tunasubiri kikao cha pamoja kujadili namna ya kusuka upya timu kwa ajili ya mzunguko wa pili, lazima tuangalie nani anaondoka au kubaki lakini tukiangalia wa kupeleka kwa mkopo,” anasema Mwambusi.

Naye Chipo anayeinoa Costal Union anasema bado hajataka tamaa na ana matumaini na matarajio makubwa na vijana wake kuweza kubadili matokeo na kumaliza salama ligi.

“Ni kweli hali siyo nzuri lakini ndiyo mpira tumepoteza mechi na zipo tulizoshinda, kimsingi tunaendelea kupambana kuhakikisha tunafanya vizuri katika zile zinazofuata,” anasema Chipo.

Chanzo: Mwanaspoti