Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha Euro 2024 pochi zao ni tamu!

Makocha Euroooo Makocha Euro 2024 pochi zao ni tamu!

Tue, 18 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Utamu wa mikikimikiki ya Euro 2024 unazidi kunoga.Mambo ni moto, vuta nikuvute kuanzia kwa mashabiki, mastaa ndani ya uwanja hadi kwa makocha kwenye mabenchi ya ufundi.

Kila taifa lililopo kwenye fainali hizo linajaribu kupambana kuhakikisha linafanya kweli na kunyakua ubingwa.

Lakini, wanasema pesa ndiyo sabuni ya roho. Ushawahi kujiuliza, makocha wa timu za taifa zilizopo kwenye michuano hiyo ya Euro 2024, wanalipwa mishahara kiasi gani? Ni kocha gani anayelipwa mkwanja mrefu kuzidi wengine?

Kwa taarifa tu, kocha anayelipwa mshahara mkubwa kwenye Euro 2024, kama angekuwa Ligi Kuu England, basi angeshika nafasi za chini huko kwenye orodha ya makocha wanaolipwa kibosi kwenye ligi hiyo.

Jarida la Football Finance limeweka bayana mishahara ya makocha wote 24 walio na timu za huko kwenye Euro 2024. Na kwenye mkeka huo, kocha wa England, Gareth Southgate, ndiye anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwa waliopo Euro 2024, akilipwa mara 29 zaidi ya pesa anayochukua kila mwaka kocha Willy Sagnol, ambaye ni kocha wa timu ya taifa ya Georgia.

Makocha kama Roberto Martinez na Julian Nagelsmann wanahitaji kulipwa mishahara mikubwa wa sababu wanafanya kazi ya kuzinoa timu kubwa kama za Ureno na Ujerumani.

Lakini, mishahara mikubwa wanayolipwa makocha hao inakwenda sambamba na presha zinazowakabili katika kuhakikisha mataifa yao yanafanya vizuri kwenye fainali hizo. Kinyume cha hilo, basi mwisho wa michuano hiyo ya Euro 2024 basi chochote kinaweza kutokea kwenye hatima za vibarua vyao. Kwenye orodha hiyo, kocha wa Georgia, ndiye anayelipwa mshahara mdogo zaidi kuzidi wote, huku timu yake pia haina presha kubwa ya matokeo kwenye mikikimikiki hiyo, hata wakikomea kwenye hatua ya makundi, hilo haliwezi kuwa shida kubwa kwao.

Nchi kama za Ujerumani, Ufaransa, Hispania, Italia, Uholanzi, England, Uswisi, Ubelgiji na Ureno zimekuwa na matarajio ya kufanya makubwa zaidi kwenye fainali hizo za Euro 2024 huku hilo likienda sambamba na mishahara wanayolipwa makocha wao.

ORODHA YA MISHAHARA YA MAKOCHA WA EURO 2024 WANAYOLIPWA KWA MWAKA

1. Gareth Southgate (England, Pauni 4.9 milioni)

2. Julian Nagelsmann (Ujerumani, Pauni 4 milioni)

3. Roberto Martinez (Ureno, Pauni 3.4 milioni)

4. Didier Deschamps (Ufaransa, Pauni 3.2 milioni)

5. Ronald Koeman (Uholanzi, Pauni 2.5 milioni)

6. Luciano Spalletti (Italia, Pauni 2.5 milioni)

7. Vicenzo Montella (Uturuki, Pauni 1.5 milioni)

8. Murat Yakin (Uswisi, Pauni 1.4 milioni)

9. Ralf Rangnick (Austria, Pauni 1.3 milioni)

10. Domenico Tedesco (Ubelgiji, Pauni 1.3 milioni)

11. Zlatko Dalic (Croatia, Pauni 1.3 milioni)

12. Dragan Stojkovic (Serbia, Pauni 1.2 milioni)

13. Luis de la Fuente (Hispania, Pauni 1 milioni)

14. Serhiy Rebrov (Ukraine, Pauni 1 milioni)

15. Kasper Hjulmand (Denmark, Pauni 970,000)

16. Sylvinho (Albania, Pauni 632,000)

17. Michal Probierz (Poland, Pauni 472,000)

18. Steve Clark (Scotland, Pauni 464,000)

19. Francesco Calzona (Slovakia, Pauni 455,000)

20. Marco Rossi (Hungary, Pauni 253,000)

21. Matjaz Kek (Slovenia, Pauni 253,000)

22. Ivan Hasek (Czech Republic, Pauni 210,000)

23. Edward Iordanescu (Romania, Pauni 202,000)

24. Willy Sagnol (Georgia, Pauni 168,000)

Chanzo: Mwanaspoti