Ligi Kuu Bara kwa sasa ni moja ya ligi bora Afrika. Inakamata nafasi ya tano. Hii inaonyesha kuna mabadiliko makubwa tofauti na huko nyuma.
Tanzania ni moja ya nchi zinazoingiza timu nne kwenye michuano ya Shrikisho la Soka Afrika (Caf). Simba, Yanga, Singida Fountain Gate na Azam FC. Hata hivyo, mbili tu ndio zimesalia kwenye michuano hiyo Simba na Yanga (Ligi ya Mabingwa Afrika).
Pamoja na ubora wa ligi, kuna tatizo kwa timu nyingi hasa uzalishaji wa vipaji vipya. Hii inasababisha baadhi ya timu kulazimika kuleta wachezaji wenye majina. Ni wazawa wachache sana wenye majina makubwa, wengi ni wageni.
Tatizo hili si kwa wachezaji wa ndani pekee, hata kwa makipa lipo. Makipa wazawa ni wachache kwenye Ligi Kuu Bara. Ni wachache wanaofanya vizuri. Hili ni tatizo kubwa na linatoa ugumu kwenye uchaguzi wa makipa wa timu za taifa.
HAWA NDIO VINARA
Msimu huu kwenye msimamo wa makipa bora, wazawa ni wawili kati ya sita kwa mtazamo wa ‘Cleen sheet’ zao hadi sasa.
Kipa Mcongo wa Coastal Union, Leny Matampi ndiye kinara. Kwenye michezo 14, sita kati ya hiyo hajaruhusu nyavu bao. Wa pili ni Yona Amosi wa Tanzania Prisons ambaye ni mzawa. Michezo 14, sita hajaruhusu bao licha ya timu yake kwenye msimamo haipo kwenye nafasi nzuri.
Djigui Diarra wa Yanga ni wa tatu. Raia huyu wa Mali, kwenye mechi 11, tano tu hajaruhusu bao, ikiwa ni nusu ya mechi ilizocheza Yanga.
Costantine Malimi wa Geita Gold ni wa nne. Kwenye michezo 14, hajaruhusu bao michezo mitano sawa na John Noble, Mnigeria anayeichezea Tabora United. Jonathan Nahimana, kipa raia wa Burundi anayeidakia Namungo FC ya Ruangwa, ndiye pekee aliyecheza michezo minne na yote hajaruhusu bao.
Kwenye orodha hiyo, wazawa ni wawili msimu huu. Hii ni tofauti na kipindi cha nyuma na asilimia kubwa ya makipa walikuwa wazawa. Ni anguko kubwa linaloibua maswali na tafakari ya nafasi ya makipa wazawa ligi kuu misimu ijayo.
SIMBA, YANGA, AZAM ZAONGOZA KWA WAGENI
Miaka ya nyuma miamba hii ya soka golini waliwaamini zaidi makipa wazawa. Kwa Simba ilikuwa kama utamaduni, golini ataanza mzawa na walikuwa bora.
Makipa bora wazawa waliopita simba ni kama Mohammed Mwameja, Steven Nemes, Iddi Pazi, Kelvin Mhagama, Juma Kaseja na wengine akiwamo Aishi Manuala ambaye ameonyesha kiwango bora kipindi chote akiwa na Wekundu wa Msimbazi.
Hata hivyo, baada ya Manula kuumia, ilikuwa ni fursa kwa makipa wengine na Simba ilisaka makipa kutoka nje akiwamo Jefferson Luis Szerban de Oliveira Junior, ambaye wakiwa kambini Uturuki aliumia hivyo hakupata nafasi ya kuichezea timu hiyo.
Simba ikarejea kwa Hussein Abel ambaye ni mzawa, hata hivyo, ilionekana hawezi kuendana na mikikimikiki ya timu hiyo, ikaamua kumchukuaAyoub Lakred raia wa Morocco. Ni anguko la wazawa. Simba ni wazi imeshindwa kuendeleza utamaduni wake wa miaka mingi. Tatizo ni kukosekana kwa makipa bora wazawa. Lisemwalo, kama itahitaji msaidizi wa Ayoub, bado itakimbilia nje ya nchi ingawa wazawa wapo.
Kwa upande wa Yanga, kipa wao tegemeo ni Diarra. Ndiye anayeaminiwa zaidi golini. Amewaacha mbali Metacha Mnata na Aboutwalib Mshery ambao ni wazawa. Hii inaonyesha kama Yanga itahitaji kipa mbadala wa Diarra itakwenda tena nje.
Azam ndiyo balaa. Makipa watatu wote wanatoka nje, ingawa hakuna picha halisi ya nani namba moja.
Hata hivyo, makipa Abdulai Iddrisu raia wa Ghana na Ali Ahamada raia wa Comoro wamekuwa wakipata nafasi mara kwa mara na kuonyesha kocha anawaamini wote wawili.
Timu hiyo pia imemwongeza Mohamed Mustafa raia wa Sudan baada ya Idrissu na Ahamada kuumia, nafasi hii ingefaa kwa mzawa kutokana na hali ya kiuchumi na nafasi za wageni kuwa chache kuliko za wazawa. Ni wazi kungekuwa na makipa bora wazawa Azam ingemchukua akawanie namba na Zuber Foba ambaye amefanya vizuri kwenye Michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Picha halisi inaonyesha makipa wote wageni timu zao zipo 10 bora kwenye msimamo wa ligi, Namungo ipo nafasi ya nane, Coastal ya sita, Simba, Yanga na Azam zipo kwenye tatu bora kileleni. Ni Tabora United tu yenye kipa mgeni na iko nje ya 10 bora. Hii inaonyesha makipa wageni wana msaada mkubwa kwa timu hizo.
STARS MAMBO MAGUMU
Hapa maswali ni mengi. Makipa walioitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars sio wote wanaoanza kwenye timu zao kwenye Ligi Kuu.
Makipa, Manula, Beno Kakolanya ndio walioko Stars kwa sasa baada ya Metacha Mnata kuachwa kwenye kikosi kilichokwenda Ivory Coast wa ajili ya Afcon.
Hata hivyo, mbali na wazawa hao,. kipa Kwesi Kawawa anayecheza soka nje ya nchi, ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kuanza golini.
Wazawa wawili, Manula amecheza mechi moja tu ya Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Yanga na Simba ilipoteza kwa mabao 5-1. Uwepo wake Stars umeibua maswali. Hata hivyo, kuitwa kwake inaonekana ni kutokana na kutokuwa na makipa wengi wenye uzoefu nchini na si ubora, kwani ingeangaliwa ubora, kuna Yona Amosi wa Tanzania Prisons. Alistahili kuwemo kwenye kikosi hicho.
Kakolanya hakutumika kwenye mechi nne za mwisho za Singida FG. Sababu haijatolewa. Yuko Ivory Coast na Stars. Ni wazi kwa makipa wa ligi kuu kuna anguko kubwa, ndiyo maana hatutashangaa Kawawa akaanza golini kwenye mechi za Afcon.
TATIZO NI HILI
Taaluma ya ukocha wa makipa imeonekana ndio tatizo. Ni wazi kama hakuna makocha bora wa makipa, tatizo la makipa halitaisha. Baadhi ya makipa wanaomaliza kucheza soka hawafikirii kuendelea na taaluma ya ukocha wa makipa bali wanatamani kuwa makocha wakuu. Hii inaua taaluma ya ukocha wa makipa hivyo ni ngumu kupata makipa wazuri.
Kocha wa makipa Simba, Dani Cadena, wasifu wake unaonekana alisomea ukocha wa makipa na baada ya hapo akachukua leseni A ya Uefa ya ukocha, hivyo anaonekana anafanya kazi yake ipasavyo.
Baadhi ya timu makocha wa makipa ni wa kuongea tu idadi. Ni kazi ambayo inaonekana kila mtu/kocha anaiweza. Hii inachangia kupoteza makipa wengi.
Mfano kipa wa zamani wa Taifa Stars, Simba, Yanga na KMC, Kaseja kabla ya kusomea leseni A ya Caf, alionekana kuwa kocha bora wa makipa lakini alienda chuoni na kusomea ukocha wa jumla badala ya ukocha wa makipa, eneo lake alilolizoea, ingawa kwa sasa ndiye kocha wa makipa wa Kagera Sugar. Ni kama wengi wanaidharau kozi ya ukocha wa makipa na kusababisha uwepo wa makocha wachache kwenye fani hiyo, jambo linalochangia pia kukosekana kwa makocha bora wazawa kwenye ligi kuu na baadhi ya timu kuajiri makocha kutoka nje.