Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makipa wa boli wamechoma nyumba!

Dfgb Diarra Makipa wa boli wamechoma nyumba!

Thu, 5 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Soka la kisasa linahitaji sana makipa wanaojua kutumia vyema miguu kusambaza pasi za upendo, sambamba na kuokoa hatari kwa kutumia mikono, lakini siku ya jana la leo haikuwa njema kwa makipa wa boli Djigui Diarra wa Yanga, Andre Onana wa Man United na David Raya wa Arsenal, ambao wote walishuhudia timu zao zikipasuka kiulaini tu.

Katika mechi ya Ligi Kuu Bara, Yanga imekumbana na kipigo cha pili mfululizo cha 2-1 kwenye Uwanja wa Higland Estate, Ubaruku kule Mbarali dhidi ya Ihefu huko bao la kwanza wenyeji likitokana na makosa ya kipa, Djigui Diarra, ambaye alipiga pasi fupi kwa beki wake Bakari Mwamnyeto, ikaibwa na mchezaji wa Ihefu, beki huyo wa Yanga akacheza faulo. Never Tigere akapiga frii-kiki ya moja kwa moja langoni, Diarra akaichemka tena kwa kuipangulia ndani Lenny Kisu akauweka mpira kambani likawa bao la kusawazisha dk40.

Hapo Ihefu walizinduka kutoka kutanguliwa kwa bao la mapema dakika ya 4 tu lililofungwa na Pacome Zouzua akimalizia krosi ya Clement Mzize.

Ihefu wakakaza ile mbaya na dakika ya 66 wakaweka bao la pili kwa kaunta lililowekwa kambani kiufundi kabisa na Charles Ilanfya na kurudia ushindi kama ule ilioupata msimu uliopita ambao ulichangiwa na frii-kiki tena ya yule yule Tigere aliyeiweka kambani moja kwa moja na bao jingine lililotokana na kona iliyochongwa na Tigere huyo huyo.

Mbaya zaidi kipigo cha msimu uliopita kilihitimisha mwendo wa kihistoria wa Yanga kucheza mechi 49 bila ya kupoteza na msimu huu kimemkaribisha kocha mpya Gamondi kwamba Ubaruku sio mahala pazuri kwa Wanajangwani.

Na kule Ulaya, kipa wa Man United, Onana ambaye anasifika kwa kupiga pasi, jana alipiga pasi mkaa ikamsababishia kadi nyekundu kiungo wake Casemiro aliyekuwa akijaribu kuzuia wasifungwe, ikawa penalti lakini mauro Icardi wa Galatasaray akakosa tuta hilo. Hata hivyo dakika chache baadaye, Icardi akawaweka United na kuchangia kipigo cha 3-2 cha Mashetani Wekundu.

Yule Haaland wa United yaani Rasmus Hojland, alipiga mbili lakini hazikusaidia kitu. United ikapasuka mechi ya pili mfululizo tangu irudi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na sasa kikosi cha Ten Hag kinashika mkia katika msimamo wa Kundi A.

Pia, kipa mwingine aliyechoma ni David Raya wa Arsenal. Katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Lens, alipiga pasi fupi ikaibwa, wakawekwa. Gunners wakafa 2-1.

Raya ndiyo huyu huyu anayesifika kwa kupiga pasi matata za miguu, ambaye uwezo wake wa kutumia miguu kuanzisha mashanmbulizi ndio uliomfanya amng'oe kipa aliyekuwa namba 1 wa timu hiyo, Muingereza Aaron Ramsdale.

Chanzo: Mwanaspoti