Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makipa janga timu ya taifa

Makipa Stars Makipa janga timu ya taifa

Thu, 20 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Simba, Yanga na Azam, ni timu ambazo zimekuwa zikitawala soka la Tanzania kwa muda mrefu. Kuanzia mwaka 2008 ambapo Azam FC ilianza kushiriki Ligi Kuu Bara, timu hizi tatu pekee ndizo zimefanikiwa kubeba ubingwa wa ligi hiyo.

Katika kipindi hicho cha misimu 16, Azam imebeba mara moja 2013-2014, huku misimu 15 wakigawana Simba na Yanga. Yanga wamechukua makombe tisa na Simba wamebeba sita.

Mbali na kubeba ubingwa, pia timu hizo tatu kwa muda mrefu zimekuwa zikipishana nafasi tatu za juu katika msimamo wa Ligi Kuu. Msimu uliopita wa 2023-2024 Yanga ilikuwa mabingwa, Azam ya pili na Simba ikishika nafasi ya tatu. Coastal Union iliishia nafasi ya nne.

Katika vikosi vya timu zote hizo nne ambazo msimu ujao wa 2024-2025 zitashiriki michuano ya kimataifa ikiiwakilisha Tanzania, kuna makipa wa kigeni wanaoanza kikosi cha kwanza. Djigui Diarra (Yanga), Mustafa Mohamed (Azam), Ayoub Lakred (Simba) na Ley Matampi (Coastal Union). Hiyo inatoa picha kwamba makipa wazawa wamezidiwa na wageni jambo ambalo linawafanya kuamka hivi sasa ili iwe faida kwao na taifa kwa ujumla linapokuja suala la timu ya Taifa.

Mchezo uliopita wa Taifa Stars ambao ilishinda ugenini bao 1-0 dhidi ya Zambia ukiwa ni wa kufuzu Kombe la Dunia 2026, Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Suleimani Morocco na msaidizi wake, Juma Mgunda walikwenda na makipa ambao ni chaguo la pili na tatu ndani ya klabu zao.

Ally Salim, ambaye alidaka mechi hiyo, ni kipa chaguo la tatu ndani ya Simba baada ya mzawa Aishi Manula na Ayoub Lakred raia wa Morocco, wakati Aboutwalib Mshery aliyekuwa benchi naye ni chaguo la pili pale Yanga nyuma ya Djigui Diarra raia wa Mali. Lakred hachezi Timu ya Taifa ya Morocco, lakini Diarra ni kipa namba moja wa Mali.

Rekodi zinaonyesha kwamba, katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara 2023-2024, Ally Salim alicheza mechi 6 sawa na dakika 540 akiwa na kikosi cha Simba, akaruhusu mabao 6 wastani wa bao moja kila mchezo akiambulia clean sheet 1 pekee. Kwa upande wa Aboutwalib Mshery, alicheza mechi 6 katika kikosi cha Yanga kwa dakika 438, akaruhusu mabao 3 wastani wa 0.5 ya mabao kwa mchezo na kukusanya clean sheet 3.

Takwimu hizo zinadhihirisha wazi kwamba makipa hao wamepata nafasi ndogo ya kucheza kwenye vikosi vyao kwani katika mechi 30 za msimu mzima, hawajatumika hata robo yake huku wageni wakitawala.

Azam FC, kipa wao aliyemaliza msimu akiwa amefanya kazi kubwa ni Mustafa Mohamed raia wa Sudan, lakini awali alikuwepo Ali Ahamada raia wa Comoro ambaye kwa sasa ni majeruhi kama ilivyo kwa Mghana, Abdulai Iddrisu. Kipa mzawa ambaye mara mojamoja anapewa nafasi ni chipukizi Zuberi Foba.

Upande wa Azam wana makipa watatu wa kimataifa, hata walipoumia hao wawili, bado waliamini nje ya nchi ndiyo kuna kipa bora.

Imekuwa kama utamaduni wa makocha wa Taifa Stars kuwakumbatia makipa wanaocheza Simba na Yanga kwenye vikosi vyao hivyo wazawa wanaocheza timu hizo wanaacha maswali ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi.

Hivi karibuni katika kikosi cha Taifa Stars alitambulishwa kipa Kwesi Kawawa anayecheza soka nchini Sweden katika timu ya Syrianska FC ambapo alidaka mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Morocco na Stars kupoteza nyumbani kwa mabao 2-0 hakupata nafasi tena kwenye mechi nyingi za Stars zilizofuata.

Kinachoonekana katika hili ni kwamba, licha ya kwamba Tanzania ina makipa wengi wazuri, lakini wanapofika katika timu hizi kubwa wanashindwa kuwa na mwendelezo mzuri.

Metacha Mnata, alifanya vizuri akiwa na kikosi cha Mbao FC, Polisi Tanzania na Singida Big Stars, lakini kila alipoenda Yanga alishindwa kupambania nafasi ya kwanza. Hiyo imemtokea Mshery aliyetamba pale Mtibwa Sugar lakini ndani ya Yanga, anasubiri mbele ya Diarra.

Kutotoa ushindani kwa makipa wazawa wanapokwenda Simba na Yanga, limewafanya viongozi wa timu hizo kuamua kubadilisha utamaduni wa kusajili makipa wazawa na kuwapa nafasi ya wageni ambao pia wana uzoefu wa michuano ya kimataifa.

Awali timu hizo zilikuwa zikisajili makipa wazawa jambo lililofanya wageni wasifikiriwe sana na hata wanaposajiliwa walikuwa wanakalishwa benchi.

Juma Kaseja aliwahi kuwika na Simba kuanzia 2003 hadi 2014 ambapo timu hiyo ilikuwa haifikirii kwenda nje ya nchi kusajili kipa mwingine wakiamini golini kwao kupo salama kutokana na uwepo wake. Hata alipokwenda Yanga msimu wa 2014–2015, pia alikuwa akidaka sambamba na mzawa mwenzie Ally Mustapha ‘Barthez’.

Mambo yalianza kubadilika Simba ilipoamua kuwa na makipa wawili wote wa kigeni, msimu wa 2016-2017, ambao ni Daniel Agyei raia wa Ghana na Vicent Angban kutoka Ivory Coast ambapo ujio wa Aishi Manula kutoka Azam 2017 ukairudisha kwenye utamaduni wao licha ya kwamba hivi sasa wanawika wakiwa na Ayoub Lakred.

Kwa muda mrefu, Aishi Manula amekuwa akikaa langoni katika kikosi cha Taifa Stars, timu hiyo ilipokwenda Afcon 2019 alikuwepo yeye akisaidiana na Metacha Mnata na Aaron Kalambo kisha Afcon 2023 alijumuishwa sambamba na Kwesi Kawawa na Beno Kakolanya lakini majeraha aliyoyapata siku za karibuni, majeraha yamemweka nje.

Kila kocha anayekuja kuinoa Taifa Stars, amekuwa akiumiza kichwa juu ya kipa wa kumtumia, hiyo ni tangu kuumia kwa Manula. Wametumika makipa tofautitofauti kwa kipindi cha muda mfupi.

NINI KIFANYIKE

Kutokana na hali hiyo, wadau mbalimbali wametoa maoni yao wakiwemo makocha na makipa wa zamani ambao wamepita Simba na Yanga.

Kipa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Ivo Mapunda ambaye kwa sasa yupo kwenye Benchi la Ufundi la Biashara United inayoshiriki Ligi ya Championship, amesema katika klabu kongwe za Simba na Yanga ambazo ndizo huwa zinatoa wachezaji wengi wanaounda timu ya taifa wakiwemo makipa, anashauri kuwepo na mifumo ya kutosajili makipa wa kigeni ili kuwapa nafasi wazawa ambao watalibeba taifa.

“Binafsi naona makipa wazawa wana uwezo kuliko wageni, shida hawapati nafasi ndani ya klabu zao, mfano mzuri nimeona alivyodaka Ally Salim dhidi ya Zambia, kafanya vizuri lakini hapewi nafasi katika klabu yake,” alisema na kuongeza;

“Ukiangalia mimi, Juma Kaseja, Shaban Kado kipindi chetu tulikuwa tunapewa nafasi ndio maana tulikuwa na viwango vikubwa, pia hizo klabu za Simba na Yanga kama tulizifanyia makubwa zingetupa nafasi za kuwanoa makipa ili tuwajenge katika misingi imara, changamoto inakuja hawathamini vya nyumbani.”

Kwa upande wa aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba na kipa wa timu hiyo, Iddy Pazi, alisema: “Simba ndiyo ilikuwa na utaratibu wa kusajili makipa wazawa pekee ndio maana walikuwa wanatoa Tanzania One. Leo hii anakosekana Aishi Manula unaona pengo lipo, naona jina la Tanzania One anaondoka nalo Aishi, maana sifa zake anakuwa namba moja katika timu yake na timu ya taifa.

“Klabu zinataka ziwafurahishe mashabiki, lakini nafasi ya makipa katika klabu hizo ziwe za wazawa, maana tuna makipa wazuri, mfano akijengwa Ally Salim na Aboutwalib Mshery watalisaidia sana taifa, vinginevyo kuwepo na mifumo ndani ya klabu hizo za kupewa nafasi wazawa kuliko wageni.”

Kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars ambaye kwa sasa ni kocha wa makipa, Juma Pondamali, ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuondoa nafasi ya kusajili makipa wa kigeni ili kujenga wigo mpana eneo hilo kwa wachezaji wa ndani.

Pondamali amesema hawawezi kupata kipa bora mzawa kama timu kubwa zenye ushawishi na uwakilishi wa michuano ya kimataifa Simba, Yanga, Azam FC na Coastal Union zitaendelea kuwa na makipa wa kigeni.

“Timu kubwa zimekuwa na uwezo mkubwa wa kusajili mchezaji wanayemtaka hivyo ni rahisi kwao kuwa na makipa bora kulingana na kujenga ukuta imara kuanzia mabeki hadi mlinda lango, huwezi kufananisha kipa wa timu nyingine ambazo zina mabeki wa kawaida na Simba au Coastal Union ambao wana ukuta imara na kipa bora,” alisema na kuongeza;

“Ili kutengeneza makipa bora na watakaotubeba kwenye michuano mikubwa ushauri wangu ni kuondoa nafasi ya kusajili makipa wa kigeni ili kutengeneza wazawa ambao watakuwa bora.”

Pondamali alitolea mfano mechi ya kufuzu Kombe la Dunia ambapo Taifa Stars walipocheza na Zambia, timu iliongozwa na kipa ambaye kwenye timu yake anakaa benchi na walifanikiwa.

Chanzo: Mwanaspoti