Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makatta anaitaka Tanzania Prisons hii!

Makata Pic Data Mbwana Makatta

Sun, 21 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kambi inayoendelea nayo Tanzania Prisons huko jijini Dar es Salaam, imeonekana kumkuna Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbwana Makatta akitambia ubora wa nyota wa kikosi hicho akisema ndicho anachokitaka na Agosti 16 Ligi Kuu Bara itakapoanza kitaeleweka.

Prisons yenye makazi yake Ruanda jijini Mbeya, imeweka kambi Jijini Dar es Salaam hadi Agosti 1 kujiwinda na Ligi Kuu itakayoanza kurindima Agosti 16, huku ikiwa na matumaini makubwa.

Makatta anayeinoa timu hiyo kwa mara ya tatu katika historia, huku akiwa na rekodi nzuri, mashabiki na wadau wa soka jijini Mbeya wanasubiri kuona iwapo ataipa tena mafanikio kama alivyowahi kufanya huko nyuma.

Kocha huyo mwenye historia ya kuzipandisha timu kadhaa Ligi Kuu, tayari ameshaanza majukumu yake kuwaongoza Maafande hao huku akieleza kikosi chake kuwa bora na kitasumbua Ligi ikianza.

Makatta aliliambia Mwanaspoti,a kambi waliyonayo Dar es Salaam inampa nguvu na kutamba kufanya vizuri akieleza kuwa hata usajili waliofanya nyota wote wanaonesha uwezo na utimamu.

“Tunaendelea vyema ikiwamo mechi za kirafiki kupata utimamu na kutengeneza muunganiko kwa vijana, uwezo wa kila mmoja ni mapema lakini kipo kitu nakiona chenye kutia moyo kufanya vyema” alisema Makatta.

Makatta aliongeza anafahamu Ligi Kuu ilivyo na ushindani, hivyo anapoelekeza anafahamu ni namna gani ya kuweza kupambana na timu pinzani, huku akijivunia historia yake.

"Sina ugeni wa Ligi wala kwenye timu ni mambo madogo ya kufanyia kazi kuleta ushindani, kimsingi nahitaji kuona Prisons yenye kasi na soka safi uwanjani ya matokeo" alisema Makatta.

Chanzo: Mwanaspoti