Wakati baadhi ya timu za Ligi Kuu zikichekelea mapumziko mafupi ili kujiimarisha, huko Ruvu Shooting imekuwa tofauti kwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mbwana Makata akieleza kasi yao imekata na sasa wanaanza upya.
Timu hiyo ambayo ipo nafasi ya 15 ikiwa na pointi 20, imeweka kambi yake jijini hapa kujiandaa na mchezo dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa, Aprili 9 kwenye Uwanja wa Sokoine.
Katika mechi iliyopita Maafande hao wakicheza kwenye uwanja huo waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City huku wakionesha soka safi na la kasi mwanzo mwisho.
Kwa sasa Ligi Kuu imesimama kupisha michuano ya kimataifa na ya Kombe la Shirikisho (ASFC) na inatarajia kuendelea Aprili 9.
Akizungumza jijini hapa, Makatta alisema licha ya mapumziko kuyatumia kurekebisha makosa, lakini pia imewapunguzia kasi waliyokuwa nayo na sasa ni kama wanaanza upya kusuka nyota wake.
Alisema hadi sasa anaona bado kazi kubwa ipo kwa beki na straika wake akieleza anaendelea kupambana na maeneo hayo kuhakikisha mchezo ujao wanaendeleza ushindi.
“Uliona mechi iliyopita tulicheza vizuri na kupata ushindi, lakini mapumziko haya vijana walienda kupumzika inamaana ile kasi imepungua tunaanza upya. Tatizo kubwa lipo kwenye eneo la beki na straika kwa sababu katika mechi za kirafiki tumeruhusu mabao mengi na kufunga machache, lazima nilifanyie kazi kabla ya mechi ijayo,” alisema Makatta.
Straika wa timu hiyo, Evaligestus Mujwahuki alisema licha ya matumaini waliyonayo kuinusuru timu hiyo, lakini presha ni kubwa kikosini kutokana na kiu waliyonayo ya uhitaji wa alama tatu kwenye mechi zilizobaki.
“Mechi zilizobaki tunafikiria ushindi ili kukwepa kushuka daraja, hatujakata tamaa,” alisema.