Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makatta: Pamba haijengwi kwa siku moja

Pamba Jiji Mwanza Makatta: Pamba haijengwi kwa siku moja

Wed, 18 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maneno ya mashabiki kwamba Pamba haichezi vizuri na inapata ushindi kwa tabu ni kama yamemfikia kocha mkuu wa timu hiyo, Mbwana Makatta ambaye amewaomba wawe wavumilivu kwa kikosi hakijengwi kwa usiku mmoja tu.

Licha ya kupata ushindi katika michezo mitatu,sare mbili na kupoteza mchezo mmoja pekee huku ikiwa imeruhusu mabao mawili katika mechi sita za Ligi ya Championship, lakini mashabiki wa klabu hiyo kongwe hawafurahishwi na soka linalochezwa na kikosi chao kilichosheheni nyota wengi kutoka Ligi Kuu.

Akizungumzia maendeleo ya kikosi chake, Makatta anayefahamika kwa kupandisha timu mbalimbali kwenda Ligi Kuu, alisema ligi siyo kushinda tu kila siku bali ni safari ndefu ya kuyafikia mafanikio hivyo wanapaswa kuwa wavumilivu na kuiunga mkono timu yao.

“Nazidi kuwasihi wawe wavumilivu kwa sababu siku zote ligi siyo kushinda tu kwa hiyo waelewe ni safari ndefu sana kuweza kufikia mafanikio, hata hao mabingwa wa kihistoria Yanga nao walipoteza kwenye ligi wakajipanga upya kuweza kushinda,”

“Kwa hiyo wawe wavumilivu pale kwenye kasoro tukae turekebishe tuone nini cha kufanya tutafikia tageti kabisa niwapongeze kwa kuwa bado wako na timu yao, sisi ahadi yetu ni kuwaheshimisha waajiri wetu na kulipa imani waliyotupatia,” alisema Makatta.

Wachezaji wa timu hiyo wamewekewa bonasi ya Sh100,000 kila wanaposhinda mechi ya Championship, ambapo kutokana na mwenendo wa kusuasua hivi karibuni mlezi wa timu hiyo, Amos Makalla alitembelea na kuzungumza na wachezaji na benchi la ufundi akitaka waongeze bidii.

Akizungumzia hali hiyo, Makatta alisema :“Ujumbe wa mkuu wa mkoa na ujio wake mazoezini ni meseji tosha ya kuwa wameweka malengo ya kuhakikisha timu inapanda Ligi Kuu pale mwenendo unapokuwa hauendi vizuri yeye kama mlezi ni wajibu wake kujua nini tatizo na nini cha kufanya,”

“Alitupa maagizo yake akazungumza na wachezaji na sisi tukasema ya kwetu ili kumaliza changamoto zilizokuwepo na kutekeleza mambo ya msingi, kwa hiyo kilichobaki sasa ni kumheshimisha kwa kupata pointi tatu muhimu ili ujio wake iwe ni chachu ya kufanya vizuri,” alisema Makatta.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live