Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makata ashika kichwa pa kuanzia Ruvu Shooting

Makata Pic Data Kocha mpya wa Ruvu Shooting, Mbwana Makata

Thu, 8 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kutangazwa kuchukua nafasi ya Kocha Boniface Mkwasa aliyebwaga manyanga kuifundisha Ruvu Shooting, kocha mpya wa timu hiyo, Mbwana Makata amesema ni furaha kwake kurejea tena kwenye soka la ushindani baada ya kukaa nje kwa muda mrefu japo anakiri kukabiliwa na changamoto kubwa.

“Siwezi kusema ni kitu gani nitakachoanza nacho kwa sasa hadi kesho (leo) nitakapokutana na wachezaji na kuona tunaanza na kipi lakini hakuna jambo kubwa la kufanya isipokuwa kuangalia mapungufu yaliyopo na kuyarekebisha,” alisema Makata kwa kifupi.

Juzi Jumanne, Msemaji wa Ruvu, Masau Bwire alimtanga Makata na msaidizi wake Renatus Shija na tayari wapo kambini kuendelea na mazoezi kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi huku Mkwasa akiacha ripoti ya kuongezwa kwa washambuliaji kwenye dirisha dogo la usajili.

Matokeo mabaya hasa katika mechi 10 za mwisho za mzunguko wa kwanza yanaelezwa kuwa ndio chanzo cha Mkwasa kuamua kujiuzuru nafasi yake kwani katika mechi hizo Ruvu Shooting ilivuna pointi moja tu iliyopata katika sare dhidi ya Prisons lakini mechi nyingine tisa ilipoteza zote.

Makata anaingia kuinoa Ruvu Shooting baada ya kumaliza adhabu yake ya kufungiwa miaka mitano na Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) kwa kugomea kuingiza timu uwanjani katika mchezo wao dhidi ya Namungo msimu uliopita wakati akiinoa Mbeya Kwanza. Hata hivyo, alipunguziwa adhabu na kutakiwa kutumikia kwa miezi sita baada ya kuomba radhi.

Masau alisema wamesononeshwa na wamehuzunishwa na uamuzi aliouchukua Mkwasa kwani waliamini matokeo mabaya waliyokuwa wanapata ni kipindi cha mpito.

“Tulikuwa na kocha wetu Mkwasa na kwa hakika kazi yake tuliifurahia na kuipenda sana na hakuna Mtanzania asiyejua kazi ya yake katika kufundisha mpira.

“Mkwasa ameandika barua kwa uongozi ya kuuomba kuachia ngazi kutokana na mwenendo na matokeo ya timu hasa katika mechi 10 za mwisho za mzunguko wa kwanza ambazo tumeambulia pointi moja tu jambo ambalo halijawahi kutokea,” alisema Masau

“Kocha nadhani akaona apumzike kwa hiari yake licha ya kwamba tumepokea kinyonge uamuzi huo kwa sababu bado tulimwamini na tulijua ni changamoto za kawaida ambazo zipo siku hasa mzunguko wa pili zingeisha na tungeanza kufanya vizuri. 

“Tuliwahi kushuka mwaka 2014 tukiwa na Kocha Tom Olaba, lakini hatukumwacha tuliendelea naye hadi Daraja la Kwanza na akaipandisha tena timu, hivyo timu kupata matokeo mabaya huwa hatukimbilii kumfukuza kocha bali tunaangalia wapi kuna tatizo na tunalitatua.”

Alisema baada ya Mkwasa kuandika barua ya kujiuzulu, walianza harakati za haraka kutafuta kocha mbadala na kumpata Makata.

“Makocha wetu wapya, Makata na Shija tayari wako kambini kuendelea na mazoezi na timu ili mzunguko wa pili turejee kwa nguvu kubwa.

 “Tunaamini mzunguko wa pili tutarudi tukiwa vizuri kwani wachezaji wetu 11 ambao ligi ilipoanza walienda kwenye mafunzo ya kijesho tayari wamemaliza na kuna taratibu tunakailisha hivyo mzunguko wa pili tutakuwa nao.

“Hivyo yale mapungufu yaliyoonekana kwenye mzunguko wa kwanza yaliyosababisha tukawa nafasi ya pili kutoka mwisho yatamalizika kwani tutaanza kumshusha mmoja mmoja na kupanda hadi kileleni na sisi tukaonje hilo baridi la kileleni,” alisema Masau.

Wakati huohuo, Masau alisema mwishoni mwa mwezi huu uwanja wao wa Mabatini unaweza kukamilika na wakaanza kuutumia kwenye mechi za mzunguko wa pili.

“Tangu msimu huu uanze tumekuwa tukitumia uwanja wa Uhuru baada ya uwanja wetu kufungiwa kutokana na sehemu ya kuchezea (Pitch) kuonekana haistahili.

“Mwishoni mwa mwezi Desemba kama mambo yatakwenda jinsi tulivyokusudia uwanja wetu utakuwa bora sana na wenye viwango na tunataka ufanane na ule uwanja utakaotumika kucheza mechi fainali ya kombe la Dunia kule Qatar,” alisema Masau.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live