Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makapu atoboa siri alichoambiwa na Yondani mechi na Simba SC

99310 Makapu+pic Makapu atoboa siri alichoambiwa na Yondani mechi na Simba SC

Thu, 19 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mashabiki wa Yanga huwaelezi kitu kuhusu beki wao kisiki Kelvin Yondani ambaye amekuwa kiongozi ndani ya uwanja akibebwa na uzoefu.

Uzoefu, ubora na kujituma ndani ya uwanja kumemtambulisha Yondani kama mmoja wa mabeki hodari katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Uwezo wa kucheza kwa nguvu dakika zote akiipigania Yanga na timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ unamtambulisha Yondani kama mmoja wa mabeki bora waliowahi kutokea nchini.

Kipaji binafsi cha Yondani kinakumbusha enzi za Yusuf Bana, Ahmed Amasha, Isihaka Hassan ‘Chukwu’, Athumani Juma Chama ‘Jogoo’, Rashid Idd ‘Chama’ na Allan Shomari.

Jumapili iliyopita ilichezwa mechi ya watani wa jadi baina ya Yanga dhidi ya Simba, Dar es Salaam ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Yanga ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Bernard Morrison.

Sura ambayo haikutarajiwa katika mchezo huo ni Said Juma ‘Makapu’ wa Yanga ambaye alicheza kwa ustadi.

Pia Soma

Advertisement
Wengi walitarajia kumuona Yondani akicheza pacha na Lamine Moro, lakini hali ilikuwa tofauti baada ya jina la Makapu kuchomoza katika orodha ya kocha Luc Eymael.

Haikuwa mara ya kwanza Makapu kucheza mechi ya watani wa jadi, lakini kitendo cha kumuweka benchi Yondani kiliwashitua mashabiki wengi.

Akizungumza na Spoti Mikiki, Makapu anadokeza hakutarajia kama Eymael alikuwa amemuweka katika hesabu zake kwa kuwa nafasi hiyo aliamini atacheza Yondani.

Eymael alimwambia nini

Makapu anakumbuka neno la kwanza aliloambiwa na Eymael baada ya kumwambia atacheza mchezo huo wakati akitangaza kikosi wakiwa kambini.

“Nilianza kudadisi jambo wakati tukijiandaa na mechi, kocha alikuwa akiniangalia sana katika mazoezi, kila mara alinisisitiza niwe makini katika ulinzi

“Hakuniambia mapema kama nitacheza lakini jicho lake kwangu lilikuwa tofauti na kawaida yake wakati akifundisha. Ilipofika usiku aliniita na kuniambia kesho utacheza naamini unawamudu Bocco (John) na Kagere (Meddie) nenda kafanye kazi usiniangushe,”anasema Makapu.

Anasema baada ya kupewa taarifa hiyo ambayo kwake hakutarajia kwa kuwa nafasi hiyo alikuwepo Yondani, alijipa moyo wa kujiamini kwamba atacheza kwa ufanisi.

Yondani alimpa neno hili

Makapu anasema muda mfupi baada ya kumalizana na Eymael, Yondani alimfuata na kumwambia ni mechi ngumu yenye kila aina ya ushindani, lakini acheze kwa kujiamini.

Anasema Yondani alimwambia amekuwa akicheza vyema katika nafasi ya beki wa kati, hivyo asiwe na hofu na alimpa mbinu za ziada namna ya kuikabili safu ya ushambuliaji ya Simba.

Mbali na Kagere, Bocco, wakali wengine wa Simba walikuwa Francis Kahata, Hassani Dilunga, Clatous Chama na Luis Misquissone.

“Yondani aliniambia umepata nafasi ya kucheza nenda kaonyesha kipaji chako, usiogope majina ya wachezaji wa Simba, alinipa mbinu ya kuokoa mipira ya hatari

“Baada ya mechi Yondani alinifuata akaniambia umecheza vizuri endeleza ulipoishia alinisisitiza nisilewe sifa ambazo zitamaliza kipaji changu,”anasema.

Nafasi ya beki

Anasema kocha amembadilisha namba kutoka kiungo mkabaji hadi beki wa kati (namba nne) ambayo anasema amekuwa akifanya vyema akiiga kutoka kwa Yondani na Lamine.

Pia anasema ana uwezo wa kucheza nafasi beki wa pembeni, nne, tano, sita, saba, nane na 11 ambazo amewahi kucheza akiwa na timu tofauti uwanjani.

Amtaja Mkude

Makapu anasema Jonas Mkude alikuwa kikwazo kwa Yanga katika mechi zao kutokana na uwezo wa kumiliki eneo la kiungo.

“Najua kazi ya Mkude uwanjani huwa namuona ndiye amekuwa tishio kwetu, amekuwa akifanya kazi kubwa ya kupunguza kasi kwa mfano siku ile kwa Bernard Morrison,”anaongeza Makapu.

Kiraka huyo anasema kamwe hatalewa sifa licha ya kusikia mashabiki wa soka wakisifu kazi nzuri aliyofanya katika mchezo huo kwa kuwa mkakati wake ni kucheza kikosi cha kwanza.

Makapu anasema kauli ya Yondani kumtaka asibweteke haitatoka ndani ya kichwa chake na ameichukua kama fursa kwake ya kucheza kwa nidhamu.

Chanzo: mwananchi.co.tz