Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makame "saluti" kwa John Bocco

Makame Pic Abdulaziz Makame

Sun, 7 Nov 2021 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa mtazamo wa harakaharaka ukikutana na kiungo wa Namungo FC, Abdulaziz Makame (25), unaweza kudhani ni mkimya, lakini ukibahatika kupiga naye stori jamaa ni mcheshi na huwezi kuchoka kuzungumza naye.

Mwanaspoti liligundua ucheshi wa Makame baada ya kufanya naye mahojiano ambapo muda mwingi kicheko kilitawala kutokana na maongezi yake.

Anasema hapendi kuikarahisha nafsi yake, jambo linalomwezesha kufanya kazi kwa kiwango kikubwa akiwa na Namungo

“Moyo wangu una raha. Nafanya kazi kwa utulivu mkubwa na akili ikichoka kwa ajili ya majukumu, basi huwa naangalia mpira wa kikapu. Nikikaa sawa nawajibika ipasavyo,” anasema kiungo huyo aliyewahi kukipiga Simba na Yanga.

SIMBA, YANGA

Makame anasema maisha ya Simba na Yanga ni ghali akitolea mfano wa kambi kuwekwa katika hoteli za kifahari ndani na nje ya nchi, posho nzuri na marupurupu kutoka kwa mashabiki wao vinawapa ari zaidi wachezaji kuupiga mwingi.

“Pamoja na neema iliyopo kwenye timu hizo hapakosekani changamoto kama za mashabiki wanaokupa ufalme. Ukifanya vibaya wanaishusha thamani yako kuonekana siyo kitu,” anasema.

Pamoja na hilo, Makame anasema hakuondoka Yanga akiwa mtupu kwani imempa somo na mwanga wa maisha.

Makame aliyesajiliwa na Yanga msimu wa 2017/18 akitokea Mafunzo ya Zanzibar, anasema elimu aliyoipata katika timu hiyo anaifanyia kazi Namungo FC.

“Yanga ina mchango mkubwa. Nimekutana na makocha waliokiinua kipaji changu kwa kunipa nafasi ya kucheza kama Boniface Mkwasa na Mwinyi Zahera ambao walikuwa wananiambia nina kitu mguuni kwangu napaswa kukifanyia kazi.”

Nje na makocha hao, anasema kuna wachezaji akiwamo David Molinga kabla ya kukutana naye tena Namungo FC, wakiwa Yanga alimjenga kustahimili changamoto kwa kupigania kipaji chake.

“Wakati nipo Yanga Molinga alikuwa ananiambia nina kipaji kikubwa anatamani kuniona mbali. Mungu mkubwa nimekutana naye Namungo ambapo tunaendelea kuelekezana vitu vingi vya kimpira,” anasema.

NDANI YA NDEGE

Katika msimu wa 2014/15 akiwa na Simba wakienda Afrika Kusini kuweka kambi kujiandaa na msimu mpya wa ligi, Makame anakisimulia kilichomkuta kuwa hakukitarajia.

“Nilijiunga na Simba B mwaka 2014 baada ya kucheza mechi moja ya michuano ya vijana ya Rolling Stone, nikapandishwa timu A. Sasa nilikuwa sijawahi kupanda ndege,” anasema.

“Nikapanda ndege, ilipoanza kupaa nikapiga kelele. Kila mtu akanigeukia na kunicheka. Nilihisi utumbo unakatika. Baada ya kufika Afrika Kusini, Awadhi Juma kocha wa Mtibwa Sugar B kwa sasa akawa ananiambia umezoea kupanda boti na magari, sasa huku ndugu yangu utatapika.”

Mbali na hilo, Makame anamzungumzia meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu kwamba ametumia mali na muda wake mwingi kwa ajili ya kuwaendeleza vijana.

“Kiukweli wachezaji tuliopitia mikononi mwa Rweyemamu tunajua alivyotoa mali na muda wake kwa ajili yetu. Hata tukija kufanikiwa lazima tuje kumkumbuka huyo baba,” anasema.

BOCCO STRAIKA WA NCHI

Makame anasema tangu aanze kucheza soka la ushindani anamfuatilia nahodha wa Simba, John Bocco namna alivyo bora katika kucheka na nyavu akimuona kuwa ni straika bora kitaifa.

“Binafsi namuona Bocco kama straika wa nchi. Anastahili kuigwa na chipukizi kwa nidhamu yake ya kazi, kujituma na kutimiza majukumu,” anasema Makame.

Anamtaja mchezaji mwingine aliyemvutia hadi kucheza kiungo kwamba ni Athuman Idd ‘Chuji’ jinsi alivyokuwa na stamina na kucheza soka la burudani.

“Wapo wachezaji wengi ninaowakubali kwa nafasi zao nje na hao. Kuna Jacob Massawe ambaye amekuwa mfano wa kuigwa katika mambo mengi,” anasema. Massawe anaichezea Namungo kwa sasa.

POLISI TZ, NAMUNGO

Mchezaji huyo anasema japokuwa kipato cha Polisi Tanzania na Namungo FC hakifanani na vile vya Simba na Yanga, anachokifurahia timu hizo ni utulivu.

“Hizi timu viongozi wanajua ‘kuhendo’ wachezaji sana. Ndio maana wanacheza kwa viwango vikubwa kwani nina utulivu wa akili ya kazi. Kitu nachokipenda maishani mwangu ni raha ya moyo sipendi kukarahishwa,” anasema.

“Mfano posho ambayo nilikuwa napata wakati nikiwa Polisi Tanzania ilikuwa Sh250,000, ila kwa sababu ya utulivu niliokuwa napata nilijikuta nina furaha.”

SOKA LA KITAA

Makame anasema wakati anasaka mafanikio ya soka aliwahi kucheza ndondo sehemu mbalimbali na anaeleza kuwa kuna wakati alikuwa akiichezea timu ya FC Siko ya Daraja la Pili iliyopo Zanzibar ambapo walikwenda kucheza michuano ya kuwania mbuzi.

“Kwetu ni mjini kunaitwa Kwahani, mechi tulikwenda kucheza mbali kunaitwa Bungi. Tumemaliza kucheza tukapewa Sh500 tena ya nauli. Narudi nyumbani nimechoka sina kitu, iliniuma sana ila sikukata tamaa ya kutafuta,” anasema.

MAMA YAKE NA PRESHA

Makame anasema mama yake, Mwanaheri, kuna siku alipatwa na presha kutokana na mwanawe kununuliwa na timu ya FC Siko.

“Nilikuwa nimetokea timu ambayo haichezi daraja lolote nikanunuliwa na FC Siko kwa Sh300,000 moja kwa moja nikampelekea mama yangu. Akaniuliza umezipata wapi, akaambiwa na viongozi wangu kwamba ameuzwa. Hapo ndipo ilipoanzia shida,” anasema.

“Akawaambia sitaki mwanangu auzwe.... Atarudi nyumbani kweli?” Wakamfafanulia akaelewa ila pesa alizikataa.”

Chanzo: Mwanaspoti