Licha ya kupata pointi sita katika michezo miwili ya nyumbani kwenye Ligi ya Championship, Mlezi wa Pamba Jiji, Amos Makalla amesema bado kuna mambo mawili ya kufanyia kazi wakati kikosi hicho kikiwa ugenini.
Pamba imepata pointi hizo katika uwanja wa nyumbani wa Nyamagana jijini Mwanza baada ya kuzichapa Cosmopolitan mabao 4-0 na Pan African bao 1-0 na kukaa kileleni baada ya kufunga mabao matano bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Makalla ambaye ni mkuu wa mkoa wa Mwanza aliwapongeza wachezaji na benchi la ufundi kwa kuanza vyema huku akiwataka kuongeza umakini katika eneo la mwisho na kuongeza upambanaji ili kupata pointi nyingi ugenini.
“Ni mwanzo mzuri kwetu na tumeona Pan imetupa upinzani mkali, tunashukuru kwa ushindi tuliouapata ingawaje jukumu lililoko mbele yetu ni kuhakikisha tunaendelea hivihivi kwenye michezo yetu ya ugenini,” alisema.
Kwa upande wa kocha wa timu hiyo, Mbwana Makata alisema licha ya ushindi mwembamba walioupata ila malengo yao mama msimu huu ni kupata pointi tatu tu kwenye kila mchezo japo juhudi kubwa zinahitajika kutimiza malengo hayo.
“Tuna kazi ngumu, kwani kila timu imejipanga kufanya vizuri,|” alisema.