Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makala Maalum: Gharama za mchezo ndo kina nani?

Mashabiki Simba Mkapa Gharama za mchezo ndo kina nani?

Sun, 23 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kila baada ya Shirikisho la Soka (TFF) kutangaza mapato na mgawanyo wa mechi za Ligi Kuu na hasa za watani wa jadi, Simba na Yanga, huibuka mjadala wa uwingi wa makato yanayochotwa na vyombo vingine shiriki. Huku swali kubwa likiwa “hao kina gharama za mchezo ndio kina nani?”

Hii hutokea kila mwaka na maoni ya wengi ni kwamba makato ni mengi na yanazinyonya klabu ambazo hutumia fedha nyingi kwenye maandalizi, zinasajili wachezaji kwafedha nyingi, ndizo zinazohangaika kutangaza mechi hizo ili mashabiki wafurike uwanjani na ndizo hasa zenye mechi hizo au Ligi Kuu kwa ujumla.

Makato hayo hutokana na kanuni ambazo huandaliwa au kuboreshwa kila wakati msimu mpya unapokaribia na baadaye klabu kupewa kwa ajili ya kujua jinsi zitakavyopata mgawo wake pamoja na miongozi mingine ya kimchezo.

Ni vigumu kusikia klabu zikilalamika baada ya kanuni hizo kutoka, labda ombi lao kubwa lilikuwa ni lile la kutaka klabu mwenyeji achukue mapato yote.

Kwa mujibu wa kanuni za sasa mgawanyo wa mapato ya mlangoni unafanywa kwa kwanza kabisa kutoa asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, na fedha zinazobaki hukatwa asilimia 3 kwa ajili ya kupeleka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambalo linashughulika na maendeleo ya michezo pamoja na gharama za mchezo huo.

Baada ya kutoa makato hayo, fedha zilizosalia zitagawanywa kwa klabu mwenyeji kuchukua asilimia 60, Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kuchukua asilimia 8, huku asilimia 7 zikitengwa kwa ajili ya gharama za mchezo. Wengine wanaonufaika na fedha hizo ni uwanja ambao huchukua asilimia 15, TFF ikichukua asilimia 4, chama cha mkoa ambao mechi imechezwa hupewa asilimia 6.

Maelezo katika mgawanyo huo yako bayana kabisa, ingawa ufafanuzi wa baadhi ya vipengele ndio huibua mijadala. Mfano kipengele cha gharama za mchezo.

Zamani ukosoaji wa kipengele hiki ulilenga zaidi katika soda na vitafunio kwa watazamaji wanaokaa eneo la wageni muhimu. Wakati ule zikitajwa Sh. Milioni 2 kuwa zilitumika kwa vinywaji na vitafunio, kila mtu alighadhibika asikubaliane na mchanganuo huo. Ni dhahiri kuwa hicho ni kiwango kidogo, hata kama wakati ule kilionekana kikubwa.

Lakini hadi leo bado kipengele hicho hakijaeleweka vizuri kwa wadau, kibaya zaidi hata kanuni hazitoi mwongozo wa wazi kuhusu kipengele hicho.

Katika mechi ya mwishoni mwa wiki baina ya Simba na Yanga, kipengele hicho kilibeba Sh. Milioni 22.048 kati ya Sh. Milioni 410.6 zilizopatikana.

“Asilimia saba (7) ya gharama za mchezo itatumika kulipia gharama mbalimbali za huduma zitakazoalikwa na kutolewa kufanikisha mchezo husika. Gharama za mchezo zigawanywe kwa kutumia fomu maalum inayotolewa na TPLB,” inasema kanuni ya 29 ya Kanuni za Ligi Kuu.

“TPLB/TFF itatoa waraka mwanzoni mwa msimu utakaofafanua viwango vya malipo ya maofisa wa mchezo na utaratibu wa malipo.”

Kwa hiyo kanuni haziendi mbali kufafanua wahusika katika kipengele hiki, ingawa mbele kidogo inaeleza kuwa “gharama za msimamizi wa kituo, kamishna, mratibu wa mchezo, mtathmini wa waamuzi na waamuzi zitalipwa na TLPB” labda kwa kutambua kuwa Ligi Kuu ina mdhamini, NBC, ambaye anagharimia malipo hayo.

Tatizo kama ni kweli TPLB inatumia fedha hizo za mdhamini au inasubiri mgawo huo wa gharama za mchezo iweze kuwalipa waamuzi. Hofu hii inatokana na habari kuwa kuna madai makubwa ya waamuzi kiasi kwamba mmojawapo ameamua kulifikisha suala hilo mahakamani, huku wale wenye msimamo kuhusu haki zao, ama wakitishiwa au kuondolewa kwenye ratiba.

Kabla ya mechi hizo za watani, TPLB hutoa orodha ndefu ya maofisa wa mechi na safari hii ilikuwa na watu 16, akiwemo mtathmini wa waamuzi, Brian Nsuba Miino ambaye alitokea Uganda. Bado sababu hasa za kusafirisha tathmini wa waamuzi kutoka zaidi ya kilom ita 1,300 kuja kutathmini mwamuzi wetu.

Ni kitu gani hasa kiliifanya TPLB ikubali kuingia gharama hizo kubwa kwa ajili ya mtathmini tu na klabu shiriki zilishirikishwa kufikia uamuzi huo?

Ingawa ni kweli kwamba hao watalipwa na TPLB, bado uamuzi huo ni ufujaji wa fedha au pengine ulifanywa kwa kuwa sinema inaweza kutumika kutumia kipoengele cha gharaza za mechi kuingiza malipo hayo.

Kipengele kingine ni mgawo wa Sh. Milioni 18.9 kwenda kwa Chama cha Soka cha Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA). Huu ni mgawo ambao hulalamikiwa kila mwaka kwa kuwa hakuna shughuli kubwa ambazo DRFA inafanya, hasa ikizingatiwa kuwa wilaya za Dar es salaam huchukuliwa kama mikoa.

Hata ligi za wilaya, licha ya kuwa mkoa kuwa katika kitovu cha shughuli za kibiashara na kijamii, bado hazina mvuto wa kuweza kuvutia wadhamini. Siku hizi ni shida hata kumjua bingwa wa Kinondoni au Ilala au Temeke, achilia mbali hizo wilaya mpya ambazo zinazidiwa na Ubunge iliyochangamka.

Klabu za Dar hazitafuti tena nafasi ya kucheza Ligi Kuu kwa kupitia mchakato uliowekwa tangu ngazi ya wilaya, bali zinafanya njia ya mkato ya kununua klabu ambazo zimeshafika Ligi Daraja la Kwanza au la Pili. Ndiko Pan African wanakotafutia nafasi ya kufufuka.

DRFA inatumiaje mgawo wa mechi zote za Ligi Kuu zinazochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Uwanja wa Azam Complex na Uwanja wa Uhuru? Swali limekuwa kuna haja ya kuipa DRFA fedha zozote? Au kuna haja hata ya DRFA kuwepo? Iweje DRFA kiwe chombo cha kunyonya mapato ya hizi klabu kubwa wakati haina shughuli zozote ama kuzisaidia ama kusaidia maendeleo ya soka.

Kama ni mafunzo kwa makosa, ni wanafunzi ambao huchangia kuanzia Sh50,000 kwa cheti cha awali na husimamiwa na wilaya. Kazi kubwa ya DRFA ambayo unaweza kusema ilimamsha hadi mkuu wa mkoa aende kuwa mgeni rasmi ni ipi?

Wakati TFF ilipoamua kuanza kutumia tiketi za kielkektroniki, lengo lilikuwa ni kupunguza gharama za mechi. Lakini kuna uongozi ambao ulikuja kuvuruga uwekezaji mkubwa wa miundombinu uliofanywa na benki ya CRDB kufanikisha tiketi hizo.

Takriban miaka 10 baadaye, gharama za tiketi ziko palepale pamoja na kutumia N. Card. Katika mechi ya mwishoni mwa wiki, kipengele hicho kilichota Sh. Milioni 22.6. Hizi ni gharama ambazo hazitolewi kwa asilimia bali ni bili ambayo ni lazima ilipwe.

Tiketi ni za kielektroniki, lakini bado utaratibu wa uingiaji si wa kidigitali. Wakati kwa utaratibu wa mpango wa CRDB, shabiki angeweza kukata tiketi yake kwenye maeneo mbalimbali kama katika mashine za ATM, kwa utaratibu wa N. Card shabiki anaweza kulipia kimtandao, lakini bado akalazimika kwenda kuchapisha tiketi pale uwanjani.

Matokeo yake, kumejazwa wakatisha tiketi wanaoka ndani ya uzio wan je ya uwanja ambao kwa kiasi kikubwa husababisha kero kwa watu wanaotaka kuingia kwa kuwa hakuna utaratibu wa kusimama foleni bali kukumbatia nyavu hadi mkatishaji akuone.

Bado kuna wale wahakiki tiketi, ambao kielektroniki walitakiwa wawe na tochi maalum zinazong’amua tiketi hiyo. Ni wazi kwamba hapa utahitaji tena watu wengi kuweza kufanikisha uiongiaji, hasa katika nchi kama hii ambao mashabiki wamejijengea utamaduni wa kuingia uwanjani dakika chache kabla ya mechi kuanza, ukiacha wale mashabiki wanaoenda kuanzia asubuhi.

Na kwa maana hiyo, bado utakuwa na gharama kubwa, iwapo wahakiki hao wa tiketi na wakataji wanahusishwa kwenye kipengele cha tiketi. Na hata kama hawatahusishwa, bado wataingia kwenye gharama za mechi.

Mjadala mwingine ni kwenye mgawo wa Sh. Milioni 12.6 ambazo zimeenda TFF na Sh. Milioni 25.2 ambazo zimeenda TPLB. Ni dhahiri kuwa TPLB ni lazima ichukue mgawo wake ili iweze kufanya shughuli nyingine za kiutawala na mafunzo, ingawa haionekani kuipromoti ligi yenyewe au kuitangaza chapa ya Ligi Kuu kama ilivyo kwa Premier League, La Liga, Serie A na Bundesliga zinavyojitangaza hadi huku.

Wengi wanaona TPLB na TFF ni kitu kimoja na hivyo kuchukua mgawo huo ni kuzinyonya klabu. Hili bado halijakaa sawa na litakaa sawa iwapo TPLB itakuwa na mamlaka hyake kamili, kuanzia katika fikra hadi utendaji. Ni kweli TFF ni lazima ijipatie chochote kutoka mechi za Ligi Kuu, lakini kwa kiwango gani? Mbona CAF au Fifa hazichukua mgawo kwa asilimia?

Haya ni naswali na hoja ambazo huibuka kila wakati mapato ya mechi za Ligi Kuu yanapotangazwa. Hizi ni kanuni ambazo ziko miaka na miaka na mamlaka haziwezi kujitetea kuwa mbona utawala fulani ulifanya hivyohivyo. La hasha, kadri dunia inavyobadilika ndivyo watu inabidi wabadilike.

Wakati huu ambao tunaelekea kwenye uchumi wa kidigitali, mengi yanmgesharahishwa na teknolojia. Kesho tutaangalia ni vipi tunaweza kutoka katika mijadala hii na kujikita zaidi kujadili maendeleo.

Chanzo: Mwanaspoti