Orodha ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi imeongezeka kadiri siku zinavyokwenda mbele.
Hii imechangiwa na namna ambavyo wachezaji ambao walitoka mapema kuitangaza vizuri nchi sambamba na klabu za ndani kufanya vizuri kimataifa.
Leo hii yupo Mtanzania, Baraka Majogoro ambaye ametoka katika Ligi Kuu Bara na moja kwa moja ameenda Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Mwanaspoti lilimtafuta na kufanya mazungumzo kwa kina juu ya safari yake kutoka KMC hadi Afrika Kusini.
KMC INGEKAZA ASINGECHOMOKA
Wakati anapata dili la kwenda Afrika Kusini alikuwa tayari ameshazungumza na klabu yake ya zamani KMC juu ya kuongeza mkataba na kukubaliana kila kitu.
Kilichobaki kwa pande hizo mbili ni kusaini tu na KMC tayari ilishamuweka kwenye mipango ya kumtumia msimu huu.
Majogoro anakiri kama mabosi wa KMC wangeamua asiondoke basi ingekuwa ngumu leo hii kuitumikia Chippa United.
“Naushukuru sana uongozi wa KMC tena sana, umeonyesha utu kufanikisha hili jambo bila wao kutokuwa na utu kwangu ingekuwa vigumu.
“Ieleweke tu walikuwa na utu kwa sababu nashindwa kuweka wazi (nina kigugumizi) kwa walichonifanyia.”
Hata hivyo, Mwanaspotii lilipenyezewa kwamba Majogoro alisaini mkataba wa awali ambao kama KMC wangekomaa asingeweza kuondoka.
MAJARIBIO WIKI, YAMPA ULAJI
Baada ya Ligi Kuu kumalizika ndipo mchakato rasmi wa kwenda Afrika Kusini kucheza soka la kulipwa ulianza kwa Majogoro.
Majogoro anasema mchakato ulikuwa wa muda mrefu lakini rasmi ulikolea moto baada ya ligi kumalizika na KMC ilipomruhusu basi alikamilisha na kuondoka.
Anasema kwenye majaribio hakuwa na wakati mgumu kutokana na kwamba alikuwa fiti kwa sababu alitoka katika Ligi Kuu.
“Hayakuwa majaribio ya uwanjani tu, tulianza kwa kupima afya na kuingia darasani kusoma kisha gym, nilijua nimemaliza majaribio na kupita baada ya kukamilisha lakini haikuwa hivyo;
“Nilitolewa na kuambiwa zamu inayofuata ni uwanjani, walinipa mechi nne ambazo tulicheza Durban baada ya hapo nikasaini na ilikuwa wiki tu.”
Majogoro anaongeza akisema; “Changamoto kubwa ilkuwa ugeni wake kwenye mazingira mapya lakini pia lugha ila havikumfanya ashindwe kutimiza malengo yake.”
ACHEKELEA KUCHEZA NJE, MSOSI NI FRESHI
Majogoro anasema baada ya kufuzu majaribio na kutimiza ndoto alibaki akitabasamu kwani jambo hilo lilikuwa ni ndoto ya muda mrefu.
“Kwakweli nafurahi kucheza mpira nje kwani ilikuwa ndoto yangu ya muda mrefu, Mungu anisimamie nifikie malengo yangu,” anasema kiungo huyo aliyeibuka mchezaji bora kwenye mechi mbili.
Majogoro anasema baada ya kupata dili la kucheza Afrika Kusini alipata wasiwasi wa masuala ya chakula lakini baada ya muda alijionea ni vitu vya kawaida.
“Nilipata changamoto kidogo lakini hii yote ni Afrika kuna baadhi ya vyakula vinaendana, kama ugali upo ila upikaji ni tofauti.
“Huku wana mchele wa tofauti na nyumbani, nyama ni zilezile ila upikaji nao ni tofauti lakini nimeanza kuzoea kidogo kidogo.”
HAKUNA KAMBI
Majogoro anasema kitu pekee ambacho kimezidi kumkomaza ni masuala ya kutokaa kambini kama ilivyo kwa timu ambazo amecheza hapa nchini.
Kiungo huyo anasema katika timu yao ni siku moja kabla ya mchezo huwa wanakaa kambini na muda mwingine hukutana asubuhi kisha jioni mechi.
“Kuna utofauti mkubwa na nyumbani, huku kila mtu yupo kwake inaweza ikawa jioni mna mechi kwahiyo mnakutana asubuhi.
“Muda mwingine mnaingia leo jioni kisha asubuhi ndio mnacheza mechi na baada ya hiyo mechi kila mmoja anaenda kwake.”
Kwa nyumbani hata timu zenye uchumi mkubwa na wachezaji wa kimataifa, Simba, Yanga na Azam huwa zinakaa kambini kwa muda wa takribani wiki moja kujiandaa na mchezo husika.
SAUZI KUISHI KWA AKILI
Afrika Kusini inadaiwa jamii ya wageni huwa na wakati mgumu kutokana na kuonekana kama vile wameenda kuchukua malisho ya wenyeji.
Katika hilo usalama wa wageni unakuwa mdogo katika miji kadha na hilo hata Majogoro amekiri kulisikia na aliambiwa kuwa nalo makini.
“Nilisikia ila sasa najionea, nipo Port Elizabeth kidogo naona hayo matukio ya namna hiyo sio sana;
“Kikubwa mlinzi wa kwanza ni wewe mwenyewe, kuna muda haina haja ya kuambiwa bali wewe mwenyewe unatakiwa kujichunga.”
MALENGO BADO
Anasema Afrika Kusini hajafika ndoto yake ni kucheza Ulaya.
“Imani yangu ni nikipambana zaidi nitafika mbali zaidi, kwanza nashukuru kucheza hapa kwani nimepiga hatua moja.
“Inabidi ijulikane nimepiga hatua ya kwanza, hivyo naweza kupiga hatua ya pili muda wowote.”