Imefahamika kuwa, Kiungo kutoka nchini Tanzania Baraka Gamba Majogoro amezivutia klabu nguli nchini Afrika Kusini Kaizer Chiefs na Orlando Pirates.
Baada ya kucheza michezo kadhaa ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini ‘PSL’ akiwa na klabu ya Chippa United iliyomsajili mwanzoni mwa msimu huu 2023/24, Majogoro amezivutia klabu hizo nguli zenye maskani yake makuu eneo la Soweto mjini Johannesburg.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa katika Tovuti ya Soccer Laduma ya Afrika Kusini zinaeleza kuwa, tayari baadhi ya maafisa wameanza kumfuatilia kiungo huyo wa zamani wa klabu za Mtibwa Sugar na KMC FC zote za Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Ni Chiefs ambao walikuwa wameonyesha nia ya kwanza kwa mchezaji huyo lakini sasa Pirates pia wanamfuatilia. Ni kiungo wa kipekee. Watu wengi wanamlinganisha na Andile Jali katika enzi zake. Labda ndio sababu anavutia umakini kutoka kwa timu kubwa,”
“Kwa sasa hatuwezi kusema ni wapi atakwenda kwa sababu klabu zote mbili zimeonyesha nia na hakuna chochote rasmi kilichofanyika. Lakini ni dalili nzuri kuwa na timu zinazomfuatilia,” imeeleza taarifa ya Tovuti ya Soccer Laduma.
Hata hivyo imefahamika kuwa Uongozi wa Chippa United umejizatiti kumabisha Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26, lakini inakabiliwa na changamoto ya mwaka mmoja uliosalia katika mkataba wake ambao utafikia kikomo Juni 2024.