Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maji ya shingo Bayern

Bayern Mapumziko Maji ya shingo Bayern

Sat, 9 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Haya ni maji ya shingo kuogelea kwa Bayern Munich katika kampeni ya kutetea taji lake la Bundesliga msimu huu wakati ikiialika timu iliyo hatarini kushuka daraja ya Mainz leo kuanzia saa 11:30 jioni.

Ilikuwa ni vicheko tu katikati ya wiki mjini Munich wakati Bayern ilipopindua matokeo ya mechi yao dhidi ya Lazio na kutinga hatua ya robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mapacha wazoefu wa ushambuliaji Harry Kane – ambaye sasa ana mabao 33 katika mechi 33 akiwa na klabu hiyo – na Thomas Müller walishirikiana katika ushindi wa 3-0. Hata hivyo, katika ligi ya ndani, sare ya 2-2 dhidi ya Freiburg wiki iliyopita iliipa nafasi Bayer Leverkusen kuongoza kileleni mwa msimamo wa Bundesliga kwa tofauti ya pointi 10.

Tatizo la mabeki limekuwa ni ishu kubwa kwa kocha anayeondoka madarakani Thomas Tuchel, ambaye alijenga jina lake mara ya kwanza akiifundisha timu ya Mainz.

Joshua Kimmich amekuwa akicheza kama beki wa kulia kuziba pengo la Noussair Mazraoui, Sacha Boey na Konrad Laimer. Laimer amerejea na huenda akaanza leo, jambo litakalomruhusu Kimmich kusogea kwenye eneo la kiungo kuchukua nafasi ya Aleksandar Pavlovic aliyefungiwa. Leroy Sane alianza dhidi ya Lazio baada ya kupona majeraha ya nyonga na anatarajiwa kuendelea kuwapo kikosini nyuma ya washambuliaji watatu Kane, Muller na Jamal Musiala. Serge Gnabry aliingia dakika za mwishoni dhidi ya Lazio baada ya miezi kadhaa ya kuuguza majeraha na anatarajiwa atacheza kwa dakika kadhaa leo, sawa na kinda Mathys Tel ambaye amesaini kuongeza mkataba wa muda mrefu wiki iliyopita.

Mainz wanaingia katika mechi 10 za mwisho za msimu wakiwa katika nafasi ya 17, baada ya kushinda mechi mbili tu msimu huu. Mara yao ya mwisho kushinda ilikuwa ni mwaka mzima uliopita, Aprili mwaka jana, ingawa bado wanayo matumaini madogo ya kunusurika kushuka daraja kutokana na ukweli kwamba FC Cologne wako juu yao kwa pointi moja tu katika nafasi ya kucheza mechi za ‘play-off’ za kuwania kuepuka kushuka daraja.

ALONSO NDOO TATU?

Kikosi cha Xabi Alonso kina nafasi ya kuandika historia mwaka huu kwa kubeba mataji matatu na kubadili jina la utani walilopachikwa la ‘Neverkusen’ hadi kuwa ‘Treblekusen’, na miezi mitatu ijayo itaamua hatima ya timu hii kali.

Bayer Leverkusen haijapoteza mchezo wowote katika mechi 35 za kimashindano msimu huu na hii ni rekodi ya kibabe zaidi Ujerumani ikiipita kwa mbali ile ya Bayern ya kucheza mechi 32 bila ya kupotea mchezo.

Kikosi cha Alonso kinaweza kutwaa ubingwa wa Bundesliga, DFB Cup na Europa League ambako kote mambo yake ni mazuri sana.

Jambo moja linalowatisha mashabiki wa Leverkusen ni kwamba wameshawahi kuwa katika nafasi kama hii huko nyuma, lakini walitoka patupu. Msimu wa mwaka 2001/2002, kikosi matata kabisa cha Leverkusen kikiundwa na mafundi wa boli kama Michael Ballack, Oliver Neuville, Dimitar Berbatov, Lucio na Ze Reberto kilikaribia kutwaa mataji matatu makubwa lakini kiliambulia patupu.

Mei 2002, kikosi cha Leverkusen kililikosa taji la Bundesliga kwa pointi moja tu nyuma ya waliolitwaa Borussia Dortmund, kisha kikalala 4-2 dhidi ya Schalke katika fainali ya Kombe la DFB Cup na kupasuka 2-1 mikononi mwa Real Madrid licha ya kuupiga mwingi sana katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid, kiungo Zinedine Zidane akifunga lile bao kali kabisa la ushindi. Msimu ule ndio wakapachikwa jina la kebehi la ‘Never-kusen’ (kwamba wao kamwe hawabebi ubingwa).

Tangu imeanzishwa Julai 1, 1904 -- yaani miaka 120 iliyopita, Leverkusen haijawahi kutwaa ubingwa wa Bundesliga.

Ikiwa kileleni kwa pointi 64 ikifuatwa na Bayern yenye pointi 54, Leverkusen kesho Jumapili itaivaa Wolfsburg inayoshika nafasi ya 13 kwa pointi 25. Kwa mujibu wa ubashiri wa matokeo ambao unazingatia ubora wa vikosi, matokeo ya siku za hivi karibuni na matokeo ya timu husika zilipokutana, Leverkusen inapewa asilimia 72 za kushinda mechi hii huku Wolfsburg ikipewa asilimia 11 za kushinda na asilimia 17 zikionyesha huenda mechi ikaisha kwa sare.

VfB Stuttgart inayoshika nafasi ya tatu, jana Ijumaa usiku ilikuwa na nafasi ya kuongeza katika pointi 50 ilizokuwanazo wakati ilipoialika Union Berlin, huku Dortmund inayoshika nafasi ya nne ikiwa na pointi 44 itakuwa ugenini leo pia dhidi ya Werder Bremen yenye pointi 30 katika nafasi ya nane.

RB Leipzig yenye pointi 43, moja tu nyuma ya Dortmund, itazidi kuweka presha ya kutaka kuingia kwenye Top 4 ya kukamatia tiketi kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao wakati itakapoialika timu inayoshika mkia ya SV Darmstadt na pointi 13 leo.

Chanzo: Mwanaspoti