Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majeraha ya ugoko, kigimbi hayatakosekana Qatar

Ugoko Kigimbi Majeraha ya ugoko, kigimbi hayatakosekana Qatar

Fri, 21 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Eneo la mguu ndilo la mwili wa mchezaji wa soka ambalo hukumbana na majeraha ya mara kwa mara kutokana kiungo hiki cha chini ya mwili hutumika wakati wa kucheza.

Ni vigumu kwa wachezaji wenye majukumu mengi yakiwamo ya klabu na taifa kutopata majeraha ya ugoko na kigimbi kwani ndio eneo la chini ya mguu ambalo linakwatuliwa zaidi na wapinzani wao wanapotimiza wajibu wao.

Angalau kwa eneo la ugoko huwa na kilinda ugoko kijulikanacho kama ‘Sheen Guard’ lakini kwa eneo la nyuma ambalo ni kigimbi huwa halina kifaa chochote cha kujikinga na majeraha ya kukwatuliwa.

Kwa wanasoka misuli ya kigimbi inawawezesha kufanya mambo mengi ikiwamo kupiga mpira lakini ni eneo mojawapo linalopatwa na majeraha ikiwamo kuchanika kwa misuli yake.

Hapa tunapata picha kuwa wachezaji ni kawaida pia kukutana na majeraha ya eneo hili.

Eneo la mguu chini ya goti mbele yaani ugoko huwa na kikinga majeraha na huwa halina nyama hivyo kutojeruhiwa sana, leo tutaona hatua zinazochukuliwa kwa mchezaji aliyepata majeraha ya kimchezo katika eneo la kigimbi.

KUPUMZISHWA

Inalazimika mchezaji kuondolewa mchezoni endapo amepata jeraha litakalomfanya kushindwa kuendelea. Kuondoa maumivu na uvimbe

Kuwekewa barafu, jeraha la kigimbi hukandamizwa kutumia bandeji yenye kuvutika kama mpira na unyanyuaji mguu kuzidi kifua.

Dawa za maumivu za kupaka au kupulizia pia zinatumika kuzuia maumivu zaidi.

Kundi la misuli ya kigimbi ni yenye nguvu inayoweza kutoa msukumo mkubwa wa kuweza kukimbia, kuruka na kutembea.

Katika hatua za mwanzoni mjeruhiwa anaweza atembee kwa kuchechemea, hivyo ataendelea na hatua hizi na mapumziko.

Uvikaji wa vifaa tiba maalumu kama kiatu, usaidizi wa kutembea na kiti au magongo maalumu.

Kufanya hivi kunasaidia mguu kupata utulivu na kuwa mahali pamoja bila kuchezacheza, vilevile husaidia kutokuwapo au kupunguza kwa shinikizo la uzito wa mwili, hivyo kupunguza kujijeruhi zaidi.

Barafu ni moja ya nyenzo muhimu katika matibabu ya awali ili kupunguza maumivu na uvimbe. Inaweza kuwekwa kwa muda wa dakika 10-20 kwa kila saa 2-4, weka pale unapohisi mguu umepata moto au una vuguvugu.

Ingawa dawa za maumivu zinaweza kutumiwa kukata maumivu na uvimbe mara nyingi huepushwa katika saa 48-72 za mwanzoni kwani dawa hizi zinaweza kuchangia damu kuongezeka na kuvuja katika jeraha.

Katika saa za awali kabisa wengi hupewa paracetamol ya vidonge tu kwani ndio inayokuwa salama na kuvumilika na mwili wa majeraha pasipo tatizo lolote.

Kadiri unavyoimarisha ukandamizaji kwa kutumia ‘clip bandage’ husaidia kuzipa nafuu tishu laini zilizo jeruhiwa na pia kuzuia damu kujivujisha ndani ya mguu.

Kuuweka mguu uliojeruhiwa juu kidogo kuzidi kifua chako ukiwa umelala au kukaa husaidia kurudisha damu kutoka eneo la mguu kwa haraka, hivyo kupunguza uvimbe kwa haraka.

KURUDISHA UFANYAJI KAZI

Kama zoezi la kwanza litaenda vizuri kama inavyotakiwa ubora na ufanisi wa misuli hiyo huweza kurudi kama ilivyokuwa awali.

Ukarabati wa jeraha na kujiunga huchukua takribani wiki sita tu. Wakati huu dhumuni linakuwa ni kusaidia kuzuia gamba la jeraha lilojiunda liwe imara na ufanisi mzuri ili kusiwepo na kujirudia kwa majeraha haya hapo baadaye.

Ni muhimu sana kuliimarisha na kulirudishia ufanisi jeraha lilounga kwa kutumia kusingwa (massage), kuinyoosha misuli hiyo na kuimarisha mishipa ya fahamu na damu kwa mazoezi mepesi ya viungo.

Dalili na viashiria kuwa sasa jeraha limepona ni pamoja kuweza kutembea bila kuchechemea na kuweza kufanya ile mijongeo mbalimbali na kuinyoosha misuli ya kigimbi bila mkwamo.

KURUDISHIA KIGIMBI UWEZO

Ukakamavu na nguvu za misuli hii ni lazima iimarishwe taratibu kuondakana na ile hali ya kutokuweka shinikizo la uzito na kuanza kuweka shinikizo la uzito wa mwili kidogo kidogo mpaka hapo baadaye kuweka shinikizo kubwa la uzito.

Hii ina maana kama mjeruhiwa alikuwa anatumia kifaa au alikua hautumii mguu kuukanyagia moja kwa moja sasa anapaswa kuacha na kuanza kutembea bila usaidizi wa chochote.

Baada ya majuma 1-2 anawezaa kuanza kutembea, kisha akaanza kujinyanyua kidogo kidogo na kuuvuta mwili na kukimbia kidogo kidogo na baadaye akaanza kuruka ruka.

Kuruka na kukimbia kwa nguvu zaidi ina maana kuwa sasa eneo hilo la kigimbi linapata shinikizo la uzito wa mwili na hapo ndipo wataalamu wa viungo hujiridhisha kuwa eneo limepona na mchezaji huendelea na programa ya mazoezi ya viungo na mafunzo.

KUURUDISHIA UWEZO

Misuli ya miguu ndio inayo fanya mielekeo miwili muhimu, yaani kukunyanyua na kukudhibiti kudondoka au kukuvuta chini.

Hatari ya kujitonesa kwa misuli na kuchanika tena hutokea wakati wa unyooshaji misuli. Kuepusha jambo hili mtaalamu wa viungo hutoa mwongozo wakati wa programu maalumu ya mazoezi ya viungo yanayomwezesha kuhimili kujivuta chini kama vile kuchuchumaa, kupiga msamba, kukaa na kuruka kichura haya yanafanyika tu endapo hali ya jeraha itaruhusu.

KURUDISHA UWEZO WA KUKIMBIA

Majeraha ya kigimbi hujitokeza sana pale kunapokuwa na shughuli zinazohitaji kukimbia kasi, hali hii huleta msukumo mkubwa mwilini hasa kujikunja na kujikunjia kwa misuli.

Ili kuzuia kujirudia kwa majeraha unapokuwa unarudi katika mchezo mtaalamu wa viungo atakupa mwongozo maalumu wa mazoezi unaokuelekeza mambo muhimu katika programu ya mazoezi ili kukujengea uwezo wako kama livyokuwa awali.

Ingawa pia itategemea pia na mchezo upi unaocheza na nafasi ipi na kasi unayohitajika kuwa nayo, utapewa mazoezi na mafunzo ili kukuandaa na kwa kuanza mazoezi mepesi.

KURUDI UWANJANI

Baada ya madaktari na wataalamu wa viungo na watoa mafunzo yaani benchi la ufundi kujiridhisha kuwa uko fiti ndipo unapoanza majaribio madogo madogo.

Wataalamu wa viungo huendelea kukufuatilia na kujadili shabaha yao pamoja na muda uliopangwa kurudi mchezoni na ratiba nzima ya mazoezi na mafunzo, hii ni kwa ajili ya kuweza kupata picha kamili kama umepona moja kwa moja.

Matokeo mazuri ni pale tu unapoweza kukimbia kwa kasi, kutumia nguvu, uwezo wa kufanya mambo kwa akili na umakini, na huku pia akijihami dhidi kujijeruhia au kujeruhiwa.

Hii inamaanisha kwamba majeraha ya ugoko na kigimbi hayatakosekana katika fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar kuanzia Novemba 2022.

Lakini kama wakufunzi wataamua kuzingatia matibabu kwa hatua hizi kunaweza kusaidia kurudisha utendaji wa mguu wa mchezaji kama ilivyokuwa hapo awali.

Chanzo: Mwanaspoti