Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta hakuwa sehemu ya kikosi hicho kilichosafiri hadi Algeria kwa ajili ya kupigania nafasi ya kwenda Ivory Coast kutokana na kusumbuliwa kwake na majeraha ya enka aliyoyapata kwenye mchezo wa ligi huko Ugiriki dhidi ya Asteras Tripolis.
Hesabu za Kocha wa Taifa Stars, Adel Amrouche zilikuwa ni kumtumia nahodha huyo kwenye mchezo huo kutokana na uzoefu wake lakini mipango ikawa sio matumizi na badala yake majukumu yake akabebeshwa Simon Msuva.
Samatta ilimbidi atumie mtandao wake wa kijamii kuwatakia kila kheri wapambanaji wenzake waliofanya kile kilichotakiwa na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa 24 yatakayoshiriki fainali hizo.
“Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki wapambanaji wetu.Kila la kheri Taifa Stars,” aliposti Samatta na mara baada ya mchezo huo ambao ulimalizika kwa suluhu, alirejea tena na kusema, “Asante Mungu. Asante wapambanaji, asante wote mlioomba dua njema. Wanangu nawapenda sana.”
Mara baada ya mchezo huo, alionekana Amrouche katika mahojiano yake akitokwa na machozi haamini kilichotokea licha ya kokosekana kwa nahodha huyo na hata kipa, Aishi Manula ambaye naye ni majeruhi lakini imewezekana.
Samatta kwa sasa anauguza majeraha yake na yupo mbioni kurejea katika majukumu yake huku akiwa na kibarua cha kulipigania chama lake kuhakikisha linafanya vizuri kwenye Europa Conference League wakiwa kundi G pamoja na Helsingin Jalkapalloklubi ya Finland, Eintracht Frankfurt ya Ujeruman na Aberdeen ya Scotland.
Katika mashindano hayo, Samatta ataweka rekodi ya kuwa Mtanzania kwa kwanza kucheza michuano yote mitatu barani Ulaya, alianza kukiwasha kwenye Europa League, Ligi ya Mabingwa Ulaya na sasa ni Europa Conference League.
Kwenye ligi ya ndani Ugiriki, PAOK inashika nafasi ya tatu baada ya raundi tatu kuchezwa, imejikusanyia pointi sita nyuma ya Panathinaikos na OFI wote wenye pointi sita na Olympiakos inayoongoza ikiwa na pointi tisa.