Timu ya Manchester United huenda itamkosa kipa namba moja, Andre Onana kwa sababu atakuwa katika majukumu ya kimataifa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2024).
Hiyo ni baada ya kipa huyo kujumishwa kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon hivi karibuni, hivyo litakuwa pigo kwa Man United.
Kipa huyo alikuwa na mgogoro na kocha wa Cameroon, Rigobert Song iliyomfanya kujiondoa katika kikosi ambacho kilishiriki fainali za Kombe la Dunia Qatar 2022.
Baada ya kujiondoa katika kikosi hicho kutokana na bifu na kocha alitangaza kustaafu soka la kimataifa na kuwashangaza mashabiki.
Mlinda Lango huyo wa zamani wa Ajax na Inter Milan alishangazwa baada ya kujumuishwa katika kikosi cha Cameroon kitakachocheza dhidi ya Burundi mechi ya kufuzu AFCON.
Hata hivyo, bado haijafahamika kama Onana atakubali kujiunga na timu ya taifa kufuatia sintofahamu iliyotokea kati yake na Song.
Endapo atakubali kujiunga na timu ya taifa, Onana atakosa mechi nyingi za Man United itakapofika Januari.
Man United itacheza dhidi ya Tottenham Hotspur, Wolves, West Ham na Aston Villa bila kipa huyo aliyesajiliwa kwa Pauni 47 milioni.
Akizungumza kuhusu uamuzi wa kumjumuisha Onana kikosini, Song alisema: “Kama yupo katika orodha, basi amefanya uamnuzi sahihi. Ni kipa mzuri mlango upo wazi kwa ajili yake. Onana hana tatizo.”