Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yazuia uchaguzi wa Chama cha soka Temeke

Nyundoo Mahakama yazuia uchaguzi wa Chama cha soka Temeke

Sat, 3 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, imezuia kufanyika kwa uchaguzi wa Chama cha Soka Wilaya ya Temeke (Tefa) uliokuwa umepangwa kufanyika kesho, Agosti 4, 2024.

Amri ya kuzuia uchaguzi huo imetolewa jana Agosti 2, 2024 na Jaji Obadia Bwegoge, kufutia shauri la maombi ya zuio la muda baada ya kukubaliana na hoja zilizotolewa na waombaji waliosikilizwa upande mmoja (wao pekee bila wajibu maombi kuwepo mahakamani).

Shauri hilo namba 16604/2024 limefunguliwa mahakamani hapo na Lawrence Kimea, Mwinjuma Kondo na Twaha Uwesu dhidi ya Ally Musa Kamtande, ambaye ni mwenyekiti wa Tefa, Bodi ya Wadhamini wa Tefa na Kamati ya Uchaguzi ya Tefa.

Akitoa amri hiyo Jaji Bwegoge amesema kuwa kwa kuwa waombaji wamefungua shauri hilo wakiomba amri hiyo ya zuio la muda kutokufanyika kwa uchaguzi huo, ambayo mahakama hiyo inaona kuwa ni ya haki katika maslahi ya haki kwamba waombaji wasikilizwe.

Amesema kuwa kwa kuzingatia kuwa kama wajibu maombi wataendelea na mchakato wa uchaguzi unaokusudiwa ambao ndilo jambo la msingi katika shauri la msingi lililopo mahakamani hapo, basi shauri hilo halitakuwa na maana.

“Mahakama hii inalazimika kutoa amri zinazoombwa za zuio la muda na kudumisha hali iliyopo kusubiri uamuzi wa shauri hilo kwa pande zote”, amesema Jaji Bwegoge na kuamuru:

“Wajibu maombi (kimahsusi mjibu maombi wa tatu, kamati ya uchaguzi) wanazuiwa kuendesha uchaguzi wa Chama cha Soka Wilaya ya Temeke (Tefa) uliopangwa kufanyika Agosti 4, 2024 au tarehe nyingine yoyote kusubiri uamuzi wa mwisho wa shauri hili kwa pande zote. Wakati huohuo wadaawa wanaamuriwa kudumisha hali iliyopo.”

Katika shauri hilo lililofunguliwa chini ya hati ya dharura, waombaji hao waliomba mahakama hiyo itoe amri ya zuio la muda la uchaguzi huo ulipangwa kufanyika tarehe hiyo au tarehe nyingineyo, kusubiri uamuzi wa mwisho wa shauri lao la msingi walilofungua mahakamani hapo.

Pia waliiomba mahakama hiyo iizuie kamati hiyo ya uchaguzi kuidhinisha utolewaji pesa za chama hicho katika akaunti ya benki namba 02282580007 iliyoko katika Benki ya Africa (BoA), tawi la Tandika, kusubiri kumalizika kwa shauri hilo.

Pamoja na mambo mengine Kimea na wenzake katika hati ya kiapo chao kilichounga mkono maombi hayo wamedai kuwa uchaguzi huo umepangwa kufanyika chini ya Katiba mpya ya chama hicho ambayo haijapitishwa na Mkutano Mkuu.

Hivyo wamedai kuwa jambo hilo linakinzana kabisa na Katiba yake ya mwaka 2009.

Pia wamedai kuwa Kamtande ambaye uteuzi wake haujathibitishwa na mkutano mkuu, aliwapendekeza wagombea kutangaza tarehe ya uchaguzi kuwa utafanyika Agosti 4, 2024 kinyume cha kanuni za uchaguzi wa chama hizo ambazo zinataka taarifa ya uchaguzi kutolewa ndani ya siku 40.

Zaidi wamedai kuwa bodi ya wadhamini wa Tefa kinyume na kanuni za uchaguzi, imeweka ada kwa wagombea zaidi ya kiwango kilichobainishwa na kanuni.

Hivyo Kimea na wenzake wamedai kuwa wakiwa wanachama watanyimwa haki yao ya kushiriki katika mchakato wa upigaji kura ambao ni haki yao ya kikatiba.

Vilevile wameelezea hofu yao kwamba fedha za chama hicho ambazo ni michango yao zitafujwa na kutumika vibaya katika mchakato wa uchaguzi ambao ni batili, jambo ambalo ni kinyume na maslahi yao na malengo ya chama hicho.

Wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa, wakili wa waombaji hao, Mayenga ameieleza mahakama hawakuweza kuwapatia wajibu maombi hati ya maombi kutokana na ofisi zao kuendelea kufungwa mpaka mchana wote.

Pia wakili Mayenga amedai kuwa Katibu mjibu maombi wa pili (bodi ya wadhamini Tefa) alikataa kupokea hati ya wito wa mahakama kwa ajili ya kwenda kusikiliza maombi hayo.

Sambamba na maelezo hayo pia aliwasilisha mahakamani kiapo cha mpeleka nyaraka wa mahakama hapo kama ushahidi wa katibu huyo kukataa kupokea wito huo.

Hivyo akaiomba mahakama hiyo amri ya muda dhidi ya wajibu maombi, hususan mjibu maombi wa tatu, Kamati ya Uchaguzi, kutokuendelea na uchaguzi huo kwa tarehe hiyo kusubiri uamuzi wa shauri hilo.

Vilevile wakili Mayenga aliomba amri ya kuendelea kudumisha hali ilivyo kusubiri uamuzi wa maombi hayo

Mahakama hiyo baada ya kusikiliza hoja hizo imeridhika na kuamua kusikiliza maombi hayo na kutoa amri ya upande mmoja, bila wajibu maombi kuwepo.

Chanzo: Mwanaspoti