Mwisho wa msimu wa soka ni wakati wa msisimko mkubwa kwa timu zote za soka. Pia ni wakati wa kufanya tathmini ya wachezaji waliopo na wale ambao wataruhusiwa kuondoka klabuni bure.
Kila mwaka, kuna wachezaji wachache ambao wanakuwa huru. Baadhi yao wamekuwa nyota katika timu zao, huku wengine wakiwa bado hawajajiimarisha kama washindi kwenye vikosi vyao.
Makala haya yanawaangalia wanasoka watano ambao wamethibitisha ustadi wao mara kwa mara. Uzoefu wao na ustadi wao umewafanya kuwa wa thamani kwa timu zao, lakini wamepangwa kuwa wachezaji huru.
Hawa ni magwiji watano wa soka ambao mikataba yao itamalizika mwishoni mwa msimu huu...
#5. Marco Reus Nahodha wa Borussia Dortmund anayekabiliwa na majeraha, Marco Reus yuko katika miezi ya mwisho ya mkataba wake kule Signal Iduna Park. Winga huyo amekuwa mtumishi mwaminifu kwa klabu hiyo tangu ajiunge nayo akitokea Borussia Monchengladbach mwaka 2012, akikataa kuhamia Bayern Munich.
Reus amechangia kwa mabao manne na asisti tatu katika mechi 15 alizoichezea klabu hiyo msimu huu. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33, amekuwa na wakati mgumu na majeraha katika maisha yake ya soka, na kukaa nje kwa muda mrefu.
Reus anasemekana kuangaliwa na klabu kadhaa za Mashariki ya Kati, pamoja na Al-Nassr ya Saudi Arabia.
Reus ameichezea Borussia Dortmund zaidi ya mechi 300 katika miaka yake 11 katika klabu hiyo. Winga huyo sasa anaweza kuchukuliwa kuwa ni ziada kwa mahitaji katika klabu na anaweza kuwa njiani kuondoka kama mchezaji huru Julai mwaka huu.
#4. N'Golo Kante Baada ya miaka saba Chelsea, huenda ukawa wakati wa N'Golo Kante kuiaga klabu hiyo.
Kiungo huyo wa kati wa Ufaransa, aliimarisha nafasi yake kama mmoja wa wachezaji bora zaidi ulimwenguni katika nafasi yake wakati akiwa Stamford Bridge. Hata hivyo, Kante amekuwa na wakati mgumu kubaki fiti katika misimu ya hivi karibuni akiwa Chelsea na hajaichezea klabu hiyo tangu Agosti mwaka jana.
Kante alishinda taji la Ligi Kuu England akiwa na Chelsea katika msimu wake wa kwanza na klabu hiyo na pia ameisaidia kunyanyua Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Umiliki mpya wa Chelsea unaonekana kujenga timu ya soka ya vijana wenye vipaji na Kante akiwa na umri wa miaka 31, hawezi kuonekana kuwa kijana.
Mazungumzo juu ya mkataba mpya yamekwama. Kante bado anafanya kazi ya kurejea Stamford Bridge kabla ya uamuzi wake kuhusu hatima yake kufikiwa. Pande zote mbili zinasemekana kuunga mkono kuendelea na uhusiano wao ikiwa tu masharti sahihi yatatimizwa. Kiungo kama Kante atakuwa na klabu nyingi zitakazomwania kama mchezaji huru.
#3. Luka Modric Mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or mwaka 2018 na kiungo wa kati wa Real Madrid, Luka Modric yuko katika tafrija ya maisha yake ya soka.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37, mkataba wake Santiago Bernabeu unamalizika Juni mwaka huu na hakuna dalili zozote za kuongeza muda wake wa kubaki katika klabu hiyo. Modric anasalia kuwa miongoni mwa viungo bora zaidi duniani licha ya umri wake.
Licha ya umri wake, Modric ameichezea Real Madrid mara 26 msimu huu katika michuano yote. Kiungo huyo mkongwe amekuwa katika klabu hiyo tangu mwaka 2012 na amepata mafanikio makubwa klabuni hapo.
Modric alitia saini mkataba mpya katika klabu hiyo mwaka 2020 baada ya kudaiwa kuhamia Inter Milan. Kiungo huyo sasa anaweza kuchukuliwa kuwa amepita kiwango chake bora na huenda asipewe nafasi ya kuongezwa tena.
Real Madrid wameripotiwa kumtaka Modric kustaafu soka la kimataifa ikiwa ana nia ya kuendelea kuitumikia klabu hiyo.
Nahodha huyo wa Croatia, Modric alitangaza nia yake ya kuendelea na timu ya taifa baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu nchini Qatar. Katika miezi ijayo, Real Madrid na Modric wataamua iwapo wataendelea pamoja au kuachana.
#2. Karim Benzema Mshambuliaji wa zamani wa Ufaransa, Karim Benzema aliandika jina lake kwenye vitabu vya historia aliposhinda tuzo ya Ballon d'Or mwaka 2022.
Nahodha huyo wa Real Madrid amekuwa na maisha mazuri katika klabu hiyo, lakini wakati wake unaweza kuwa unakaribia mwisho. Amepambana na majeraha msimu huu, akicheza mechi 19 pekee na kufunga mabao 12.
Benzema alijiunga na Real Madrid mwaka 2009 na amewashinda Gonzalo Higuain, Alvaro Morata na Luka Jovic ili kusalia kuwa muhimu katika klabu hiyo.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 35, amepata hadhi ya kuwa maarufu Santiago Bernabeu na huenda anatafuta kuondoka katika klabu hiyo. Amecheza soka lake bora katika rangi za 'Los Blancos' hao.
Real Madrid walitumia euro milioni 60 kumsajili kinda wa miaka 16 kutoka Brazil, Endrick kutoka Palmeiras.
Mshambuliaji huyo ambaye atajiunga na klabu hiyo atakapofikisha umri wa miaka 18, anaonekana kuwa mbadala wa muda mrefu wa Benzema. Miezi ijayo itakuwa muhimu katika kutoa ufafanuzi wa wazi wa mipango ya klabu kwa Benzema.
#1. Lionel Messi Lionel Messi alisaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Paris Saint-Germain kutoka Barcelona mwaka 2021.
Nyota huyo wa soka wa Argentina amefurahia muda wake wa kukaa Paris, lakini anaonekana kuwa na wasiwasi kuhusu kuongeza mkataba wake katika klabu hiyo. Aliiongoza nchi yake kwa mafanikio kushinda Kombe la Dunia la mwaka 2022 na uvumi umeenea juu ya mustakabali wake.
Messi amekuwa mmoja wa wachezaji waliochangia vema PSG msimu huu, akiwa amefunga mabao 10 na kutoa pasi za mabao 10 kwenye Ligue 1. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35, anasemekana kuwa ametulia kuhusu hali ya mkataba wake klabuni hapo, lakini hakuna dalili zozote kama atasaini.
Tangu Kombe la Dunia, imekuwa ikikisiwa sana kwamba amepokea ofa kutoka kwa David Beckham anayemiliki klabu ya Inter Miami inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani, MLS.
Kurejea Barcelona pia kumekuwa na uvumi, ingawa anasemekana kutokuwa na maelewano mazuri na rais, Joan Laporta.
Messi amewahi kuchezea klabu mbili tu katika maisha yake ya soka. Kuna uwezekano kwamba atarejea Argentina kuchezea Newell's Old Boys, klabu yake ya utotoni, mwishoni mwa maisha yake ya soka.
Mshindi huyo mara saba wa Ballon d'Or ana miezi michache kuamua ni wapi anakusudia kutumia maisha yake ya baadaye.