Beki wa Manchester United, Harry Maguire amedai kuwa ataendelea kucheza mechi nyingine zinazofuata baada ya kuanzishwa kikosini kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Leeds United wikiendi iliyopita.
Maguire alicheza mechi yake ya tano ya ligi tangu msimu ulipoanza Man United ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Elland Road.
Beki huyo alisema licha ya kukosa nafasi nyingi za kucheza chini ya kocha Erik ten Hag, anaamini atacheza katika kikosi cha kwanza ingawa mashabiki wanamponda kutokana na kiwango chake msimu huu.
“Hata kama nikicheza au sitacheza nataka timu ipate matokeo mazuri na kufanikiwa. Tumekuwa na msimu mzuri mpaka sasa tulipofikia. Kuna mengi ya kuboresha na kuimarika zaidi tutakapocheza na timu kubwa. Nimefurahi tumepata matokeo mazuri hapa ugenini (juzi dhidi ya Leeds United), mechi ilikuwa ngumu, kila mtu alifahamu ubora wetu ungetupa ushindi tusonge mbele,” alisema Maguire.
Beki huyo amepitia kipindi kigumu akiandamwa na mashabiki - wengi wakidai hastahili kuichezea Man United kutokana na kiwango kibovu.
Nafasi ya Maguire kikosini ilikuwa hatarini tangu Ten Hag alipomsajili Lisandro Martinez kutoka Ajax katika dirisha la usajili la kiangazi lililopita.
Mara nyingi Ten Hag anawapanga Martinez na Raphael Varane kwenye safu ya ulinzi ya kati huku Maguire akisugua benchi. Hata hivyo beki huyo hana presha kuhusu hilo.
Maguire alisajiliwa na Man United kwa rekodi ya usajili iliyogharimu kitita cha Pauni 80 milioni akitokea Leicester City mwaka 2019.
Beki huyo wa kimataifa wa England alikiwasha alipokuwa akikipiga Leicester lakini tangu alipotua Old Trafford mambo yamekuwa tofauti.