Wanasimba mpo? Mtendaji mkuu wa zamani wa Simba, Crescentius Magori amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kusema hakuna safari isiyokuwa na mabonde wala miinuko, huku akiwahakikishia kuwa bado rais wa heshima, Mohamed Dewji yupo 'kamili gado' kuendelea kusukuma gurumudu.
Hali ndani ya Simba sio swali, wadau na mashabiki wa timu hiyo wanaonekana kugawanyika kufuatia kufanya vibaya kwa timu hiyo huku wakionyesha wazi kutokuwa na imani na baadhi ya viongozi wao.
Magori ambaye ni mshauri wa Dewji ametumia jukwaa la mitandao ya kijamii kuandika ujumbe mrefu ambao umekuwa na mapokezi tofauti kwa mashabiki wa timu hiyo ambayo siku chache zilizopita ilitolewa katika Kombe la Shirikisho (FA).
"Safari ya Simba mpya ilianza mwaka 2018, safari ambayo mpaka sasa haijakamilika! Mategemeo ya kila Mwana-Simba ni kuwa baada ya mabadiliko ya katiba ya mwaka huu (2024) Januari, Serikali itakamilisha mchakato huo hivi karibuni," ujumbe huo uliendelea kwa kusema;
"Katika kipindi hiki cha miaka 6 ya Simba mpya, timu imepiga hatua kubwa kimaendeleo kama ifuatavyo; 1. Kutoka katika timu isiyojulikana ni ya ngapi Afrika (unranked) mpaka namba 5 Afrika, 2. Kutoka bajeti ya sh 3bilioni mpaka bajeti ya zaidi ya Sh20 bilioni.
"3. Timu imechukua ubingwa wa Tanzania mara nne, 4. Ubingwa wa FA mara tatu, 5. Ngao ya jamii mara nne, 6. Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara nne, 7. Robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mara moja 1, 8. Ushiriki wa African Football league katika timu nane bora bora Afrika, 9. Viwanja vyake vya mazoezi."
Magori hakuishia hapo, ameendelea kwa kusema,"10. Timu ya wanawake Simba Queens kuchukua ubingwa mara tatu, 11. Timu ya wanawake Simba Quee na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa Wanawake Afrika."
Mafanikio amesema mafanikio hayo katika kipindi cha miaka sita siyo madogo kwa namna yoyote ile huku akidai hakuna timu yoyote Tanzania iliyowahi kufikia mafanikio hayo.
"Hongera Mo Dewji, Bodi ya Simba na Menejimenti ya Klabu, Walimu, Wachezaji na kila Mwana-Simba. Nafahamu hamu ya Wanasimba ni kurudisha Ufalme wetu hapa nyumbani na kuvuka hatua ya robo fainali kwenye michuano ya CAF. Ndoto hizi haziwezi kufikiwa kwa mabishano, mvurugano na ugomvi bali kwa kukaa chini na kujipanga kimkakati.
"Naomba niwahakikishie baada ya mazungumzo na Rais wa Heshima wa Klabu Mohamed Dewji naomba niwatoe hofu kuwa Mo hajawahi kuiacha Simba na hataiacha Simba na kuanzia sasa atashirikiana na uongozi kujipanga upya kurudisha heshima ya Simba na kuzidi kuimarika."
Ujumbe huo aliutamatisha kwa kusema,"Tuachane na kelele za mitandaoni, tuwe nyuma ya timu yetu! Simba imara inakuja."
WASIKIE WADAU
Kupitia chapisho hilo, wadau mbalimbali wa Simba wameibuka kwenye uwanja wa kutoa maoni na kuonyesha matumaini yao.
Amosamweli; "Walau ww tutakusikiliza, ila Mangungu, Salim na Kajula hao hapana kwakweli. #NguvuMoja."
Max_peter_albert; "Mi huwa sijui wala sioni umuhimu wa kuanza kufight kwa kusema timu haijafanya vizuri naamin good things take time hofu ya nn #nguvumoja✊????."
Kelvinthekop; "Wewe ndo miongoni mwa watu ambao tunawapenda ndani ya Simba lakini hatukuoni sana ndo maana tunahisi kuna mgogoro maana hiyo Simba unayoisema iliyotawala wewe ulikua mstari wa mbele na Barbra pamoja na the late Hanspope. Kama vipi turudishieni Barbra kwenye uongozi tunataka matokeo na usimamizi imara Simba kwa sasa tumeyumba kwenye uongozi."
Nzalalilah; "Umesahau kuandika kibegi na WhatsApp Channel, mnatufanya sisi hatuna akili. Timu haipati matokeo mazuri, viongozi mnatuletea siasa za mpira. Shame on you.