Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mageuzi ya majina ya Simba, Yanga mikoani 1972

Simba Jina.jpeg Mageuzi ya majina ya Simba, Yanga mikoani 1972

Mon, 20 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Siyo kila mtu anajua hili. Kwa maana hiyo ni vigumu kwa mtu mwingine kuweza kukupa undani wa habari hizi.

Mageuzi ya majina ya timu yaliyosimamiwa na Makamu wa Rais, Hayati Abeid Amaan Karume kabla hajafiriki dunia kwa kupigwa risasi mwaka 1972.

Baada ya nchi za Tanganyika na Zanzibar kupata uhuru na kuungana mwaka 1964, Makamu wa Rais, Karume akaona kulikuwa hakuna tena umuhimu wa kuyatumia majina ya kizungu, yaliyokuwa na nasaba na ukoloni. Kiongozi huyo akapitisha azimio la kuondokana na majina hayo.

Hivyo, timu nyingi zilibadili majina na kurudi katika majina ya asali yaliyobeba uzalendo. Ikumbukwe nchi ilikuwa imetawaliwa au kugawanyika katika pande kuu mbili na klabu mbili kubwa, yaani Sunderland na Young African.

SIMBA NA YANGA

Sunderland na Young African ndizo zilizokuwa timu za kwanza kuathirika na azimo hili, ingawaje inaoekana Sunderland ndiyo iliyoathirika zaidi. Timu hiyo ilibadili jina lake kwa kiasi kikubwa na kuitwa Simba. Hatua hii iliifanya ibaki na SSC yake. Yaani Sunderland Sports Club na kuwa Simba Sports Club.

Young African ikawa Yanga kutokana na matamshi, ingawaje jina hilo la Young African lililoanza kutumika mwaka 1935 linaendelea mpaka leo hii kwenye mabango ya klabu hiyo.

Jina hilo lilionekana kukaa kizalendo zaidi ndio maana halikuwa na shida kuandelea kutumika. Kabla ya hapo kulikuwa na timu iliyokuwa ikiitwa Jangwani na ilikuwa ikivaa jezi za rangi za pundamilia, nyeupe na nyeusi baadaye ikawa Young African.

TIMU NYINGI ZILIATHIRIKA

Baadhi ya timu zilizokuwa zikitumia majina ya Young African na Sunderland za mikoani zililazimika kubadilisha majina yao. Pale Ifarakara, Morogoro kulikuwa na timu iliyokuwa ikiijita Sunderland, na nyingine ikijiita Young African.

Sunderland ya Ifakara ikabadili jina na kujiita, Shupavu na Young African ya mjini hapo ikatumia jina la Asante Afrika.

Kitu cha ajabu ni kwamba, Cosmopolitan ya Dar es Salaam haikubadili jina lake lakini Cosmopolitan ya Morogoro mjini ilibadili jina na kuitwa Mseto.

Hii ndiyo timu iliyowatoa wachezaji mahiri kama kina Omary Hussein ‘Keegan’, Charles Boniface Mkwasa, Hussein Ngulungu, Aluu Ally, Shilingi na wengine wengi.

TOTO AFRICA IMO

Young African ya Mwanza ndio ikabadili jina na kujiita Toto Africa na Sunderland ya Mwanza ikawa Nyamaume. Pia, kule Lindi kulikuwa na Young African nyingine ambayo nayo ilibadili na kujiita Nchi Yetu, hapa ndipo alipotoka mchezaji wa zamani wa Yanga na Pan Africa, Muhaji Muki.

Sunderland ya Lindi nayo ikajiita Nguvu Moja. Hapo utakubaliana nami kwa kuwa Simba inatumia slogani yake ya Nguvu Moja.

VIPI KUHUSU ZANZIBAR

Zanzibar kulikuwa na timu iliyokuwa ikiitwa African Sports ikiwa na itikadi za Young African nayo ikajikuta ikibadilisha jina na kujiita Miembeni na ile iliyokuwa ikijiita Sunderland ikabaili jina na kujiita Kikwajuni.

Mabadiliko haya yaliifanya hata Liverpool ya Ilala kubadili jina na kujiita Ashanti na baadaye Ashanti United. Mtwara kulikuwa na timu iliyojiita Yaunda ambayo ilikuwa ni timu yenye nasaba na Yanga na Safari iliyokuwa na uhusiano na Simba. Hata jijini Dar es Salaam pale Temeke kulikuwa na timu iliyoiitwa Goodhope ikiwa na uhusiano na Simba na Temeke Squad ikiwa na urafiki na Yanga.

Enzi hizo timu hizi zilipomuona mchezaji mzuri wa kiwango cha kucheza Ligi Kuu (zamani Ligi Daraja la Kwanza), ilikuwa lazima viongozi wake wawasiliane na mabosi wa Simba na Yanga ili akacheze huko.

KUHUSU COASTAL NA SPORTS

Watu wengi wanachanganya mabadiliko haya na kuzihusisha timu za Coastal Union na African Sporst za Tanga.

Timu za mikoani na wilayani nilizozitaja huko juu zilikuwa ni matawi ya Simba na Yanga kasoro Coastal na African Sports.

Timu hizi za Tanga zilikuwepo kipindi cha azimio la kubadili majina na ziliendelea na majina yao hayo hadi leo hii.

Coastal Union na African Sports ni marafiki tu wa Simba na Yanga, hazijawahi kuwa matawi ya timu hizo za Dar es Salaam.

Ni kama kulikuwa na makubaliano fulani ya baadhi ya viongozi yaliyosababisha timu hizo nazo kuingia katika athari za Usimba na Uyanga.

Ndio maana leo hii Coastal Union inatumia jezi nyekundu na nyeupe na African Sports ikitumia jezi zinazofanana na Yanga.

MAHADHI NA YANGA BWANGA

Ukitaka kuona timu hizo hazikuwa matawi ni jinsi wachezaji wa timu hizo walivyoweza kuzitumikia Simba na Yanga.

Laiti kama ingekuwa Sports ni tawi la Yanga, isingewezekana kwa kipa bora wa Afrika mwaka 1973, Omary Mahadhi ‘Bin Jabir’ kutoka Sports na kujiunga na Simba.

Ingekuwa vigumu kwa wachezaji kama Yanga Bwanga, Elisha John na Joseph Lazaro na Juma Mahadhi kutoka Coastal Union na kujiunga na Yanga. Hivi karibuni beki Bakary Nondo Mwamnyeto naye alitua Jangwani.

Ukiangalia Yanga imenufaika na Coastal Union kuliko Simba. Kwa miaka ya sasa siyo ajabu kumuona shabiki wa Coastal Union akishabikia Yanga na shabiki wa African Sports akiishabikia Simba.

Chanzo: Mwanaspoti