Siku zinavyokwenda michezo inakuwa na ushirikishi mkubwa na hivyo kuwa kiwanda kinachoingiza mapato na kutoa ajira nyingi kuliko sekta na viwanda kama tulivyozoea.
Mathalani, katika mpira wa miguu kuna watumishi wengi wanaomwezesha mchezaji wa soka kufika uwanjani na kuonyesha kile anachokijua mbele ya mashabiki 50,000 au zaidi.
Sayansi za uchumi, lishe, tiba na hata akili bandia sasa zimekuwa sehemu ya maendeleo ya mpira wa miguu.
Kuongelea maendeleo ya mpira wa miguu na mafanikio katika mashindano ni sawa na kuongelea maendeleo ya kilimo na mafanikio katika gulio la chakula.
Ni sawa na kuongelea kinachoendelea katika tasnia ya kilimo dhidi ya kinachoendelea katika masoko ya Kariakoo, Tandale, Nyuki, Soko Jipya na mengine yanayouza vyakula kama yalivyotapakaa Dar es Salaam na miji mikubwa nchini.
Hivi karibuni kumekuwa na mafanikio makubwa katika Ligi Kuu Bara kwa kulinganishwa na nyingine za mataifa ya Afrika.
Mtandao mmoja wa kimataifa umeitaja Ligi ya Bara kama moja kati ya ligi tano bora Afrika. Hayo si mafanikio madogo hasa kwa nchi iliyo Kusini mwa Jangwa la Sahara nje ya Afrika ya Kusini. Kana kwamba hiyo haitoshi, klabu zinazotokea katika Ligi Kuu Bara (hasa Simba na Yanga) zimewekwa miongoni mwa klabu 20 bora kabisa Afrika.
Kwa sasa Simba ni miongoni mwa timu nane waanzilishi wa mashindano mapya ya Ligi ya Afrika (African Football League), huku klabu hizo mbili zikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu uliopita. Simba imekuwa mwenyeji katika hatua za makundi na robo fainali za mashindano ya klabu barani humo, huku Yanga ikifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.
Ligi Kuu tayari imechezwa mechi mbili lakini unaweza kuona namna klabu hata zile zinazoitwa ndogo kama Kitayosce au Tabora United zikiwa zimesheheni wachezaji mahiri hasa wa kigeni. Timu ya taifa inaitwa kuelekea Algeria naangalia kikosi kwa kulinganisha na mataifa mengine hata majirani zetu Uganda, nahisi bado sisi ni madalali wa Kariakoo na hatujawekeza vya kutosha mashambani. Hatuna wigo mpana wa uchaguzi wa wachezaji wa timu ya taifa. Kwa maana nyingine hatujafanya vya kutosha katika maendeleo ya soka.
Hapo juu ni maendeleo makubwa kwa ngazi ya klabu kama nilivyoonyesha hapo awali. Hata hivyo, ligi yetu na klabu zetu zimekuwa kama mlaji wa mazao ya Kariakoo; anauza asichozalisha. Ligi yetu ni bora, sawa lakini tunazalisha wachezaji wa kutosha kuilisha ligi ili iendelee kuwa bora? Je, tunazalisha makocha wengi wenye viwango kuitosheleza ligi yetu? Madaktari je? Wataalamu wa lishe? Watawala? Masoko na habari? Naamini sehemu kubwa ya majibu yatakuwa ni HAPANA.
Jibu hilo ndilo linaturudisha kwenye ukweli kuwa tumewekeza zaidi katika gulio (matukio/mashindano) kuliko shambani (maendeleo).
Lala uamke ukutane na tangazo kwamba wachezaji wa kigeni kwenye Ligi Kuu wamepunguzwa idadi kwa kila klabu; je, ligi yetu itakuwa ileile? Walimu wa kigeni wakipunguzwa au wataalamu wa viungo je, Jibu linarudi palepale kwamba hatujawekeza vya kutosha katika maendeleo endelevu. Angalia viwanja vyetu mikoani na mitaani nje ya vile vinavyochezewa Ligi Kuu, utaumia sana. Viwanja havina viwango vya kusaidia vijana wadogo kujifunza mpira kisayansi maana kuna vichuguu, mabonde, majaruba n.k.
Maendeleo ya soka yanaanza na uzalishaji wa wachezaji kwa maana ya soka la vijana. Taifa lolote haliwezi kusema linafanya maendeleo endelevu ya soka na hata michezo mingine kama halina miradi na miundombinu ya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya vijana. Klabu zinazonunua wachezaji bila kuzalisha wachezaji zina maendeleo bandia ambayo yanaweza kuondoka wakati wowote.
Duniani kote hakuna klabu iliyofanikiwa kuzalisha wachezaji wote inaowataka lakini siku zote uti wa mgongo wa mafanikio ya klabu ni wachezaji na hata wataalamu waliokulia katika mpango wa klabu husika.
England imekuwa na ligi tajiri na inayovutia vipaji kutoka pande zote za dunia, labda kuliko ligi yoyote ya Ulaya. Ligi Kuu ya England ndio inayoonekana sana kwenye televisheni huku ikiingiza mabilioni ya fedha. Hata hivyo, kwa kipindi kirefu timu zake za taifa kuanzia vijana hadi ile kubwa zilikuwa hazifanyi vizuri. Waingereza waliziangalia kwa wivu timu za mataifa kama Ufaransa, Uhispania na Ujerumani zilizokuwa zinafanya vizuri. Siri ya wenzao ilikuwa ni uwekezaji katika maendeleo kuliko mashindano. Hadi hivi karibuni England ilikuwa ni mnunuzi mkubwa wa wachezaji lakini ikiwa haiuzi wachezaji nje. Hali ilikuwa mbaya, hata upande wa wataalamu wengi walikuwa wa kigeni kiasi cha timu ya taifa kufundishwa na Mswidishi, Sven- Goran Eriksson na Mtaliano, Fabio Capello jambo ambalo si utamaduni wa mataifa yaliyoendelea kisoka.
Baada ya kugundua umuhimu wa kuwekeza katika maendeleo sasa soka la England linaanza kuonekana kwa timu zao za vijana na wanawake kufanya vizuri kimataifa. Timu ya taifa inafanya vizuri chini ya kocha mzawa aliyetokea kwenye kufundisha timu za vijana, Gareth Southgate. Chama cha Soka cha England (FA) kimedhamiria kuwekeza katika maendeleo kiasi cha kukaribia kuuza uwanja maarufu wa Wembley ili kupata fedha za maendeleo.
Hapa kwetu ni jukumu la mamlaka za mpira na hata wizara inayohusika na michezo kuwekeza na kuweka sera zaidi katika maendeleo ili kuendana na kasi ya uwekezaji katika matukio. Ukiangalia viwango vya Fifa wastani wa viwango vya Tanzania kwa timu ya taifa ya soka ya wanaume ni nafasi ya 125 duniani na nafasi zaidi ya 30 Afrika huku tukiwa na ligi bora na klabu bora.
Ni kama kuvaa suti na kandambili. Tunatakiwa kuwekeza katika vijana, wataalamu na miundombinu ya kutosha wakati soko linapatikana hapa nyumbani. Tunatakiwa kukimbia wakati wenzetu wanatembea.