Klabu ya Real Madrid itakata rufaa ya kadi nyekundu ya Jude Bellingham dhidi ya Valencia, vyanzo viliiambia ESPN.
Kiungo huyo wa kati wa England alitolewa nje baada ya kipenga cha mwisho cha sare ya mabao 2-2 mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Valencia kwa madai ya kumtukana mwamuzi.
Ripoti ya mwamuzi ilidai Bellingham alionesha tabia ya uchokozi na akapiga kelele mara kwa mara "ni bao letu."
Bellingham ilipiga mpira kwa kichwa akiunganisha krosi ya Brahim Diaz na ulitinga wavuni, lakini mwamuzi Jesus Gil Manzano alipuliza kipenga cha kumaliza mchezo wakati mpira ukiwa angani katika dakika ya tisa ya muda wa nyongeza katika kile ambacho kingekuwa ni ushindi kwa Madrid.
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, alisisitiza baada ya mchezo huo kuwa Bellingham hakumtukana mwamuzi. "Tulichukizwa na kadi nyekundu ya Bellingham," alisema Ancelotti.
"Hakusema matusi yoyote. Alisema kwa Kiingereza ni goli, lakini alikuwa akisema kile ambacho sote tulikuwa tukifikiria. Mwamuzi aliruhusu mchezo uendelee.
Nadhani makosa. Bellingham alikuwa wazi katika kile alichosema. "Alikuwa na hasira katika majibu yake, lakini hiyo ni kawaida, baada ya kile kilichotokea. Haikuwa tusi, hata kidogo."