Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madogo wanaokiwasha WPL

WPL Madogo wanaokiwasha WPL

Sat, 6 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Kuu ya Wanawake (WPL) inaendelea kuwa na mvuto wa kipekee huku kila timu ikipambana kuhakikisha inafanya vizuri.

Timu 10 zimekuwa zikiundwa na wachezaji wa aina mbalimbali wadogo kwa wakubwa, wenye uzoefu na wapya, wenye vipaji na wale wa kawaida, wote unawakuta humo.

Msimu huu kuna wachezaji wachanga ambao wamepata nafasi ya kucheza na kuonyesha kiwango bora na wamekuwa tishio.

Mwanaspoti limekuchambulia baadhi ya mabinti wadogo ambao wamepata nafasi ya kucheza kwenye timu na kuonyesha matokeo chanya na kama wataendelea hivyo basi huenda tukawaona wakitua katika nchi mbalimbali kukiwasha.

1. WINIFRIDA GERALD (JKT QUEENS)

Kwa mujibu wa mtandao wa Soccerway, kiungo mshambuliaji, Winifrida Gerald hadi sasa ana miaka 16, bado ni binti mdogo lakini amekuwa akifanya makubwa kwenye ligi ya wanawake.

Msimu uliopita alikuwa na Fountain Gate Princess na kuisaidia timu hiyo kumaliza ndani ya nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa WPL.

Kwa sasa yupo na wanajeshi JKT Queens na amekuwa na kiwango bora kwa kuisaidia timu hiyo eneo la ushambuliaji akiweka kambani mabao saba kwenye mechi tisa.

Msimu wa kwanza akiwa na JKT pamoja na kuwa na wachezaji bora na kikosi kizuri lakini binti huyo mdogo ameonekana kukubalika na kocha Ester Chabruma ambaye tangu atue ameingia kwenye kikosi cha kwanza moja kwa moja.

Ujio wa Winifrida umeongeza ushindani katika kikosi eneo la ushambuliaji la JKT ambalo wanacheza Stumai Abdallah, Jamila Rajabu na Amina Bilal ambao ni wachezaji bora wa muda wote WPL.

2. NOELA LUHALA (YANGA PRINCESS)

Ndio mzawa tegemeo kwenye eneo la beki wa kati wa Yanga Princess na timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 18.

Ubora wake kwenye eneo la ulinzi unaifanya Yanga Princess kubaki salama na kwenye ligi timu hiyo imeruhusu mabao tisa ikiwa kwenye orodha ya timu zilizoruhusu mabao machache baada ya JKT kutikiswa mara nne na Simba mara tano.

Mbali na hivyo aliwahi kuisaidia timu ya Serengeti Girls kubeba ubingwa wa CECAFA mwaka jana kwa kuitoa Uganda kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Si hapo tu msimu wa 2022 aliisaidia Tanzania kufika robo fainali ya michuano ya FIFA U-17 Women’s World Cup akiwa kama nahodha.

3. ASHA MNUNKA (SIMBA QUEENS)

Unaweza kusema huu ni msimu wake bora akiwa na Simba Queens kutokana na kiwango bora alichokionyesha kwenye mechi za Ligi Kuu.

Mabao 11 aliyofunga msimu huu yamemfanya kocha wa timu hiyo, Juma Mgunda kumuamini na kumpa nafasi ya kucheza ambayo kwa asilimia kubwa ameonekana kuifanyia kazi kwa kuwa anapopata nafasi ya kufunga anafanya hivyo.

Wakati anajiunga na Simba msimu wa 2021 akitokea Alliance Girls alikutana na upinzani wa kina Asha Djafar, Opah Clement, Mwanahamis Omary ‘Gaucho’ ambao walikuwa bora na kumfanya akae benchi.

Msimu huu ni kama Djafar na Gaucho hawana makali yale na Opah yuko nchini Uturuki akiitumikia timu yake ya Besiktas, hivyo usukani ni wake Mnunka na anampa wakati mgumu Mkenya Jentrix Shikangwa ambaye msimu uliopita alikuwa mfungaji bora na mabao 17.

4. HASNATH UBAMBA (FOUNTAIN GATE PRINCESS)

Haimbwi sana na hii inatokana na timu anayocheza pengine kutokuwa na wingi wa mashabiki ukifananisha na Simba au Yanga.

Kiraka huyo ana uwezo wa kucheza kama winga, kiungo mshambuliaji na hata kiungo, vyovyote tu kocha atampanga na kumpa majukumu.

Ndio mchezaji tegemeo hasa eneo la ushambuliaji baada ya Winifrida kwenda JKT hivyo ana jukumu la kuhakikisha timu hiyo inafunga mabao.

5. HUSNA MTUNDA (YANGA PRINCESS)

Ukimtoa kipa namba moja wa Yanga Princess, Safiatu Salifu anayefuata Husana Mtunda ambaye amekuwa akifanya vizuri kwenye timu hiyo na timu ya taifa ya wanawake Serengeti Girls na Tanzanite.

Achana na kipa namba moja wa timu ya taifa ya Twiga Stars, Naijat Abbas anafuata Husna ambaye kwenye kikosi cha Yanga hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara lakini ana uwezo mkubwa wa kudaka. Kipa huyo aliyezaliwa Mei 31, 2005 amekuwa mmoja ya wachezaji chipukizi wanaokiwasha katika Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) japo amekuwa akisubiri kwa Safiatu.

Kama hujui, kwa sasa Simba na Yanga makipa namba moja wote wanatoka nje, hivyo kuwapa nafasi baadhi ya makipa wa ndani kujifunza kutoka kwao na kuzitumikia timu za taifa za Tanzania.

6. ALIA SALUM (JKT QUEENS)

Kwa mujibu wa mtandao wa Playermarket, kiungo mshambuliaji wa JKT Queens, Alia Salum ana miaka 17.

Umri wake na kimo chake unaweza kumwita ‘kiberenge’ kutokana na spidi yake lakini kubwa zaidi ni ana uwezo wa kukaba na kupeleka mashambulizi kwa timu pinzani.

Hapati muda mwingi wa kucheza kutokana na upinzani uliopo eneo analocheza kwani wapo kina Stumai, Winifrida na Donisia Minja na kumfanya kocha ambadilishe eneo hilo na kumchezesha kama winga.

7. ESTER MASEKE (BUNDA QUEENS)

Ndio kwanza anachipukia kwa upande wa soka la wanawake na ndio msimu wa kwanza kucheza ligi.

Aliisaidia Bunda kupanda Ligi Kuu akiwa kama nahodha mwaka 2022 na kuibuka na tuzo ya mchezaji bora wakiibuka mabingwa wa mikoa.

Pamoja na umri wake mdogo ndio tegemeo Bunda na mara kadhaa ameitwa timu ya taifa ya wasichana.

Chanzo: Mwanaspoti