Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madogo hawa wameaminiwa Bara

Mzize Wa Annaba Na Kigali Na Fursa Zake Tatu Mkononi Madogo hawa wameaminiwa Bara

Wed, 22 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara imeendelea kuchanganya huku kila timu ikivuna ilichokipanda. Timu zote 16 zimekuwa zikipambana kuhakikisha zinapata matokeo chanya kwenye mechi zinazocheza lakini mwishowe dakika 90 za kila mchezo ndizo huamua matokeo.

Sahau kuhusu matokeo. Ligi hii inayokua kila uchao, timu zake 16 zimekuwa zikiundwa na wachezaji wa lika mbalimbali, wadogo na wakubwa, wenye uzoefu na wapya na wanaojua soka sana, kawaida na wengine ni unga unga mwana. Ndivyo soka lilivyo.

Ukiachana na yote hayo, kwenye Ligi Kuu msimu huu kuna madogo wamepata nafasi ya kuwa sehemu ya vikosi vya timu hizo 16 na usipowaona wakicheza, basi utawakuta kwenye benchi.

Hali hiyo inawaongezea kitu kwenye wasifu wao, inawapa uzoefu na kubwa zaidi ni sehemu ya wao kujiuza hivyo kama watafanya vizuri kwani Ligi Kuu inatazamwa pande zote za dunia na ni soko zuri kwa wachezaji kufikia ndoto zao.

Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea baadhi ya vijana wadogo, waliopata fursa ya kuwa kwenye timu za Ligi Kuu msimu huu na wameaminiwa huku wao pia wakifanya vizuri. Kama wakiendelea hivi milango yao ya kutoboa ipo karibu sana. Washindwe wao tu.

Lameck Lawi- Coastal Union

Huyu ni beki wa Coastal Union aliyeibuka mchezaji bora chipukizi msimu uliopita.

Hati yake ya kusafiria ‘Paspoti’ kwa sasa inaonyesha ana umri wa miaka 18, na ni miongoni mwa wachezaji wanaounga timu ya taifa ya vijana U-18.

Lawi amekuwa na mwendelezo mzuri ndani ya Coastal na katika timu za taifa za vijana, akiwa miongoni mwa wachezaji tegemeo wa timu zote hizo. Kama atakaza kamba, huenda akawa na safari njema kwenye maisha yake ya soka katika miaka ijayo.

Clement Mzize- Yanga

Huyu ni straika wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania na pastpoti yake inasomeka ana miaka 19.

Mzize alianza kuichezea timu kubwa ya Yanga msimu uliopita akipandishwa kutoka timu za vijana za Yanga.

Hata hivyo, Mzize hajamwangusha, Kocha Nassredine Nabi aliyemwamini na kumpandisha kwani amekuwa kwenye kiwango bora.

Hadi sasa ni mshambuliaji tegemeo katika kikosi cha Yanga na amekuwa akifanya vizuri kila akipata nafasi akiwa ametoa pasi za mabao tatu kwenye ligi na kama akikaza basi njia yake kutoboa ni nyeupe kwani yuko sehemu salama.

Hija Shamte ‘Pogba’ - Kagera Sugar

Huyu ni kiungo wa kati ambaye umri wake pia ni chini ya miaka 20, anayecheza Kagera Sugar na timu za taifa za vijana.

Pogba amekuwa na mwendelezo bora wa kiwango chake. Ni mingoni mwa viungo tegemeo wa kikosi cha Kagera Sugar hadi sasa kwenye ligi.

Ikiwa ni msimu wake wa kwanza Ligi Kuu, kijana huyu aliyekulia kwenye Akademi za Cambiasso na African Lyon ameonyesha mwanzo mzuri na kama ataongeza bidii na kuendelea kufanya vizuri, basi ni faida kwa taifa katika miaka ijayo.

Ladack Chasambi -Mtibwa Sugar

Huyu ni mchezaji bora wa Ligi ya Vijana katika misimu miwili iliyopita mfululizo.

Paspoti yake kwa sasa inaeleza ana umri wa miaka 19, na sasa amepandishwa kwenye timu kubwa ya Mtibwa na tayari kwa msimu huu ametoa asisti tatu kwenye ligi Kuu jambo lililomfanya kuitwa katika timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Ubora anaoendelea kuuonyesha Chasambi umezifanya timu vigogo za kariakoo, Simba na Yanga kutaka saini yake na kama ataendelea hivyo basi huenda akapata mafainikio makubwa katika safari yake ya soka.

Zidane Sereri - Dodoma Jiji

Huyu ni mshambuliaji wa Dodoma Jiji ambaye umri wake ni chini ya miaka 20.

Zidane alitambulishwa kwenye Ligi Kuu msimu uliopita na Kocha Melis Medo aliyempandisha kutoka timu za vijana.

Tangu amepanda timu kubwa, Zidane ameonyesha ubora wa hali ya juu na kugeuka kuwa mchezaji tegemeo wa timu hiyo katika eneo la ushambuliaji.

Kama atavuta soksi na kuendelea kucheza kwa ubora, muda wake wa kufurahia soka na kuweka rekodi unakaribia.

Mohamed Bakari-JKT

Huyu ni winga wa JKT Tanzania, ambaye Paspoti yake inamtambulisha ana umri wa miaka 19.

Mohamed ni mchezaji wa timu za taifa za vijana lakini pia aliwahi kupita Polisi Tanzania U-20.

Huu ni msimu wake wa kwanza Ligi Kuu baada ya kuaminiwa na Kocha Malale Hamsini aliyepanda naye kutoka Championship na sasa ni miongoni mwa mawinga kikosini hapo.

Kama ataendelea kuwa na nidhamu, bidii na hali ya kutaka kufanya vizuri zaidi njia yake kwa sasa iko salama kufikia mafanikio.

Nickson Kasami- Mtibwa Sugar

Huyu ni beki wa pembeni wa Mtibwa Sugar mwenye umri usiozidi miaka 20 akiwa amepandishwa msimu huu kutoka timu ya vijana.

Kassami msimu huu amekuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo katika ukuta wa Mtibwa akicheza kwa kiwango kizuri na kuonyesha ukomavu.

Kama mambo yasipombadilikia huenda kwa miaka ijayo akawa tegemeo kwa timu ya taifa ya Tanzania pia akapiga hatua zaidi kisoka.

Twalib Mohamed- KMC

Huyu ni beki kinda wa Azam FC anayecheza KMC kwa mkataba wa mkopo. Twalib umri wake ni chini ya miaka 20 na akiwa KMC anacheza timu zote kwa maana ya kubwa na ile ya U-20.

Ikiwa ni msimu wake wa pili kucheza Ligi Kuu lakini wa kwanza nje ya Azam iliyomlea, Twalib kwa sasa ni beki wa kikosi cha kwanza cha KMC.

Kocha mkuu wa KMC, Abdihimid Moallin ndiye alimuamini tangu kipindi anafundisha timu za vijana za Azam na alipokabidhiwa mikoba ya kuinoa KMC akamwomba kwa mkopo na sasa wawili hao wanategemeana.

Chanzo: Mwanaspoti